Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Paul James ‘PJ’ aziba pengo la Ephraim Kibonde

47352 PJ+pic

Tue, 19 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mtangazaji wa Clouds Media Group, Paul James 'PJ' ambaye alikuwa anatangaza kipindi cha Power Breakfast katika sehemu ya kuperuzi na kudadisi, ameziba pengo la Ephraim Kibonde aliyekuwa mmoja wa watangazaji wa kipindi cha Jahazi.

Mabadiliko hayo yamefanyika leo Jumatatu Machi 18, 2019, baada ya siku takriban 12 kupita tangu Kibonde alipofariki dunia. Kibonde alikuwa akitangaza pamoja na Gadner G Habashi na George Bantu.

Akizungumza na Mwananchi, Gadner Habashi amesema kutokana na kipindi chao cha Jahazi maarufu ‘Utatu mtukutu’ kuwa na upungufu wa mtu mmoja baada ya Kibonde kufariki, hivyo wameona waongeze ili itimie idadi yao ya watangazaji watatu kama mwanzo.

Gadner amesema kitendo cha kumchukua PJ kutoka kipindi cha Power Breakfast na kuja Jahazi ni kama wamemrejesha kwani hapo mwanzo alikuwa kati ya watangazaji wa mwanzo kabisa kutangaza kipindi hicho, ambapo walikuwa Gadner Habashi, Ephraim Kibonde na Paul James na baada ya hapo alihamia Power Breakfast.

"Ni kweli kabisa PJ tuko naye hapa Jahazi, niseme tu PJ amerudi nyumbani, kwani mwanzo wa kipindi kinaanzishwa alikuwa mmoja wa watangazaji wa kipindi hiki.”

“Tulikuwa watatu mimi, Kibonde na PJ, baada ya muda PJ akahamia kipindi cha Breakfast akaungana na kina Masoud Kipanya."

Hata hivyo, kipindi cha Jahazi kikiwa hewani, Mwananchi imemsikia mtangazaji wa kipindi cha Power Breakfast, Masoud Kipanya akipiga simu katika kipindi cha Jahazi na kusema ameshtushwa sana na taarifa za PJ kuhamia kwenye Jahazi.

"Nasema hivi sisi kama Power Breakfast tumeumia hasa kutokana na 'ukweli' kwamba kuna mali zetu nyingi tulikuwa tumempa PJ lakini sasa tutampokonya na tunasema Power Breakfast haiwezi kutetereka,” amesema.  

 Masoud ameendelea kusikika akisema, "Kesho tutaitisha mkutano na waandishi wa habari, lakini ifahamike sisi Power Breakfast tuna nguvu ya kumchukua mtu yeyote kutoka sehemu yoyote na kesho tunatangaza tumemchukua nani na hatushindwi kumchukua Gadner Habash au George Bantu."



Chanzo: mwananchi.co.tz