Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pepo la usaliti lamwandama Harmonize kila kona

Konde Pic 2 Data Pepo la usaliti lamwandama Harmonize kila kona

Sat, 24 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

AKIWA kwenye jukwaa la Wasafi Festival mwaka 2019, Diamond Platnumz alieleza kwa hisia kali kusalitiwa na mtu wake wa karibuni aitwaye Jeshi.

Huyu alikuwa ni Harmonize ambaye kwa wakati huo ndio tetesi za yeye kujitoa WCB Wasafi zilikuwa zimeshika kasi kwenye mitandao.

Kwa sasa Harmonize hayupo WCB, ana lebo yake, Konde Music Worldwide lakini pepo la usaliti toka wakati huo limekuwa likimwandama kuanzia kwenye muziki hadi mahusiano ya kimapenzi. Ebu tazama!.

1. Diva

Hivi karibuni Harmonize alimtaja Diva kuwa ni miongoni mwa watu aliodai wanamchafua mtandaoni na kueleza atawachukulia hatua za kisheria pamoja na kumlipa fidia ya mabilioni ya fedha.

Hata hivyo Diva miezi kadhaa alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa wanampigania sana Harmonize kila sehemu hasa mtandaoni, hata kwenye uzinduzi wa albamu ya Afro East, Diva alikuwa ni miongoni mwa wageni muhimu (VIP) lakini sasa Diva kamsaliti Harmonize.

Ndiyo kamsaliti! Kwa sasa Diva amejipambanua vilivyo kama shabiki wa Diamond ambaye ni hasimu wa Harmonize kimuziki toka aondoke kwenye lebo yake ya WCB Wasafi. Diva kwa sasa ni timu Chibu Dangote na sio Konde Music, ndicho kinachotajwa kuleta ugomvi kati yake na Harmonize.

2. Rosa Ree

Rapa huyu alikuwa karibu na Harmonize hadi kupelekea kushirikisha kwenye remix ya wimbo ‘Bedroom’ akiwa ndiye msanii pekee wa kike kwenye ngoma hiyo yenye wasanii zaidi ya nane.

Baadaye Rosa Ree akamdondoshea Harmonize kitu kizito kichwani kwa kumshtaki kutumia biti ya wimbo wake ‘Kanyor Aleng’ bila idhini yake, jambo hilo pia likapelekea wimbo wa Harmonize ‘Amen’ kufutwa kwenye mtandao wa YouTube kwa kukiuka taratibu za hakimiliki.

3. Marioo

Mwimbaji huyu naye alionyesha ukaribu sana na Harmonize wakati amejitoa WCB Wasafi, tetesi zikaibuka kuwa angemsaini Marioo kwenye lebo yake ya Konde Music.

Baadaye wakaoneka katika matayarisho ya kufanya video lakini ghafla upepo ukabadilika na bifu la chini kwa chini kati yao likaibuka hadi kupelekea Marioo kufuta picha zote kwenye ukurasa wake wa Instagram alizopiga na Harmonize.

Baadaye Marioo alikiri hawaelewani na Harmonize na hawezi kusaini Konde Music kwani ana mipango yake mikubwa kimuziki.

Kwa sasa Marioo ana ukaribu mkubwa na Diamond ambaye inaelezwa tayari wamefanya wimbo na muda wowote utatoka.

4. Sarah na Wolper

Hivi karibuni Harmonize amewaomba mashabiki wake kumshauri anarudiane na mpenzi wake yupi wa zamani kati ya Sarah na Wolper baada ya kuachana na Kajala.

Hatua hii ndio inaonyesha kuwa pepo la usaliti linamwandama Harmonize kila kona. Kivipi?.

Sarah aliamua kuachana na Harmonize baada ya mwimbaji huyo kuzaa nje ya ndoa yao, utetezi wa Harmonize kuhusu hilo ni kwamba mkewe, Sarah alikuwa nje ya nchi kwa kipindi kirefu hivyo akajikuta akichepuka, yaani kuisaliti ndoa yake hadi kupata mtoto.

Kabla ya Sarah, mpenzi wa Harmonize alikuwa Wolper ambaye alidai kilichoua mapenzi yao ni baada ya kugundua Konde Boy kaanzisha mahusiano ya siri na Sarah, hivyo alikuwa anasaliti penzi lao.

Hata sakata lake na Paula, bado lina viashiria vya usaliti mkubwa ndani yake ndio maana yale yanayodaiwa mazungumzo ya faragha kati yao yameweza kuvuja hadi kuwafikia mahasimu wake kimuziki na kuyatumia kama fimbo ya kumchapia ingawa mwenyewe amekanusha ukweli skuhusu hilo.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz