Pendekezo la kumlipa mchekeshaji aliyeshinda tuzo ya Emmy Trevor Noah randi milioni 33 ($1.7m, £1.3m) ili kuitangaza Afrika Kusini kama kivutio cha kitalii limesababisha mvutano nchini humo.
Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini Patricia de Lille aliliambia bunge kuhusu mipango ya kumlipa Noah ili kushiriki katika video ya dakika tano inayotangaza utalii wa Afrika Kusini.
Wabunge wengi wamepinga pendekezo hilo, lakini Bi de Lille anasema kuwa mchekeshaji huyo wa Afrika Kusini na mtangazaji wa TV hatalipwa kwa kutumia fedha za umma.
Alisema kuwa atalipwa kwa kutumia fedha binafsi kutoka Baraza la Biashara la Utalii la Afrika Kusini, shirika mwamvuli linalowakilisha wadau wa usafiri na utalii wa nchi hiyo.
Baadhi ya Waafrika Kusini pia wamekosoa mpango huo uliopangwa kupitia mitandao ya kijamii wakisema mpango huo haufai.
Wakati wengine wakidai muda wake haujalishi kwani Waafrika Kusini wengi wanatatizika kifedha. “Tunatarajia serikali isipoteze pesa ambazo hatuna kwa vitu visivyo na maana. Hatujali jinsi alivyo, nchi iko katika hali mbaya. Hakuna umeme, hakuna ajira lakini wana milioni 33 za kumpa Trevor Noah.
Trevor Noah amechangia nini katika kuboresha nchi hii,” mtumiaji mmoja wa Twitter aliuliza. Hata hivyo, Waafrika Kusini wengine wanasema kuwa nyota ya Noah ya Hollywood inaweza kukuza utalii wa Afrika Kusini.
Mnamo Machi mwaka huu, Noah na gwiji wa tenisi Roger Federer, ambao wote raia wa Afrika Kusini na Uswizi, waliigiza katika kampeni ya kuitangaza Uswizi kama mahali pa kusafiri.