Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rayvanny bila WCB kwisha!

Rayvanny Pic Rayvanny bila WCB kwisha!

Sat, 26 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Diamond Platnumz na Rayvanny wamefikisha ngoma 10 walizorekodi tangu mwaka 2016 ukiwa ni wastani wa ngoma 1.6 kwa kila mwaka, hivyo kuandika rekodi kama wasanii pekee Bongo walioshirikiana zaidi miaka sita iliyopita.

Rayvanny alijiunga na WCB mwaka 2015 akiwa ni msanii wa pili, baada ya miaka sita ya kufanya kazi pamoja, aliachana nao akiwa tayari amefungua lebo yake, Next Level Music (NLM) ambayo inamsimamia Mac Voice.

Licha ya kuanzisha lebo yake, Rayvanny ameendelea kuwa karibu na WCB na hasa bosi wa lebo hiyo, Diamond na hivi sasa wanafanya vizuri na wimbo wao mpya, ‘Nitongoze’ ambao ni wa 10 kwa wawili hao kufanya pamoja.

Huu ni wimbo wa kwanza kwa Rayvanny kumshirikisha Diamond akiwa nje ya WCB Wasafi lakini ni wimbo wa nane kufanya pamoja (wawili pekee) tangu mwaka 2016 walipotoa wimbo wao wa kwanza, Salome.

Rayvanny na Diamond wameshirikiana kwenye nyimbo kama Salome, Iyena, Mwanza, Tetema, Timua Vumbi, Amaboko na Woza, huku wakiwa wamekutana kwenye ngoma mbili za wasanii wote wa WCB, ‘Zilipendwa na Quarantine’, hivyo kufanya jumla ya nyimbo 10.

Katika nyimbo hizo nane, Diamond amemshirikisha Rayvanny katika nyimbo zake mbili, Salome na Iyena, huku Rayvanny akimshirikisha Diamond kwenye nyimbo sita ambazo ni; Mwanza, Tetema, Woza, Timua Vumbi, Amaboko na Nitongoze.

Hivyo, kwa kipindi cha miaka sita hakuna wasanii wa Bongo walioshirikiana zaidi ya hawa, huku Rayvanny akiwa ndiye msanii pekee aliyemshirikisha Diamond kwenye nyimbo zake nyingi kwa muda wote, ni sita.

Ukaribu wao kikazi uliingia doa baada ya Rayvanny kutoshirikishwa kwenye EP ya Diamond, First of All (FOA) ya Machi mwaka huu ikiwa na nyimbo 10, huku Zuchu na Mbosso wakiwa pekee Bongo walioshirikishwa.

Na Rayvanny alipotangaza rasmi kuondoka WCB Wasafi, hakuna aliyetegemea kuwa wawili hao watakuja kufanya tena kazi pamoja, wengi walifikiri shughuli yao ndio imekwisha ila shughuli bado ipo.

Hata hivyo, hiyo ni tofauti kwa upande wa Harmonize na Rich Mavoko ambao waliachana na WCB Wasafi kwa mvutano mkubwa hadi kufikishana Basata, hadi wanaondoka Diamond alikuwa hajamshirikisha yeyote kati yao katika wimbo wake.

Nyimbo ambazo Harmonize alimshirikisha Diamond ni ‘Bado’, ‘Kwangwaru’, naye Rich Mavoko akampa shavu Diamond katika ngoma yake ‘Kokoro’, huku tangu wameondoka WCB Wasafi zaidi ya miaka minne hakuna aliyeweza kufanya tena kazi na Diamond.

Hivyo, Rayvanny anaendelea kubaki kama msanii pekee aliyeshirikishwa zaidi na Diamond zikiwa ni nyimbo mbili, ndani ya WCB Wasafi kwa muda wote Diamond kawashirikisha wasanii watatu tu katika nyimbo zake ambao ni Rayvanny, Zuchu na Mbosso. Lava Lava, Queen Darleen, Harmonize na Rich Mavoko hawajawahi kupata nafasi hiyo, Darleen ndiye mwenye bahati mbaya zaidi maana hajawahi hata kumshirikisha Diamond katika wimbo wake wowote ule hajafanikiwa licha ya kuwa ni ndugu!.

Ngoma ambazo Rayvanny amemshirikisha Diamond, video zake zimekuwa zikipata idadi kubwa ya watazamaji YouTube, mfano ‘Tetema’ ina watazamaji milioni 70, ‘Mwanza’ milioni 59 na ‘Amaboko’ milioni 16.

Ukimtoa Rayvvanny, msanii mwingine ambaye ameshirikiana zaidi na Diamond ni Mbosso, wamekutana kwenye ngoma kama ‘Baikoko, Karibu na Yataniua’ zote za Mbosso, huku Diamond akimshirikisha Mbosso kwenye ngoma yake ‘Oka’, ukichanganya na ngoma za lebo ambazo ni; Zilipendwa, Jibebe na Quarantine, jumla ni saba.

Wasanii wengine wa Bongofleva walioshirikiana zaidi na Diamond ni Zuchu (5), Lava Lava (5), Harmonize (3), Rich Mavoko (2), Queen Darleen (2), huku Nay wa Mitego, Shetta na Linex kila mmoja akimshirikisha Diamond kwenye nyimbo zake mbili.

Mwimbaji wa Nigeria, Mr. Flavour ndiye msanii wa kimataifa ambaye amefanya kolabo nyingi zaidi na Diamond zikiwa ni tatu, wawili wao wameshirikiana kwenye nyimbo kama ‘Nana’, ‘Time to Party’ na ‘Berna Reloaded’, huku Patoranking (Nigeria), Morgan Heritage (Jamaica) wakifanya kolabo mbili na Diamond. Ukichana na Diamond, msanii mwingine Bongo na WCB Wasafi ambaye Rayvanny amemshirikisha zaidi kwenye nyimbo ni Zuchu ambaye amesikika kwenye ngoma zake mbili, Number One na I Miss You.

Nyimbo hizi zimetoka ndani ya miaka miwili na kufanya vizuri, mfano video ya wimbo, Number One, ndio inayoongoza kwa Rayvanny kuwavutia watazamaji wengi YouTube, kisha zinafuata video za ngoma, Tetema na Mwanza ambazo amemshirikisha Diamond. Hivyo, unapata picha kwanini Rayvanny karudi tena kufanya kazi na ikiwa ni miezi minne tangu kuondoka WCB Wasafi, anajua ni kipi hasa anakipata, na ni wazi bila wao shughuli yake imekwisha.

Utakunbuka chini ya WCB Wasafi, Rayvanny aliweza kushinda Tuzo ya BET (2017), kuachia EP tatu; Flowers (2020), New Chui (2022) na Flowers II (2022), ametoa albamu moja, Sound From Africa (2021).

Aliingiza nyimbo kwenye chati kubwa duniani kama Billboard Latin na Mexico, huku akiandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza kwenye hafla ya utoaji wa tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2021 nchini Hungary.

Tangu ameondoka WCB Wasafi Julai mwaka huu, hakuna video ya wimbo wake uliofikisha walau ‘views’ 2m YouTube, Pele Pele ft. Luana Vjollca ndio wimbo wa kwanza kuutoa baada ya kuachana na lebo hiyo. Ulitoka Julai 22, 2022 na hadi sasa video yake imepata ‘views’ 1.6m tu ikiwa ni miezi mitatu tangu itoke.

Wimbo huu mpya, ‘Nitongeze’, ndani ya muda mfupi tayari umefikisha ‘streams’ milioni 2.1 Boomplay, wakati ‘Pale Pale’ iliotoka miezi mitatu nyuma ina ‘streams’ 1m. Hivyo ni wazi kazi za Rayvanny akimshirikisha Diamond au chini WCB Wasafi, ngoma zake zinapata mapokeo makubwa tofauti na akifanya pekee yake.

Wimbo wa Rayvanny uliosikilizwa zaidi Boomplay Music (most streamed) ni Number One aliomshirikisha Zuchu, hii ina wasikilizaji 11.8m. Video ya wimbo huo ndio video pekee ya Rayvanny iliyotazamwa zaidi YouTube (most viewed) ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 71 YouTube tangu Novemba 26, 2020.

Chanzo: Mwanaspoti