Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prof. Jay, Sugu waliona mbali

7729 PROF JAY34 Prof. Jay, Sugu waliona mbali

Sat, 29 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miaka 18 iliyopita, Professor Jay katika albamu yake ya tatu, J.O.S.E.P.H (2006) alieleza baadhi ya mambo ambayo hayapaswi kuwepo katika Bongo Fleva ila cha ajabu hadi leo yapo kwa namna moja au nyingine.

Kupitia wimbo wake ‘Inatosha’ akimshirikisha Mr. II Sugu, walikemea mienendo yote isiyofaa katika sanaa na kutoa mwongozo jinsi sanaa inavyotakiwa kuwa maana wametoka nayo mbali. 

Utakumbuka Professor Jay alianza kuvuma kimuziki chini ya kundi la Hard Blasters Crew (HBC) baada ya kuja na albamu yao, Funga Kazi (2000) ambayo ilikuwa na nyimbo kali kama Chemsha Bongo, Mamsapu, Kubwa Kuliko n.k.

Sasa Professor Jay anaanza versi ya kwanza katika wimbo ‘Inatosha’ kwa kuwakumbusha wasanii wenzake kuhusu majukumu yao, miongoni mwa hayo ni kukemea maovu na endapo wao ndio watayafanya nani atayakemea?.

“Inatosha kuona nadhani bora kusema, usipoelewa sasa mimi sintorudia tena, Sanaa ni kioo cha jamii toka awali, tumetoka nayo mbali misitu na majabali,” anasema Professor Jay na kuongeza.

“Tukifanya sisi nani atafuta makovu, sanaa inaelea kwenye wingu la visasi, wivu na migogoro ndio vinapata nafasi.” Hapo Professor Jay alijaribu kudadavua vitu ambavyo haviko sawa katika muziki wa Bongo Fleva.

Ukweli ni kwamba ukipiga picha katika tasnia ya sanaa nchini mambo kama haya hadi sasa bado yapo na baadhi ya wasanii hadi leo wanayalalamikia, lakini kwa nini tusiseme; Inatosha Sasa!.

Katika kiitikio cha wimbo huo wanashirikiana wote lakini zaidi anasikika Sugu akieleza yake ya moyoni kuhusu mwenendo wa sanaa kwa ujumla.

“Inatosha sasa tuendeleze tu pilika, tumeshashtuka na muziki ndio unaamka, matatizo yote nyuma; Inatosha Sasa, bifu sijui nini na nini; Inatosha sasa……” anachana Sugu kwa midadi ya kutosha.

Katika vesi ya pili Sugu anatuambia walianza kama utani kufanya muziki na ghafla Rap ikasamba mitaani licha ya kuwa walianza katika mazingira magumu, huku baadhi ya watu wakiona muziki ni uhuni.

“Taratibu tukaanza kuhesabu vimilioni, tukawatoa nishai waliosema Rap ni uhuni”. Ni wazi ndipo ilipo Bongo Fleva kwa sasa na baadhi ya wasani wanapata fedha, si haba na kundi kubwa likiendelea kujikongoja kuelekea huko.

Sugu anaendelea kwa kuwaambia wasanii  wenzake mafanikio kwenye muziki sio tu kupata hereni, mikufu ya dhahabu, balloon na fubu kama wengi walivyodhani kwa miaka hiyo.

Bali muziki ni kama biashara nyingine na inahitaji mahesabu mazuri, huku akigusia suala la hakimiliki kwa wasanii na ugomvi wa kati yao kila mara ambao umekuwa ukiwarudisha nyuma.

“Naamka asubuhi macho yangu gazetini, eti kuna bifu kati ya Afande na O-Ten, washikaji wa East Coast na machizi wa Kiumeni”. Sugu anamaliza kwa kusema; Inatosha Sasa, yote ni kwa faida gani?.

Na katika versi ya tatu, Professor Jay anarudi tena kwa kusema; “Kashfa zako zinauza magazeti ya mwenzako, kuliko hata unavyouza huo muziki wako”. Ingawa Jay hajamtaja wasanii huyo, lakini hadi sasa hilo bado lipo tena kwa sana tu!

Ikumbukwe Professor Jay na Sugu wamewahi kuwa wabunge, mwaka 2015 Sugu aliongoza kwa kuchaguliwa na wapigakura wengi kuliko mbunge yeyote kati ya wabunge 257 waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo akipata kura 108,566.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live