Miongo miwili mpaka mitano iliyopita Muziki wa mwambao 'taarabu' asili nchini Tanzania ulivuma na kuwapa majina makubwa wanamuziki wake.
Mmoja wa wanamuziki hao ni mkongwe Patricia Hillary aliyetamba na nyimbo kama vile njiwa, jamani mapenzi na ni mdodo.
Patricia Hillary, mstaafu wa jeshi, aliyedumu kwenye muziki huu kwa zaidi ya miaka 40 safari yake ya muziki ni somo na funzo kubwa kwa waimbaji wa sasa wa taarabu.
Haya ni mambo matano ambayo hayajulikani sana kumhusu.
Afisa wa jeshi Mstaafu
Kipaji chake cha uimbaji wa taarabu asilia kilifunguliwa njia na Jeshi baada ya kumaliza chuo mwaka wa pili.
Alianza kuimba kanisani mkoani Tanga lakini mwaka 1980 wakati Jeshi likizunguka mikoani kutafuta vipaji lilifika mkoani humo na kuongea na mwenyekiti wa kijiji wakati huo ambaye pia alikuwa baba yake mkubwa na kiongozi wa ngoma ya Mdumange na alimchagua yeye.
"Aliambiwa tunahitaji binti mwenye heshima anayejielewa, tunataka kwenda naye jeshini mwenye adabu, moja kwa moja niliitwa” alisema Patricia
Anasema baba yake alimwambia amechaguliwa kwenda kuwakilisha ngoma ya mdumange lakini hakuwa amewahi kuicheza hiyo ngoma zaidi ya kuimba kwaya kanisani.
"Walikaa kama siku tatu, nikawa naelekezwa na baba yangu nitakavyoimba, na baadaye walikubali wakasema huyu atatufaa mpaka kwenye taarabu”
Hapo ndipo safari yake ilipoanzia, mgambo Tanga ilikuwa kambi yake ya kwanza na akafanikiwa kufanya nyimbo yake ya kwanza ‘mpenzi wangu wa jua’ baadaye walifiki Dar es Salaam na alipofika ndipo alipotengeneza nyimbo ya Njiwa.
Kanisa, wazazi hawakutaka aondoke
Alipochaguliwa na jeshi mwaka 1980, wazazi wake ilikuwa ngumu kumuachilia lakini pia kanisa alilokuwa kisali na kuimba kwaya kabla ya hapo iliwaumiza.
"Niliwaambia nahitaji kwenda kutafuta maisha ntarudi, wengi waliumia kwanini anaondoka walizuningumzia sana lakini niliwaambia na kwenda kuiwakilisha Tanga walisikitika”
Alikuwa ndio mwanamke pekee kuchaguliwa katika eneo alilokuwepo la Korogwe huku wengi zaidi walikuwa wanaume.
Kwa sasa wanajivunia sana kuhusu yeye "Hawafanyi chochote bila kunitafuta hata kama kuna harusi watanitafuta niende nikaimbe”
Siri ya sauti isiyochuja
Sauti ya Shakira unaweza kusema ndio ile ya kumtoa nyoka pangoni, katika miaka yake 40 ya uimbaji sauti yake ipo vile vile, ya kuvutia na inanguvu ile ile aliyoimba Njiwa mwaka 1980.
“Naitunza sana sauti yangu mimi nina vitu situmii kabisa kutokana na kuitunza hii sauti yangu maana ndio mtaji wangu na ndio ofisi yangu”
Patricia anasema hatumii kabisa maji baridi, vinywaji vikali ili kuitunza sauti yake lakini pia anafuata masharti kama vile kutokukaa muda mrefu bila kuimba
“Uimbaji pia unamasharti na nayafuata, hutakiwi kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi”
Familia yake ndio timu yake ya muziki
Alijaaliwa kupata watoto wawili na mume wake ambaye ni marehemu kwa sasa na baadaye mtoto wake mmoja alifariki kwa ajali na kubaki na mtoto mmoja
Lakini Patricia anasema mbali na mtoto wake wa kumzaa, ana kundi kubwa la vijana anaoishi nao kama watoto wake ambao ni watoto alioachiwa na wadogo zake na amewalea mwenyewe.
“Nilijaaliwa watoto wawili lakini nina watoto wengi nimachiwa na wadogo zangu, nimewalea mwenyewe na ndio wamiliki wa kila kitu changu katika muziki”
Anasema katika timu yake hiyo kuna wanamuziki, meneja na watayarishaji wa muziki pamoja wasimamizi wa shughuli zote za muziki wake
Anavutiwa na Shakira Saidi
"Nilikuwa napenda sana uimbaji wa Shakira Saidi, alikuwa ni muimbaji mzuri Afrika Mashariki”
Shakira saidi alimvutia zaidi kuingia katika taarabu na moja ya nyimbo zake alizokuwa akizipenda kutoka kwake ni ‘akukatae hakwambii toka’
"Alikuwa na nyingi kama viva Frelimo, mapenzi ni kama donda alinivutia kwa vitu vingi”
Mwaka 2016 alistaafu Jeshi na kuendelea na shughuli binafsi za uimbaji wa taarabu ambapo kwa sasa anajivunia kuimba katika hafla mbalimbali za serikali anazopata mialiko, matamasha ya taarabu, harusi na hata katika majukwaa makubwa ya muziki kama Sauti za Busara.