Paula Kajala amefunguka hataweza kamwe kumchagulia mwanaye Amara kazi ya kufanya na atachagua mwenyewe kwani hata ya muziki kwake itakuwa freshi tu hatampangia.
Paula ambaye amezaa na nyota wa Bongo Fleva, Marioo ameliambia Mwanaspoti lililotaka kujua kama mwanaye atafuata nyayo zake au za baba yake au nyingine, ndipo alipujibu ataamua mwenyewe cha kufanya.
"Mwanangu afanye kazi ya baba yake au nyingine sawa tu, maana sitakuwa namtendea haki, Mungu ndiye anayejua alichompangia, hivyo atakachopenda mimi kama mama nitamsapoti atapohitaji awe nani na nitamwelekeza vizuri mtoto wangu,” amesema Paula.
Amesema baada ya kupata mtoto huyo hafikirii kuishia hapo kwani bado ana safari ya kuendelea kupata watoto wengine na Marioo.
"Idadi ya watoto sina hesabu ninazoweza kukupa napenda watoto wengi zaidi, ninao mpango wa kuongeza mtoto mwingine huko mbeleni na baba mtoto wangu Marioo.”