Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sh1.5 bilioni kujenga soko la ndizi Rombo

Ndiziiiiiiiiii Sh1.5 bilioni kujenga soko la ndizi Rombo

Sat, 27 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Serikali imetoa zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya la ndizi la Mamsera lililopo wilaya ya Rombo, Kilimanjaro ili kuhakikisha wakulima wa ndizi wilayani humo, wanapata sehemu ya uhakika ya kuuzia bidhaa hiyo.

Wakulima hao wa ndizi wamekuwa wakifikisha bidhaa hiyo sokoni na kulazimika kupanga chini pembezoni mwa barabara kutokana na ufinyu wa soko, hali ambayo imekuwa ni kero ya muda mrefu kwao.

Akizungumza na wakulima wa ndizi katika soko la Mamsera leo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema Serikali imedhamiria kuweka mazingira rafiki kwa wakulima kote nchini, ili kuhakikisha kila Mtanzania anafanya kilimo chenye tija.

Silinde amesema likikamilika, litakuwa na uwezo wa kukusanya ndizi tani 119,625 kwa kila gulio, ambapo kwa wiki hufanyika mara mbili.

Eneo ambalo kunajengwa soko la kisasa la ndizi, Mamsera, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.

"Tuipongeze halmashauri kwa ujenzi huu ambao umeanza hapa Mamsera, ni maamuzi mazuri na ni lazima tuwasaidie wakulima wetu hawa wa ndizi. Niwahakikishie fedha hizi zinakuja na tutamaliza ujenzi wa soko hili mapema ili wakulima wetu hawa waweze kulitumia soko hili kwa manufaa zaidi lakini kuingizia halmashauri yetu kipato," amesema Silinde.

Naye, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Godwin Chacha amesema tayari halmashauri imetoa fedha Sh70 milioni kwa ajili ya kuanza ujenzi huo ambao upo katika hatua za awali na kwamba kukamilika kwake kutaleta manufaa makubwa kwa wakulima wa ndizi wilayani humo.

"Mpaka sasa halmashauri tumeshatoa fedha za ndani Sh70 milioni kwa ajili ya ujenzi wa soko hili na Serikali imetutengea Sh1.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi huu wa soko la kisasa, hivyo tunategemea wakulima wetu wataweza kufanya biashara katika maeneo rafiki,"

Amesema soko hilo lilikuwa na changamoto ya ubovu wa miundo mbinu ambapo kwa sasa wameshatafuta ufumbuzi wake ikiwa ni pamoja na kujenga soko jipya na la kisasa.

Matilda Saria, mmoja wa wakulima wa ndizi, amesema soko hilo limekuwa na changamoto nyingi ikiwemo ya ubovu wa miundombinu, hali inayosababisha wafanye biashara katika mazingira ambayo sio rafiki.

"Kwa miaka mingi tumekuwa tukifanya biashara zetu za ndizi katika mazingira magumu licha ya kutozwa ushuru wa halmashauri. Miaka yote tumekuwa tukipanga ndizi barabarani kutokana na ufinyu wa soko,"amesema.

Chanzo: Mwananchi