Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu tano za kumuunga mkono Diamond katika harakati zake

9834 Diamond+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukiachana na maisha yake ya skendo zinazohusisha wanawake, Diamond Platinumz ni msanii aliyejiimarisha katika ulimwengu wa muziki. Kusini, Mashariki na Magharibi mwa Bara la Afrika jina lake linatajika sana.

Alianza kujiimarisha kama mwimbaji na mtumbuizaji bora na kujizolea tuzo mbalimbali zilizomkuza zaidi. Kabati lake lina tuzo zote kubwa zilizowahi kutolewa miaka ya hivi karibuni. Afrimma, MTV Base, MTV EMA, Channel O, Killi Awards na nyingine nyingi.

Anaupaisha muziki

Mashabiki, wadau na Watanzania kwa ujumla wanazo sababu bilioni moja kumuunga mkono Diamond kutokana na juhudi anazofanya kuupaisha muziki wa Bongo Fleva.

Mwanamuziki wa Nigeria, Davido alipotua nchini mwishoni mwa wiki alijua bila Diamond shughuli ingedoda na ndio sababu alimuita amsaidie kuwachangamsha mashabiki.

Kwa kiasi kikubwa muziki wa Bongo Fleva sasa unatajika kote Afrika kutokana na juhudi zake za kujitangaza kwa kufanya kazi nzuri zinazoshindana katika chati za kimataifa.

Anatoa ajira

Taja orodha ya wasanii walio chini ya lebo ya WCB. Rich Mavoko, Queen Darlin, Rayvanny, Harmonize, Lavalava na Mbosso. Taja watu walio nyuma ya wasanii hawa kuanzia mameneja, wacheza shoo, DJ na watu wanaowavalisha.

Hii inatoa picha ya namna gani wazo la Diamond kuanzisha lebo ya WCB limekuwa chanzo cha ajira kwa vijana wengi nchini wanaochangia pato laTaifa kwa ujumla.

Anapandisha thamani ya muziki

Thamani ya wanamuziki pamoja na mambo mengine machache, kwa kiasi kikubwa imepanda kwa nguvu ya Diamond.

Alipoanza kudai malipo makubwa kutumbuiza aliwafungua macho wasanii wenzake ambao hata kama hawakufika alipo lakini walipanda dau.

Pia ameleta ushindani katika muziki ambao umechangia kuboreshwa kwa kazi za sanaa hasa video za wanamuziki wengi nchini.

Anawapa maisha bora wanamuziki

Kuanzisha televisheni na ujio wa Tamasha la Wasafi ni hatua nyingine ya mafanikio yake katika kuutoa muziki kwenda katika kiwango cha juu. Hii sasa siyo kwa ajili yake ni kwa tasnia nzima kwa ujumla.

Diamond anazungumzia zaidi televisheni na tamasha litakavyowanufaisha wasanii wenzake, kwamba hawatakuwa na wasiwasi wa kazi zao kuchezwa katika runinga na mwisho wa siku watapata mkwanja mrefu kwa kutumbuiza katika Tamasha la Wasafi.

Hii ni hatua nzuri kwa sababu vitu hivi vinakuja kutoa changamoto kwa wakongwe, kama msanii atalipwa vizuri kutumbuiza Tamasha la Wasafi bila shaka ni changamoto kwa wengine kumpandia dau msanii huyo.

Uwepo wa Wasafi Televisheni na tamasha ni msingi wa hatua nyingine kwa wasanii nchini kwa sababu wakishapanda thamani hawawezi kushuka na kwa nguvu moja wakimuunga mkono Diamond, wataondokana na kadhia ya kulalamikia ujira mdogo iliyokuwepo kwa miongo kadhaa.

Anatoa somo kuwa muziki na biashara vinaenda

Wasanii wengi waliwahi kuwa juu. Diamond siyo wa kwanza. Wako wapi sasa? Wengi hawafahamiki walipo ingawa wachache waliamua kufanya shughuli nyingine lakini wapo waliopotea kabisa hata baada ya kufanya vizuri wakati fulani.

Inawezekana ni kwa sababu waliamini muziki ndiyo njia pekee inaweza kuwapa heshima na kipato. Diamond kukesha akiweka mipango sawa, kuogopa kwake kufulia kunatoa somo kwa wengine kuwa unaweza kuwa mwanamuziki na mfanyabiashara mkubwa.

Jay Z, P Diddy huenda ndio wasanii anaowatazama kama kioo chake. Manguli hawa wanaendelea kuheshimika kwa kuwa hawana njaa. Wamewekeza kwenye biashara, wameajiri watu na ni wawekezaji wakubwa huko Marekani.

Chanzo: mwananchi.co.tz