Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rich Mavoko njiapanda ndani ya WCB

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tetesi za kuondoka kwa msanii wa WCB, Rich Mavoko bado kitendawili ndani ya kampuni hiyo ambayo inaongozwa na Diamond Platnumz.

Rich Mavoko alisainiwa rasmi WCB Juni 3, 2016, na kufanya idadi ya wasanii Walioko chini ya lebo ya wasafi kufikia sita.

Mpaka sasa waliopo katika lebo hiyo mbali na Rich ni Harmonize, Lavalava, Rayvanny, Qeen Darleen, Mbosso aliyesajiliwa mwaka huu na Diamond mwenyewe

Hata hivyo ndani ya mwezi huu kumekuwa na sintofahamu kuhusiana na suala la Mavoko kuondoka ndani ya lebo hiyo huku ikichangiwa na sababu kadha wa kadha watu kuhisi hivyo.

Mojawapo ni Rich Mavoko kutopost chochote katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram tangu Mei 25 mwaka huu jambo ambalo sio kawaida kwa wasanii wanaomilikiwa na lebo hiyo.

Watu wanaotembelea kurasa za wasanii hao wamekuwa wakiona matukio mbalimbali yanayoendelea kwa wasanii wa WCB ikiwemo mmojawapo anapokuwa na shoo mahali au kutoa wimbo, lakini kwa Rich imekuwa tofauti kwani hakuna alichoposti tangu Mei. Anafanya hivyo wakati matukio kibao yameshafanyika, ikiwemo ya Harmonize kufanya shoo kubwa pale ukumbi wa Dar Live siku ya sikukuu ya Idd pili, alioita Usiku wa Kusi.

Pia bosi wao Diamond hivi karibuni kamaliza ziara yake nchini Marekani, lakini hajawahi kurusha chochote kama wenzake ambavyo walikuwa wakifanya.

Kama vile haitoshi nyimbo kibao zimeachiwa na wasanii kutoka lebo hiyo, ikiwemo Kwangaru aliyoifanya Harmonize na Diamond, Iyena aliimba Diamond na Rayvanny, Nadekezwa wa Mbosso na Baila wa Diamond aliouachia hivi karibuni ambazo zote hizo Mavoko kama hajaziona vile na kuwapa sapoti wasanii wenzake kama ilivyo ada yao.

Pamoja na ukimya huo, wiki hii aliibua gumzo zaidi baada ya kurushia wimbo wake mpya wa Happy.

Jambo hilo linaifanya gazeti la Mwananchi kuutafuta uongozi wa WCB ili kusikia chochote kutoka kwao ikiwemo kujibu tetesi hizo za Rich kuondoka.

Mmoja wa watu waliozungumza ni Meneja wa Diamond, Said Fella, ambaye katika majibu yake anasema yeye hana jibu lolote kwa kuwa sio Meneja wa Rich na kutaka atafutwe mwenyewe.

“Nimekuwa nikiulizwa na watu kuhusiana na msanii huyu, lakini eleweni sina jibu kwa kuwa mimi msanii ninayemsimamia ni Diamond, kwani kila mwanamuziki pale ana meneja wake,” anasema Mkubwa Fela.

Mwananchi haikukata tamaa kwani ilimpigia simu Rich Mavoko mwenye ambaye anasema: “Kwa sasa sipo tayari kuzungumza lolote naombeni mniache, nikiwa tayari nitawaambia. Waandishi mmenipigia simu sana kuuliza hili, lakini naombeni mnipe muda kidogo kwani ni hivi karibuni mtajua ukweli wote, hata hii simu yako nimeipokea tu basi, maana nimekuwa nikizima muda mrefu kutokana na usumbufu ninaoupata wa kuulizwa suala hili, naombeni muwe na subra siku za karibuni mtaujua ukweli wote.”

Chanzo: mwananchi.co.tz