Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Professor Jay hawezi kumjibu Khaligraph Jones

Prof Jay Ajipost Kwa Mara Ya Kwanza Professor Jay hawezi kumjibu Khaligraph Jones

Mon, 4 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Raopa kutoka Kenya, Khaligraph Jones kwa kiasi fulani amefanikiwa kuichangamsha Hip Hop ya Bongo baada ya kudai muziki huo umeshuka nchini Tanzania kwa sasa ukilinganisha na hapo awali, huku akitetea kauli hiyo kupitia wimbo wake mpya, Bongo Favour.

Hata hivyo, licha ya kujibiwa na baadhi ya wasanii wa Hip Hop Bongo kupitia ngoma zao (diss track) ni vigumu kwa wasanii wakubwa na wakongwe wa muziki huo kama kina Sugu, Professor Jay, Fid Q, Jay Moe kumjibu Khaligraph Jones.

Utakumbuka Khaligraph Jones au OG ana mashabiki wake Bongo na kwa miaka ya karibu wasanii wengi Tanzania alipotaka kufanya kazi na rapa wa kimataifa, basi jina lake lilikuwa ni la kwanza kutajwa, hilo lilipelekea kufanya kazi na wasanii wengi.

Mfano kuna wasanii Bongo waliona kumshirikisha Khaligraph Jones katika albamu zao itakuwa ni biashara nzuri, miongoni mwao ni Harmonize (Afro East) na Alikiba (Only One King), huku Khaligraph naye akiwashirikisha wasanii hao.

Wasanii wengine Bongo waliomba kolabo kwa Khaligrap Jones na nyimbo zao zimeshatoka ni Ommy Dimpoz, Rosa Ree, Young Killer, Christian Bella, Nikki Mbishi, Chin Bees, Rayvanny, Roma na Stamina (Rostam), Stereo, RJ The DJ, Country Boy, Conboi n.k.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, hakuna msanii wa Kenya ambaye ameshirikiana na wasanii wengi wa Tanzania kama Khaligraph Jones na ndio sababu kauli yake imepokewa kwa uzito mkubwa na kuteka mazungumzo hasa mtandaoni.

Ikumbukwe Khaligraph Jones mwaka huu ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) 2022 kama Msanii Bora Afrika Mashariki, huku mwaka 2020 akishinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (Afrimma) kama Msanii Bora wa Hip Hop Afrika.

Lakini ni kwanini ni vigumu kina Professor Jay kumjibu Khaligraph Jones? Pengine hawajaona uzito wa kauli yake au wameamua kumpuuza? Au wamefunika kombe mwanaharamu apite?

Jibu ni kwamba muziki wa Hip Hop kwa Tanzania umegawanyika kwa vizazi, kizazi cha kina Saleh Jabir (1990 - 1995) ndio kinatajwa kuwa cha kwanza, kisha wakaja kina Sugu, Hard Blasters Crew (HBC), Professor Jay n.k (1995 - 2000) hawa ndio kizazi cha pili.

Kisha wakafuata kina Jay Moe, Mwana FA, Fid Q, AY, Ngwea n.k (2000 - 2005) hiki ni kizazi cha tatu, kisha wakaibuka kina Joh Makini, Nako 2 Nako Soldiers, Chid Beenz, JCB, Lord Eyes n.k (2005 - 2010) hiki ni kizazi cha nne.

Baadaye wakaja kina Darassa, Roma, Nikki Mbishi, Stamina, Young Killer, Izzo Bizness, Godzilla n.k (2010 - 2015) hawa ni kizazi cha tano, kisha wakaja kina Rosa Ree, Young Lunya, Frida Amani, Conboi, Rapcha n.k (2015 - 2020) hiki ndio kizazi cha sita na cha mwisho.

Kwa mtiririko huo, ni vigumu kuona kina Professor Jay, Fid Q hadi kwa kina Joh Makini wakimjibu Khaligraph Jones kwa sababu ni kaka zake katika muziki, ukifuatilia historia ya Khaligraph, yeye anaangukia kizazi cha kina Darassa na Roma.

“Niachie hili chupa (video mpya) au bado mna jambo lenu na Khaligraph Jones?” aliuliza Fid Q kupitia Instagram, Rosa Ree akamjibu kuwa ameshapambana naye, Fid Q akarudi tena na kusema, “Poa... lakini fanyeni mmalize haya mambo ili ratiba nyingine ziendelee.”

Kwa kauli hiyo inaonyesha wazi Fid Q anajua wanaopaswa kumjibu Khaligraph ni kina nani, hawa ni kuanzia kizazi cha tano cha Hip Hop Bongo ambao ni kina Roma, Young Killer hadi kuja kwa kina Rosa Ree na ndio wengi wao wamefanya hivyo. 

Hadi sasa waliomjibu Khaligraph Jones kupitia ngoma zao (diss track) ni Rosa Ree (Mama Omollo), Songa (Kali Sio Jones), Young Killer (Khali Majozi), Motra The Future (Arap Moi Jr) n.k, hawa wote ni kizazi cha tano na sita cha Hip Hop Bongo.

“Wakazi Khaligraph Jones umemsikia lakini? Tunakutegemea ‘genius’ wa muziki au tukuache kidogo bado upo ‘busy’ kufanya uchambuzi mtandaoni,” hii ni kauli ya Diamond Platnumz kupitia X (Twitter) akimtaka Wakazi kumjibu Khaligraph.

Ni wazi Diamond mwenyewe anajua kina Wakazi ambao ni kizazi cha tano ndio wenye wajibu huo na ndio sababu hajawataja kina Noorah, Fid Q, Mr. Blue, Jaffarai, Jay Moe, Solo Thang, Soggy Doggy, Imamu Abbas n.k.

Chanzo: Mwanaspoti