Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari ya miaka 10 ya Diamond kimuziki itakavyotikisa Kigoma

89959 Diamond+pic Safari ya miaka 10 ya Diamond kimuziki itakavyotikisa Kigoma

Fri, 27 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni safari ya ‘bata la kukata na shoka’. Hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia safari ya kuelekea mkoani Kigoma ya staa wa muziki wa Bongofleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mashabiki zake.

Safari hiyo iliyopewa jina la ‘Twenzetu Kigoma, 10 years of Diamond Platumz’ ni ya kuadhimisha miaka 10 tangu alipoanza muziki.

Katika safari hiyo ya kutumia usafiri wa treni itakayoanza kesho kutoka jijini Dar es Salaam, itahusisha watu zaidi ya 500 wakiwemo mashabiki zake na wasanii mbalimbali watakaopamba siku hiyo itakayofanyika Desemba 31.

“Nafurahi kuona kila mwana industry anaungana nami katika kusherehekea miaka 10 ya kulisukuma gurudumu la Bongofleva,” anasema Diamond na kuongeza:

“Orodha ni kubwa, wote hatuwezi kuenea ila nitajitahidi ili wengi twende, nimechukua behewa nane za treni,” anasema.

Diamond anayetamba na wimbo wa ‘Baba lao’ kwa sasa, ana asili ya Kigoma kwa upande wa mama yake na atatumia shoo hiyo kurudisha shukurani kwa mama na wajomba zake.

Katika safari hiyo amewalipia mashabiki wake atakaotoka nao Dar es Salaam nauli ya kwenda na kurudi Kigoma. Wakati wa safari hiyo kutakuwapo na burudani mbalimbali ikiwamo kibao kata.

Hii sio mara ya kwanza kwa Diamond kujumuika na mashabiki zake, kwani Oktoba 6 mwaka jana aliposherehekea siku yake ya kuzaliwa alijumuika na wakazi wa Tandale, eneo alilozaliwa na kukulia na kutoa zawadi ya bima za afya na mikopo kwa wanawake na pikipiki kwa vijana.

TRC wazungumza

Akizungumzia safari hiyo, mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk anasema WCB (Wasafi Classic Baby) chini ya Diamond imechukua mabehewa nane na wamelipia kama abiria wengine.

Katika mabehewa hayo, Jamila anasema matatu ni ya daraja la pili kulala ambapo kila moja lina uwezo wa kuchukua abiria 36 na mabehewa ya daraja la pili la kukaa yapo sita huku kila moja likiwa na uwezo wa kuchukua abiria 80.

Ukipiga hesabu kama behewa zote hizo zitajaza abiria ni wazi kuwa Diamond ataondoka na watu wasiopungua 500. Nauli ya abiria mmoja kwa daraja la pili kulala ni Sh79,000, wakati daraja la pili kukaa ni Sh47,600.

“Tunashukuru namna WCB walivyokuja, kwani Diamond ni msanii mkubwa angeweza kwenda na kwa njia nyingine, lakini ameona alipie fedha ambazo tunaamini zitatumika kuboresha usafiri wa treni ambao ni mkombozi wa wananchi wengi wa kipato cha kawaida,” anasema na kuongeza:

“Pia kwa kufanya hivyo ameunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kufufua usafiri wa treni ulioonekana kusahaulika”.

Anasema katika safari hiyo, Diamond atapata fursa ya kuwasilimia mashabiki zake treni itakapokuwa ikisimama katika vituo 12 kabla ya kufika Kigoma.

Kuhusu usalama, Jamila anasema TRC imejipanga vilivyo na kila abiria atapata nafasi ya kukaa kama sheria na taratibu za usafiri huo zinavyotaka na hakutakuwa na kuzidisha abiria.

“Kizuri zaidi siku hiyo atasafiri na abiria wengine, kitakachomtofautisha ni kuwa na mabehewa manane kwa ajili ya watu wake,”anasema Jamila.

Meneja aelezea safari

Meneja wa Diamond, Babu Tale, akizungumzia ratiba ya safari anasema itaanza Dar es Salaam saa 2:00 asubuhi, siku ya Desemba 27 na wanatarajiwa kufika Kigoma Desemba 28, saa 11:00 jioni.

Tale anasema ndani ya treni kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwemo kula, kunywa na kucheza muziki.

“Najua wengi wanacheza au kusikiliza kibao kata, lakini watakaosafiri na Diamond watacheza aina hiyo ya muziki ndani ya treni.

“Pia kutakuwa na behewa maalumu litakalokuwa kama klabu ambako mastaa na mashabiki watakaoambatana na Diamond watajiachia,” anasema.

Tale anaongeza kuwa: “Usisahau kuwa katika kipindi chote cha safari yaani kuanzia Desemba 27, 2019 hadi Januari Mosi, 2020 watu watakapogeuza kurudi Dar es Salaam, gharama za malazi, chakula na burudani nyingine zitakuwa juu ya WCB.

“Hapa ninavyokuambia tayari tumeshachukua hoteli na nyumba za wageni zilizopo mkoani Kigoma, tunaamini itakuwa pia ni fursa ya biashara kwa watu wa Kigoma”.

Anasema watahakikisha kila waliyeondoka naye kwa treni anaishi kwa gharama za WCB, hivyo wana kila sababu ya kuwashukuru kwa kuwakirimu Kiswahili kama kaulimbiu yao inavyosema ‘Sisi ni Waswahili’.

Anasema siku ya tamasha kwa watu waliotoka nao Dares Salaam kwa treni hawatalipa kiingilio na kwamba watahudumiwa kwa huduma maalumu.

“Wakati wa kurudi kama kuna watu hawatapenda kutumia usafiri treni ni ruksa, ingawa tumelipia treni ‘go and return’, ”anasema Tale.

Diamond atoa shukrani

Mkali huyo wa wimbo wa ‘My number One’ anawakumbuka waliong’arisha nyota yake akiwamo aliyewahi kuwa mpigapicha wake Kifesi aliyebuni nembo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na Bob Junior aliyekuwa meneja wake wa kwanza pamoja na Dully Sykes aliyempa mwongozo wa wimbo wake wa kwanza unaofahamika kwa jina la ‘Nenda Kamwambie’.

“Kifesi wewe ndie uliyetengeneza logo ya WCB na leo hii ni miongoni mwa logo maarufu...kupitia wewe tulitimiza dhamira ya kuipa heshima tasnia ya wapigapicha na kufanya waheshimiwe mtaani,” anasema.

Akiandika kupitia ukurasa wake mtandao wa Instagram, Diamond anasema anakumbuka kabla ya kuachia wimbo wake ‘Nenda Kamwambie’ alimpelekea posta Dully Sykes asikilize na ampe mwongozo, kisha alimpigia Bob Junior na kumpongeza kwa wimbo mzuri.

“Shukrani sana bro kwa kuendelea kunifunda kisanaa...Kigoma inakusubiri kwa hamu ikupe shukrani za dhati kwa miaka hii 10,” anasema na Diamond na kuongeza:

“Bob Junior thamani yako kwangu milele haitofutika labda Diamond mwingine, lakini Diamond Platnumz huyu bila wewe asingekuwepo.

“Asante kwa mchango wako mkubwa kwangu... Kigoma inakusubiri ikupe shukrani ya dhati,” anaandika Diamond katika mitandao ya kijamii.

Baadhi ya wasanii wanaotajwa kuwamo katika safari hiyo hadi sasa ni Dula Makabila, Q.Boy, Johari, Khadija Kopa, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Young Killer, Linex, Mjeda, Dully Sykes, Bob Junior na Aunty Ezekiel.

Chanzo: mwananchi.co.tz