Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi walivyozima onyesho la Sikinde, Msondo

33555 Pic+msondo Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam linadaiwa kutibua onyesho la bendi za muziki wa dansi za  Msondo na Sikinde lililofanyika jana Jumanne Desemba 25, 2018, baada ya kuamuru lisitishwe wakati mashabiki wakiendelea kukata tiketi.

Tukio hilo lilitokea katika Ukumbi wa TCC Club Chang’ombe jijini Dar es Salaam wakati bendi hizo kongwe nchini Tanzania zikitoa burudani.

Onyesho hilo lilianza saa 12 jioni huku bendi hizo zikipanda jukwaani kwa zamu na ilipofika saa 5:45 usiku wakati Sikinde wakiwa jukwaani, kiongozi wa bendi hiyo, Abdallah Hemba alitangaza kuwa onyesho hilo limefika mwisho.

“Mtuwie radhi kutokana na kufuatwa na Polisi sasa hivi. Tumeambiwa tusitishe onyesho kwani mwisho ni saa sita kamili usiku,” amesema Hemba.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 26, 2018 Kamanda wa Polisi wa Temeke, Emmanuel Lukula amesema hakuwepo eneo la tukio, lakini kama polisi walisitisha onyesho hilo saa sita usiku, walikuwa wanatimiza wajibu wao.

Lukula amesema licha ya wanamuziki kudai kuna amri ilitolewa kuwa maonyesho kuendelea hadi saa nane usiku, polisi hawakupewa taarifa.

“Sisi hatuna taarifa hiyo, unajua kuna maelekezo, sheria, kanuni na taratibu. Iwapo tutapewa maelekezo ambayo hayana madhara hatuwezi kukataa, lakini kwa hili hatuna taarifa ya mabadiliko ya muda, ”amesema Lukula.

“Sheria inasema siku za kazi maonyesho mwisho ni saa  tano usiku na siku za mwisho wa wiki maonyesho mwisho ni saa sita usiku.”

Amesema polisi hawatoi vibali, na kwamba wanamuziki wanaokwenda kuomba vibali kama watapewa vinavyozidi muda huo jukumu lao ni kuwafahamisha Polisi ili waimarishe ulinzi kwenye eneo hilo.

Katika maelezo yake Hemba aliwaeleza mashabiki waliofurika katika ukumbi huo kuwa kibali chao kutoka kwa ofisa utamaduni hakijaeleza muda huo waliotakiwa kuzima muziki na polisi.

“Mbona sielewi maana ndio naingia ukumbini nakutana na tangazo kuwa onyesho limekwisha na hata kiti sijapata. Nimelipa Sh10,000 na nimetumia usafiri, hii ni hasara,” amesema Tindwa Salum, shabiki wa muziki wa dansi aliyefika ukumbini hapo.

Kwa mujibu wa Hemba, onyesho hilo lilipaswa kumalizika saa nane usiku badala ya saa sita.



Chanzo: mwananchi.co.tz