Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu Harmonize kutoonekana Wasafi Festival zaanikwa, aomba kuvunja mkataba

72469 Wasafipic

Thu, 22 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Meneja wa kundi la Wasafi,  Sallam amesema msanii Harmonize haonekani katika matamasha ya Wasafi Festival yanayoendelea mikoa mbalimbali nchini kwa kuwa amevunja utaratibu wa tamasha hilo kwa kujitenga na wenzake.

Amesema mbali na kuvunja utaratibu,, pia ameomba kuvunja mkataba na kundi hilo.

Akizungumza katika televisheni ya Wasafi, Sallam amesema katika tamasha la Wasafi lililofanyika mjini Mwanza, Harmonize alitumia usafiri binafsi, kufanya baadhi ya mambo yaliyotoa tafsiri kuwa amejitenga.

Sallam amesema kwa sasa Harmonize moyo wake haupo Wasafi lakini ukweli ni kuwa bado ana mkataba na kundi hilo.

“Kwanini nasema hivyo, Harmonize ameshatuma barua ya maombi Wasafi kuvunja mkataba wake na yupo tayari kufuata sheria zote.”

“Sisi tumependezwa na hatua yake kwa sababu labda kuna vitu ameona akivifanya atafika mbali,” amesema Sallam.

Pia Soma

Kuhusu kujitenga na wenzake Sallam amesema, “Hili jambo si sawa kulingana na maudhui ya tamasha hilo. Maudhui ya Wasafi Festival ni umoja. Msanii akiamua kuacha kuambatana na wasanii wenzake ambao wapo pamoja katika tamasha ni kwenda kinyume.”

“Sisi katika tamasha letu hatupendi kutengeneza matabaka, tumeamua kuwa kitu kimoja, siyo kwamba Diamond, Rayvany hawakuwa na uwezo wa kutumia usafiri wao binafsi kama alivyofanya Harmonize” amesema Sallam.

Meneja huyo amewaomba radhi wasanii wote walioshiriki tamasha la Mwanza kutokana na Harmonize kufanya jambo hilo, kwamba uongozi wa Wasafi haukuwa na taarifa.

Amebainisha kuwa Harmonize amefanya jambo la kuhatarisha taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kumpandisha jukwaani msanii ambaye hakuwepo katika ratiba ya tamasha hilo. 

“Alikuja na msanii kutoka nje na hatukujua kama alishamchukulia kibali au laa,  kwa hiyo unaona kabisa anafanya vitu ambavyo vinaweza kuingiza taasisi katika tatizo,” amesema.

 

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz