DJ maarufu wa Bongo, Romy Jons hatimaye amevunja kimya kuhusu madai ya kutimuliwa katika Lebo ya kaka yake, WCB.
Akizungumzia tetesi hizo, Romy ambaye ni kaka wa bosi wa WCB, Diamond Platnumz na pia DJ wake maalum amedaiwa kufurushwa kutoka kwenye lebo hiyo mashuhuri hivi karibuni baada ya kujitokeza kwa tofauti baina yake na lebo hiyo.
Katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya kupokea tuzo la muigizaji bora wa kiume mnamo wikendi, aliweka wazi kuwa yeye bado ni familia ya Wasafi na kutupilia mbali uwezekano wa kutimuliwa.
"Mimi nafanya kazi Wasafi, nafukuzwa vipi? Mimi ni kaka'ke Diamond, watu wanajua. Mimi sitofukuzwa kazi. Nitakuwa labda kuna kitu nimetoka ama nimeingia sehemu," alisema Jones.
DJ huyo alibainisha kuwa amekabidhiwa majukumu makubwa katika Wasafi na kwa hiyo sio rahisi yeye kutimuliwa.
"Ningekuwa nafukuzwa Wasafi, mimi bado ni bosi wa muziki pale. Ningeondolewa kabisa pale kwa TV na Redio," alisema.
Tetesi kuwa Romy Jons alitimuliwa kutoka kwenye chombo hicho kikubwa cha habari cha Bongo zilianza kusambaa baada ya aliyekuwa mpiga picha wa Diamond, Lukamba ambaye aliacha kazi pale miezi michache iliyopita kudokeza kuwa huenda mcheza santuri huyo pia ameondoka.
Lukamba alidai kuwa Jones hajakuwa akionekana sana katika Wasafi kwa kuwa alisimamishwa kazi na Diamond.
"Tunaongea na kakangu Lukamba, alikuwa anatania tu," Jones alisema.
Katika mahojiano hayo, Jons pia alitetea kazi yake na kubainisha kuwa uchezaji santuri ni kazi ya kuheshimika.
Aliwaomba wakosoaji wake kujifunza jinsi ya kuthamini kazi za watu wengine na kusita kuzidharau.
"Tukiwa tunaheshimu kila kitu ambacho mtu anafanya kupata riziki, tungefika mbali zaidi," alisema.
Jons amekuwa akifanya kazi katika idara ya muziki ya Wasafi Media kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwake na pia kuandamana na Diamond katika ziara zake kama mcheza santuri wake rasmi.