Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Penzi la Paula na Marioo ni fursa au kisasi?

Paula Kajala Ana Ujauzito Wa Marioo Penzi la Paula na Marioo ni fursa au kisasi?

Thu, 24 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Uhusiano wa Marioo na Paula umegeuka fursa kwa staa huyo wa Bongo Fleva tangu walipoweka wazi kuwa pamoja, ni fursa ambayo wasanii wengi Bongo wamewahi kukumbana nayo na kuitumia vizuri ila kwa kiasi.

Hata hivyo, fursa hiyo kwa upande wa pili inaweza kutafsiriwa kama Paula amemshika mateka Marioo ili kulipiza kisasi, hii ni kutokana na vitu vinaenda kwa haraka sana kinyume na utamaduni wa wengi katika tasnia.

Marioo alianzisha uhusiano na Paula ikiwa ni muda mfupi baada ya binti huyo wa Kajala Masanja na P-Funk Majani kuachana na Rayvanny ambaye ameamua kurejea kwa mzazi mweziye, Fahyma.

Kabla ya Marioo kuwa na Paula, alihusishwa kuwa na uhusiano na Mimi Mars kwa muda ingawa wote walikanusha jambo hilo kwa madai ukaribu wao ni wa kikazi huku wakishirikiana katika nyimbo mbili, Una na La La.

Utakumbuka mwaka 2018 ndipo Marioo aliachia wimbo wake, Dar Kugumu uliyomtoa kimuziki na hadi sasa ametoa albamu moja, The Kid You Know (2022) na kushinda tuzo tatu za muziki Tanzania (TMA) 2021.

Kwa kipindi cha takribani miezi sita walichokuwa pamoja, Marioo ameweza kumtumia Paula katika video za nyimbo zake tatu, ‘Lonely’, ‘Tomorrow’ na ‘Sing’ ambayo imetoka hivi karibuni.

Ujio wa Paula katika maisha ya Marioo umekuwa ni fursa upande wa kazi yake, anajua umaarufu na sura nzuri ya mrembo huyo ni bidhaa inayotazamwa zaidi kwa sasa katika soko la burudani Bongo, hivyo kuihusisha na muziki wake itamrahisishia kuuza.

Ndicho alichofanya na Rayvanny ambaye alimtumia Paula katika video ya wimbo wake, Wanaweweseka kutoka katika EP yake ya tatu, Flowers II (2022) ila wakaachana muda mfupi tu baada ya video hiyo kutoka.

Hata hivyo, wakati Marioo akimwona Paula kama fursa ya kusukuma muziki wake mbele, Paula naye hiyo ni fursa kwake kulipiza kisasi kwa aliyekuwa mpenzi wake, Rayvanny, ili kufanikisha azma yake, ni lazima Marioo awe mateka kwanza.

Tangu Marioo amekuwa na Paula hajafanya video na mrembo mwingine yeyote yule, kila video inayotoka ni yeye Paula tu!, cha kufurahisha au kushangaza ni video hizo tatu zimetoka kwa kufuatana ndani ya kipindi cha takribani miezi miwili!. 

Hii ni tofauti na wasanii wengine Bongo kama Diamond Platnumz, Harmonize na Rayvanny ambao wamewahi kufanya video zaidi ya moja na wapenzi wao, hawa walikuwa wanazipishanisha hata miaka miwili na kuzingatia maudhui ya wimbo husika.

Mathalan Diamond alimtumia Zari The Bosslady katika video ya wimbo wake, Utanipenda (2015), kisha akajipa muda kwa kufanya video nyingine ndipo akaja kumtumia tena Zari katika video ya wimbo, Iyena (2018) ikiwa imepisha miaka mitatu na ile ya kwanza.

Ila kwa Marioo imekuwa ni tofauti sana, huwenda penzi limemkolea vilivyo na sasa kageuka mateka, mfano video ya wimbo, Tomorrow ambayo imeongozwa na Director Kenny, hakukuwa na ulazima wa Paula kuwepo kutokana na maudhui ya wimbo huo.

Paula anajua kuonekana katika video za Marioo mara kwa mara atakuwa amelipiza kisasi kwa Rayvanny, mwanamume wa kwanza katika maisha yake ambaye alikuja kuuvunja vibaya moyo wake, hiyo ni kwa mujibu wa ujumbe wake wa Mei mwaka huu.

Utakumbuka Rayvanny amekuwa na utamaduni wa kumtumia mpenzi wake, Fahyma katika video za nyimbo zake ambazo hadi sasa zimefika tano, video hizo ni Kwetu (2016), Natafuta Kiki (2016), Siri (2017), Forever (2023) na Habibi (2023).

Hapa ndipo ligi ya kulipiza kisasi kati ya Paula na Rayvanny ilipo, hii ni kwa sababu baada ya Paula kuonekana katika video mbili za Marioo, Lonely na Tomorrow ambazo zilitoka kwa kufuata, Rayvanny alijibu mapigo mara moja!.

Rayvanny alijibu mapigo hayo kwa kumtumia mpenzi wake, Fahyma katika video zake mbili, Forever na Habibi ambazo nazo hajapishana sana muda wa kutoka, hii ni mara ya kwanza Rayvanny kufanya video mbili na Fahyma ndani ya mwaka mmoja.

Kutokana na hilo, kuna uwezekano mkubwa wa kuja kumwona tena Paula katika video nyingine ya Marioo huko mbeleni, pia Fahyma katika video nyingine ya Rayvanny.

Paula ambaye anafanya reality show, Behind The Gramy na mama yake, Kajala, amekuwa akionyesha mtandaoni kujitoa sana katika uhusiano huu kuliko ilivyokuwa ule wa Rayvanny na hivi karibuni kaeleza Marioo ndiye anatembea na roho yake.

Ni Marioo huyu ambaye aliwahi kulia machozi mbele ya Dully Sykes baada ya kupigiwa simu na mama yake mzazi na kumtaka kuachana na muziki na ajikite kwenye kazi ya kuchomelea (gereji) kwani muziki hauwezi kumlipa ila sasa ni mwanamuziki mkubwa nchini.

Chanzo: Mwanaspoti