Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema mradi wa kufua umeme wa Stigler's Gorge utapata maji ya uhakika kutoka kwenye mito mitatu ya Kilombero, Ruaha na Wami.
Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Septemba 6 jijini Dar es Salaam wakati akichangia mada kwenye mkutano wa mwaka wa wahandisi.
Amekanusha taarifa kwamba mradi huo hautakuwa endelevu kwa sababu ya upungufu wa maji unaotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu.
"Mradi wa Stigler's Gorge utapata maji ya uhakika kutoka kwenye vyanzo vya mito mitatu ya Kilombero, Ruaha na Wami. Sehemu kubwa ya maji itatoka Mto Kilombero ambao unapita katika hifadhi ya Selous na haujaharibiwa," amesema.
Kuhusu upatikanaji wa maji nchini, Profesa Mkumbo amesema umezidi kuongezeka hasa baada ya serikali kuweka kipaumbele kwenye suala la hilo.
Amesema katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano, bajeti ya Sh10.4 trilioni imetengwa kwa ajili ya miradi ya maji nchini hasa katika maeneo ya vijijini.
"Maji ndiyo roho ya maendeleo ya Taifa lolote. Kwa kutambua umuhimu huo, serikali imeweka kipaumbele kwenye sekta ya maji katika mpango wa miaka mitano na bajeti yake ni Sh10.4 trilioni," amesema Profesa Mkumbo.