Inaelekea kutimia miaka mitatu tangu Staa wa Bongofleva, Zuchu kusainiwa WCB Wasafi yake Diamond Platnumz akiwa ni msanii wa pili wa kike ndani ya Lebo hiyo baada ya Queen Darleen.
Kiziwanda huyo wa Malkia wa Taarab Tanzania, Khadija Kopa, pia ndiye kiziwanda wa WCB Wasafi kwa maana tangu asainiwe Aprili 2020 hakuna msanii mwingine aliyetambulishwa licha ya kuwepo ahadi za kufanyika hilo.
Mtoto wa aliyekuwa Gwiji wa muziki Tanzania, Banza Stone, Hanstone ndiye alikuwa anatajwa angefuata muda mfupi baada ya Zuchu ila mambo kati yake na WCB Wasafi yakavurugika dakika za mwisho na hadi sasa hakuna upande ambao umekubali kuzungumza.
Uwekezaji uliofanywa kwa Zuchu umepelekea kuwa Staa mkubwa wa muziki Afrika Mashariki ndani ya muda mfupi, ndiye msanii wa kwanza wa kike ukanda huo video ya wimbo wake (Sukari) kupata ‘views’ zaidi ya milioni 80 YouTube, huku ikiwa ngoma pekee ya ‘solo’ yenye mafanikio hayo.
Rekodi nyingine ni kama; kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube, pia ndiye wa kwanza kufikisha ‘streams’ milioni 100 Boomplay Music.
Utakumbuka EP yake ‘I Am Zuchu’ yenye nyimbo saba ilikaa tano bora kwenye chati za Boomplay Album kwa wiki 75, huku ukishika namba moja kwa wiki 35, hakuna msanii wa kike Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo, ni Zuchu pekee!.
Hadi sasa tayari Zuchu amefikisha ‘views’ zaidi ya milioni 431.0 YouTube na kuwa msanii wa kike namba tatu kusini mwa Jangwa la Sahara, wanaomtangulia ni Sinach (views milioni 721.7) na Yemi Alade (milioni 694.4), wote hawa ni kutokea nchini Nigeria.
Pia ameshinda tuzo mbili za African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora Chipukizi (2020) na Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki (2022), huku akiteuliwa kuwania MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2022.
Pengine mafanikio ya muda mfupi yamepelekea Zuchu kuwa mbinafsi sana, kama sio yeye, basi WCB Wasafi ndio wamemfanya kuwa hivyo ili kulinda chapa yake kutozoeleka na kuchokwa mapema katika soko. Je, ni kwa namna gani hasa na kwanin?.
Tangu ametoka kimuziki, Zuchu hawashirikishi kabisa wasanii wa Bongofleva nje ya WCB Wasafi katika nyimbo zake!, hata wa WCB waliopata nafasi hiyo ni wawili tu; Diamond na Mbosso licha ya kuikuta Lebo hiyo na wasanii watano.
Kwa ujumla wasanii wa Tanzania ambao Zuchu amewahi kuwashirikisha ni wa tatu tu; Diamond, Mbosso na Khadija Kopa ambaye ni mama yake mzazi, huku wa kimataifa wakiwa ni wanne; Joeboy na Adekunle Gold kutokea Nigeria, pia kuna Bontle Smith na Tyler ICU kutokea Afrika Kusini.
Jux ndiye msanii pekee wa Bongofleva nje ya WCB Wasafi aliyefanikiwa kuinasa sauti ya Zuchu ambaye amesikika kwenye wimbo wake ‘Nidhibithiti’ unaopatikana katika albamu ya pili, King of Hearts (2022).
Hakuna ubishi kuwa Jux ameweza hilo kutokana na ukaribu wake wa kikazi na Diamond ambaye naye alisikika kwenye wimbo wake ‘Sugua’ unaopatikana katika albamu yake ya kwanza, The Love Album (2020).
Kwa asilimia kubwa Zuchu anacheza uwanja wa nyumbani; WCB Wasafi, huku ni Diamond, Mbosso na Rayvanny pekee ndio wamefanikiwa kumshirikisha, Lava Lava na Queen Darleen bado wanasotea benchi.
Pengine Zuchu na WCB Wasafi wanajua nguvu ya ushawishi alinayo kwa sasa, hivyo wameamua upepo huo uwanufaishe wao pekee, mathalani, wimbo ‘Mtasubiri’ aliyoshirikishwa na Diamond ndio uliofanya vizuri zaidi katika EP ya Chibu, First of All (FOA), video yake ndio iliyoongoza kutazamwa YouTube Tanzania mwaka 2022 ikiwa na ‘views’ zaidi milioni 23.
Rayvanny ambaye kabla ya kuondoka WCB Wasafi alimshirikisha Zuchu katika nyimbo zake mbili, ni mfano halisi wa jambo hilo, video ya kolabo yao ‘Number One’, ndio video pekee ya Rayvanny iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ikiwa na ‘views’ zaidi milioni 75 ikiwa ni miaka miwili tangu kutoka kwake.
Hivyo hivyo upande wa kimataifa, ni wasanii wawili tu ambao wamebahatika kuinasa sauti yake; Spice Diana (Uganda) na Olakira (Nigeria).
Ikumbukwe kipindi cha nyuma baada ya Diamond kuanza kuwasaini wasanii WCB Wasafi mwaka 2015, alikosolewa sana kwa tabia yake ya kufanya kazi na wasanii wa Lebo hiyo pekee ndani ya Bongofleva, ila baadaye akabadilika ndipo akaja kusikika kwenye ngoma za wasanii kama AY, Fid Q, Navy Kenzo, Jux, Baba Levo na Barnaba.