Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Serikali, wadau wapata pigo kifo cha Mabera

8ae4e73ad32073e19bfbaf984419605c Serikali, wadau wapata pigo kifo cha Mabera

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

S ERIKALI na wadau wa muziki wa dansi wamesema kifo cha mwanamziki mahiri wa Msondo Ngoma Music band, Mzee Said Mabera ni pigo kwa tasnia ya muziki wa dansi nchini.

Mabera alikuwa gwiji wa ukung’utaji jitaa la solo tangu alipojiunga na bendi hiyo 1973 na hakuwahi kuhama hadi anafariki dunia juzi na kuzikwa jana, Goba, Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema kifo cha Mabera ni pigo kwa tasnia ya muziki wa dansi nchini kwa kuwa enzi za uhai wake alikuwa na mchango mkubwa na alizikonga nyoyo za mashabiki wake akiwa na bendi ya Msondo Ngoma.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mzee wetu Mabera mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi. Kwa hakika kifo chake ni pigo kubwa kwa tasnia ya muziki nchini kwa kuwa enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa katika kuendeleza na kuimarisha tasnia hii; “Natoa pole kwa familia na wanamuziki wote kwa msiba huu mzito na tunamuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu, ujasiri na moyo wa ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu,”

alisema Dk Abbasi. Naye mmoja wa shabiki wanaunda kundi la masenata wa bendi hiyo, Ahmed Mwakidosho alisema Mabera alikuwa mtu mwenye misimamo na nguvu kubwa kwenye bendi hasa pale anapotoka mwanamuziki kujiunga na bendi nyingine kutaka kurejea.

“Nimeumia sana na bendi itayumba maana Mabera alikuwa kiongozi mwenye msimamo hasa mwanamuziki anapotoka kujiunga na bendi nyingi baadaye akitaka kurejea alikuwa hakubali, ilibidi itumike nguvu kubwa ya ushawishi,” alisema Mwakidosho.

Naye mtoto wa marehemu, Mabera Said alisema baba yake alifariki juzi na msiba upo nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam na mazishi yalifanyika jana saa 10 alasiri Goba.

“Baba ameugua kwa zaidi ya miezi miwili na jana usiku (juzi) na leo (jana) amezikwa”. Meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti alisema bendi yao imepata pengo kwani ni kati ya wanamuziki wa zamani wa bendi hiyo waliokuwa wamebakia.

“Msondo tumempoteza mtu muhimu kwani ndiye mwanamuziki pekee mkongwe nchini Tanzania aliyeweka rekodi ya kutulia katika bendi moja bila kuhama,” alisema Kibiriti.

Alisema marehemu Mabera atakumbukwa kwa mchango wake kimuziki na ustadi wa upigaji wa gitaa la solo. Kabla ya kujiunga na Msondo enzi ikiitwa NUTA, Juwata na mwisho OTTU Jazz Band, aliwahi kuwa na bendi za Lake jazz, Kigoma jazz na Arusha jazz.

Kutokana na kitendo chake cha kutulia kwenye bendi moja kwa muda mrefu alipewa tuzo ya heshima katika usiku wa tuzo za muziki za Kilimanjaro Machi 26, 2011 na tuzo ya Uzalendo na Utaifa katika kipengele cha muziki iliyotolewa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwaka 2018.

Mabera alizaliwa Ujiji, Kigoma mwaka 1945, ameacha mke na watoto sita. Wapenzi wa muziki wake watamkumbuka kwa vibao vyake vya Vicky Mangara Nipeleke Mwanza, Piga Ua Talaka Utatoa na Binti Maringo.

Chanzo: habarileo.co.tz