Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali ya Tanzania yashauriwa kutenga shule zitakazofundisha sanaa

Serikali ya Tanzania yashauriwa kutenga shule zitakazofundisha sanaa

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeshauriwa kutenga walau shule nne za Sekondari kwa ajili ya kufundisha sanaa.

Sambamba na hilo, wizara ya elimu  itengeneze michepuo ya masomo ya sanaa kwa shule za sekondari ili wanaofaulu kidato cha nne waendelee na masomo ya sanaa kidato cha tano hadi sita.

Ushauri huo umetolewa jana Jumatatu Desemba 16, 2019 na mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Nahimiani katika utoaji tuzo kwa wanafunzi wa sekondari waliofanya vizuri katika masomo ya sanaa kwa mwaka 2017 na mwaka 2018 katika mtihani wa taifa.

Dk Nahimiani alisema kukosekana kwa shule za kufundisha wanafunzi masomo hayo kuanzia sekondari imesababisha wengi kuanza kuyasoma wakiwa chuoni jambo ambalo sio sahihi.

"Kuwepo kwa shule hizo kutasaidia wanafunzi wachache wanaodahiliwa vyuo vikuu kwa kozi ya masomo ya sanaa kuwa na uelewa mwepesi wakati wa masomo yao kama walivyo wenzao wanaojiunga kusomea uhandisi, uchumi, uhasibu na kozi nyingine," alisema.

Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Geofrey Mngereza alisema tuzo hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2017,lengo lake ni kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma sanaa.

"Ikumbukwe sekta ya sanaa imekuwa na mchango mkubwa katika nyanja ya kiutamaduni, kijamii na kiuchumi ambapo kwa takwimu za mwaka 2018/19 sekta hii imechangia asilimia 13.7 katika pato la taifa," alisema.

Kwa upande wao wanafunzi waliopewa tuzo akiwemo Anseline Mutashobya kutoka shule ya Sekondari Bukoba, alisema kuna haja jamii kuondokana na dhana ya kuona sanaa ni kuimba na kuchora tu kwani masomo hayo yaliwasaidia kuongeza ufaulu  katika masomo.

Juliana Ngondo kutoka shule ya Sekondari Alfagems ya mjini Dodoma, alisema wazazi wasiwazuie watoto wao wanapowaona wanapenda sanaa kwa kuwa ni masomo ambayo yanaweza kubadili maisha yao na familia kwa ujumla.

Chanzo: mwananchi.co.tz