“Japokuwa (mke zaidi ya mmoja) imeruhusiwa katika baadhi ya mila na dini, lakini ukiwahoji asilimia kubwa ya wanawake utagundua hawapendi mwanamume aliyekuwa naye awe na uhusiano na mwanamke mwingine.”
Kauli hiyo ya mwanasaikolojia Charles Nduku imekuja baada ya Januari 16 mwaka huu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kutoa ripoti ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) ya mwaka 2020/21.
Kuhusu yaliyowasilishwa kwenye utafiti NPS, kuna suala la kupungua kwa idadi ya ndoa za zaidi ya mke mmoja ikilinganishwa na ilivyokuwa kwenye ripoti kama hiyo ya mwaka 2014/15.
Ripoti hiyo iliyohusisha kaya 4,164 , takwimu zinaonyesha ndoa za mke zaidi ya mmoja zimepungua kutoka asilimia 6.4 mwaka 2014/15 hadi asilimia 2.0 mwaka 2020/21, tafsiri yake ni kwamba ndoa za aina hii zimepungua kwa asilimia 4.4.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuna ongezeko la ndoa za mke mmoja, kutoka asilimia 34.8 hadi 40.5, huku idadi ya watu wanaoishi pamoja bila ndoa ikipungua kutoka asilimia 8.9 hadi 6.1.
“Ulishawahi kuona siku uliyooa ukatamani kuacha, yaani ile unatoka kuoa unafika hotelini unajionea mambo unasema nimekwisha, halafu unaangalia watu wako wanaokuheshimu na unaowaheshimu, sisi wengine huko mitandaoni nikaona nitatukanwa, basi nikawa navumilia hadi mambo ya kishetani,” alisema Haji Manara, wakati akiweka bayana kuachana na mkewe.
Kisaikolojia imekaaje?
Akizungumzia hilo, mwanasaikolojia Nduku anasema pengine ndoa za mke zaidi ya mmoja zinaporomoka kutokana na hulka ya wanawake wengi kutopendelea ‘kushare’ mwanamume hivyo kutokubali kuingia katika ndoa ya mke zaidi ya mmoja.
Nduku anasema pia wanawake wengi wamekuwa na uelewa mkubwa juu ya haki zao, hivyo inapotokea hatimiziwi haki zake kama mke anaweza kujiengua kwa haraka katika ndoa.
Kauli ya Nduku inashabihiana na mwanasaikolojia Deogratius Sukambi, ambaye anasema, “asili ya mwanamume ni kupenda kumiliki mwanamke, akiwa na uchumi mzuri matamanio yake yanaweza kuwa kumiliki hata mwanamke zaidi ya mmoja, sasa mambo yamebadilika wanawake nao wanapambana, wako vizuri kiuchumi.
“Kisaikolojia kadiri mwanamke anavyoimarika kiuchumi anapoteza ile hamu ya kuolewa kwa maana ya kumilikiwa. Halafu kingine kwa asili mwanamke hapendi kuchangia mwanamume, hivyo ikitokea yuko vizuri kiuchumi ameshapoteza interest ya kuolewa halafu ndiyo aje mwanamume kumfanya mke wa pili au wa tatu ni ngumu kukubali.”
Viongozi wa dini wanasemaje
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema kinachotokea kwa ndoa nyingi za mitala kuvunjika ni kutokana na kutoongozwa na mafunzo sahihi ya dini ya Kiislamu.
“Inawezekana hizi ndoa zinapungua, lakini ukweli ni kwamba siku hizi ndoa nyingi za matala haziongozwi na mafunzo sahihi ya dini, bali kila mmoja huziendesha ajuavyo na kwa matashi yake hivyo kukosa mizani ya uadilifu na haki kutamalaki,” anasema Sheikh Mataka.
“Pia, ukifuatilia kwa makini ndoa nyingi za mitala zinakosa sababu za msingi za kuwepo kwake, bali za muda mfupi ambazo hazithamini uhai wa ndoa hizo. Ndoa nyingi hukosa uwazi na hutawaliwa na usanii na uficho na pale siri fulani zinapovuja basi utulivu wa ndoa hizo huwa shakani.”
Sheikh Mataka anasema sababu ni za kiuchumi ambazo huvuruga uhusiano na kuondoa utulivu na hatimaye kudaiana talaka.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema kuna uwezekano kupungua kwa ndoa hizi za mke zaidi ya mmoja kunachangiwa na hali ya maisha.
Anasema licha ya dini ya Kiislamu kuruhusu mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja, lakini haimlazimishi kufanya hivyo akiwa hana uwezo.
“Dini haimlazimishi mtu kuoa wake zaidi ya mmoja, hilo ni jambo la sunna, ingawa kwa sasa wengi wetu wanaangalia hali halisi ya maisha na maelewano, hivyo anaamua kuwa na mke mmoja.”
Upande wa mila ukoje
Baadhi ya makabila mila zao huruhusu ndoa za mke zaidi ya mmoja, mfano Wagogo lakini Chifu Lazaro Chihoma anasema zinapungua.
“Miaka ya nyuma ndoa hizi zilikuwepo, tena hata wanawake kumi waliweza kuelewa kwa mwanamume mmoja. Amani, upendo na utulivu vilitawala kwenye familia, hakukuwa na vurugu kama tunavyozisikia na kuziona sasa kwenye ndoa ya zaidi ya mke mmoja,” anasema Chifu Chihoma.
“Zamani wanawake hawakuwa na tatizo kuongezewa wenzao na wakati mwingine mwanamke anamshauri mume wake aoe ili watoto wazaliwe wengi kukuza ukoo, lakini siku hizi ni nadra kukutana na familia za aina hii.
“Wanawake siku hizi ndio hawataki na ikizingatiwa tunaoana makabila tofauti utamaduni huu unapotea, wapo ambao hawataki kwa sababu ya wivu na wengine wanahofia malazi maana hili nalo limekuwa tatizo kubwa,” anasema Chifu Chihoma.
Hali ya uchumi
Akizungumza na Mwananchi, Oscar Mkude ambaye ni mchumi anasema upungufu huo unaweza kuwa unasababishwa na vijana wengi kupenda kuwa katika hali ya kujitegemea kabla ya kuoa au kuolewa, hata hivyo hilo linahitaji upatikanaji wa kazi za kipato.
“Sasa ukitazama takwimu za ajira utaona tangu mwaka 2015 zimekuwa si nzuri sana, na wasio na ajira kwa kiasi wameongezeka. Hii ina mchango wa kuwachelewesha wasio na ajira kuingia kwenye ndoa ya mke mmoja au hata wawili kutokana na kushindwa kuhudumia,” anasema Mkude.
Pia anasema hali ngumu ya kiuchumi inaweza kumfanya mwanamume kuogopa kuongeza mke mwingine kwa kuhofia kushindwa kutimiza mahitaji.
Anasema ongezeko la migogoro ya ndoa ambayo inazidi siku hadi siku linaweza kuwa sababu ya kuchangia hali hiyo.
Nini kinasababisha kupungua?
“Wake wenza hawakai pamoja, hakuna urafiki kati yao, mimi wake zangu walikaa na kuzungumza wakati naumwa, nilipopona wakaanza tena visa. Kwanza hainogi wake wenza wakipatana. Anayeweza kukubali kuwa chini ni mke wa pili lakini mke wa kwanza, huwa hakubali, muda wote anataka kuonyesha yeye ni nani,” anasema Mzee Yusuph, miongoni mwa wanaume waliowahi kuwa na mke zaidi ya mmoja, katika mahojiano yake aliyofanya hivi karibuni.
Farhan Jumaa anasema, “sikuoa mke wa pili kwa sababu wa kwanza ana upungufu, niliona sina sababu ya kufanya zinaa wakati dini yangu inaniruhusu kuoa mke zaidi ya mmoja. Nikaoa, baada ya muda nikaona yule mwanamke anataka kunipanda kichwani.
“Yaani alitaka kunifanya kama mali yake binafsi akiamini ni mke mdogo basi nitampenda zaidi ya mke wangu wa kwanza. Kilichoniuma zaidi nikaona anamdharau mke wangu na kumfuatilia, licha ya kuwa hawakuwa wakiishi nyumba moja. Nilivyoona mambo yanazidi nakosa amani basi nikampa talaka, nimebaki na mke wangu mmoja,” anasema Jumaa.
Wakati wanaume wakisema hayo, Mariam Khamis anasema alifikia uamuzi wa kudai talaka baada ya kuona mume wake ameweka nguvu kubwa kwa mke mdogo na kumuacha yeye ahangaike na watoto peke yake.
“Sikuwa tayari kuruhusu mume wangu aoe mke wa pili, lakini kwa sababu dini yetu inaruhusu hivyo na alinisihi sana niridhie basi nikaridhia akaoa, baada ya muda naona amehamishia makazi huko hana tena habari na sisi.”
Hidaya Mkazilagwa anasema alilazimika kuomba talaka baada ya kushindwa kuvumilia changamoto alizokuwa anazipata kutoka kwa mke mkubwa.
“Nilikuwa mke mdogo, lakini yule mwenzangu niliyemkuta hakukubaliana kabisa na ujio wangu, basi ikawa visa na vituko kila siku na bahati mbaya tulikuwa tunaishi kwenye eneo moja lakini kila mtu na nyumba yake ila sikuwa na amani.
“Ilifika wakati nikaona naweza kuhatarisha maisha yangu, basi nikaomba talaka hatimaye mwanaume alielewa akanipatia,” anasema Hidaya.
Wanawake wanasemaje?
“Pamoja na kuwa na imani ya dini na kuelewa kuwa wanaume wameruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja, nachukia sana namna wanavyolizingatia suala hilo pekee kwenye dini.
“Kama huyu wangu hata kumcha Mola ni mtihani, lakini anang’ang’ania kuoa kwa madai ya kuwapa nusra wanawake, inaumiza ila hakuna namna kwa sababu tumeusiwa hivyo,” anasema Mwanahamisi Rajabu.
Akilizungumzia hilo, Habiba Miyombo, ambaye ni mke wa tatu katika ndoa yake, anasema amedumu kwa miaka minne sasa, anasema mwanzoni alikubali kuolewa matala kwa sababu anampenda mumewe na hakutaka kumpoteza, licha ya kuwa na wasiwasi sana kuamua jambo hilo.
“Hata familia yangu haikukubali moja kwa moja, nakumbuka shangazi yangu (marehemu) aliniambia nikishindwa nirudi ukewenza si lelemama, lakini tofauti na tulivyokuwa tunafikiria, ninaishi kwa amani kila mmoja anaishi kwake, na mume wetu anatuhudumia bila kubagua,” anasema.
Kwa upande wa Joyce Japhet anasema kuwa kuna wakati anatamani bora mumewe angeweka wazi uhusiano wake mwingine wajijue wapo wangapi kuliko sheria inavyomzuia na kufanya kwa siri huku akimfuma na ujumbe mfupi wa simu au akizungumza na wanawake zake mara kwa mara.
“Sidhani kama kuna mwanamume anadumu na mwanamke mmoja, wengi wanatudanganya,” anasema Joyce.