Mtangazaji na Mwandishi nguli wa habari aliyefanya kazi katika Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) kwa miaka 20, Salim Kikeke amesema hakuwa na makubaliano na Serikali ya Tanzania kwamba aache kazi na arudi Tanzania kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali bali alirejea baada ya kuona ni wakati sahihi kwake kurudi nyumbani.
“Habari hizo zingekuwa na ukweli sasa hivi ningekuwa Mfanyakazi wa Serikali lakini nashukuru kama Watu wanaweza kunipa nyadhifa kama hizo, sikuwa na makubaliano yoyote na Serikali wakati naacha kazi na sina makubaliano yoyote na Serikali kama itatokea basi itatokea baadaye lakini nilirudi kwa uamuzi wangu mwenyewe na nilisema nitarudi”
Salim amesema hayo kwenye mahojiano maalum na Ayo TV, Kikeke amesema amerejea Tanzania kwa ridhaa yake baada ya kuomba zaidi ya mara moja kuacha kazi kwa hiyari yake.