Rappa wa Iran aliyefungwa kwa kuunga mkono maandamano dhidi ya serikali amehukumiwa kifo, wakili wake amesema.
Toomaj Salehi katika nyimbo zake aliunga mkono maandamano ya mwaka 2022 yaliyozuka kulalamikia kifo cha Mahsa Amini, mwanamke aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kudaiwa kuvaa hijabu "visivyo".
Mmoja wa mawakili wa Bw Salehi, Amir Raesian, alisema rapa huyo atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya kifo.
Mamlaka za Iran hazijatoa tamko lolote.
Bw Salehi alikamatwa kwa mara ya kwanza Oktoba 2022 baada ya kutoa taarifa hadharani kuunga mkono maandamano na alishtakiwa kwa makosa mengi.
Alihukumiwa Julai 2023 kifungo cha miaka sita na miezi mitatu jela baada ya kukwepa hukumu ya kifo kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi.
Lakini mnamo Januari, Mahakama ya Mapinduzi ya Isfahan ilimshtaki Bw Salehi kwa mashtaka mapya ikiwemo yale ambayo awali ameachiliwa huru, wakili wake alisema.
Akiongea na gazeti la Sharq siku ya Jumatano, Bw Raesian alisema mahakama ya mapinduzi ilipuuza uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi wa kusamehe na badala yake ikatoa mashtaka mapya kabla ya kutoa "adhabu kali zaidi".
Mashtaka ambayo alipatikana na hatia ni pamoja na rushwa duniani kwa mashtaka kadhaa, "Baghi" [uasi wa kutumia silaha], mkusanyiko na kula njama, propaganda dhidi ya taasisi tawala na kuchochea ghasia.
Bw Salehi ana siku 20 za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.