Anajiita Messi wa Bongo Fleva kutokana na ukali wa uimbaji, uandishi na uchezaji wake jukwaani. Ameshatengeneza ngoma kubwa za kutosha na anahesabika miongoni mwa waimbaji wazuri Tanzania.
Rich Mavoko, mtoto wa Mama Richard ameshatoa albamu na EP. Amefanya kolabo za kimataifa, kwa kifupi ana historia yake ndani ya Bongofleva, inakujuza zaidi;
1. Kabla ya Rich Mavoko kusaini WCB Wasafi hakuwahi kukutana au kuongea na Diamond Platnumz kuhusu hilo, AY ndiye aliyemkutanisha na Sallam SK wakiwa nchini Uganda kwenye shoo ya Jose Chameleone ndipo yalipoanza mazungumzo ya kujiunga.
2. Verse ya mwisho ya wimbo wa Malaika, Rarua imeandikwa na Rich Mavoko, ndio ngoma iliyofanya vizuri hadi Malaika kupata tour
Washington DC, Marekani mwaka 2017.
3. Lulu Diva alimlipa Rich Mavoko fedha ili kumshirikisha katika wimbo wake ‘Ona’ licha ya kudaiwa ni wapenzi, video ya wimbo huo ndio video ya pekee ya Lulu Diva iliyotumia bei kubwa kushoot kwa madai ya lulu diva.
4. Wimbo namba tisa kutoka kwenye albamu ya Diamond Platumz ‘A Boy From Tandale’ uitwao ‘Sijaona’ umeandika na Rich Mavoko wakati huo yupo chini ya WCB Wasafi.
5. Licha ya kutokea Morogoro, Rich Mavoko hajawahi kuutaja mkoa huo katika nyimbo zake kama wasanii wengine, hii ni sawa na Wizkid ambaye hajawahi kutaja jina hilo katika ngoma zake, anatumia zaidi jina la Starboy.
6. Video za nyimbo zote ambazo Rich Mavoko alizitoa chini ya WCB Wasafi kama ‘Kokoro’, ‘Rudi’ na ‘Imebaki Stori’ zimeondolewa kwenye majukwaa ya kidijitali kama YouTube.
7. Rich Mavoko hapendi kutoka ‘out’ na msichana ambaye wakifika sehemu ya kula bata ataanza kujidai anajuana na kila mtu. Hiyo ni sawa na Mwana FA ambaye huwa hapendi kukaa na msichana mwenye kelele akiwa viwanja.
8. Fid Q ndiye msanii wa Hip Hop Bongo aliyefanya kolabo nyingi zaidi na Rich Mavoko. Hadi sasa wawili hao wameachia ngoma kama ‘Sheri’, ‘Blow Up’, ‘Tawile’, ‘Champion’ na ‘Bambam’.