Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Pamoja na cheo, Jokate ni yuleyule mnayemjua’

29784 Jokate+pc TanzaniaWeb

Mon, 3 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapomtaja mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo huwezi kuizuia akili kuwaza licha ya kuwa mheshimiwa aliwahi kuwa staa kupitia filamu na muziki na kushiriki Miss Tanzania 2006 ambako alishika nafasi ya pili.

Miongoni mwa mambo anayoyafanya na kuyahusudu pamoja na kuwatumikia wananchi wa Kisarawe kama mkuu wao wa wilaya, bado anatamani kuwaambukiza fani yake vya usanii ambayo anaamini haichuji kama upo nayo.

Swali: Umeteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ukitokea kwenye ustaa, hukupata shida kubadili aina ya mavazi kutokana na nafasi uliyokuwa nayo?

Jokate: Hapana. Haikuwa taabu, nimesoma shule za kanisa hivyo mavazi ni jambo linalosimamiwa sana, ingawa mama yangu alikuwa ananiruhusu kuvaa suruali kanisani, lakini alikuwa akinitizama aina ya mavazi ninayovaa. Hivyo sikupata taabu nilifanya kitu nilichowahi kukifanya katika makuzi yangu.

Kikubwa zaidi Mungu amenijaalia kuzoea mazingira haraka, kuhama kutoka katika hali fulani kwenda nyingine kwangu ni rahisi kuliko kitu chochote.

Swali: Umeachana kabisa sanaa?

Jokate: Sanaa ipo kwenye damu na ni chanzo cha ajira siwezi kuiacha. Ndiyo maana hivi karibuni nitaanza kupiga picha kwa ajili ya filamu yangu mpya. Nitawashirikisha Gabo Zigamba na Nandy nataka awepo.

Unajua sanaa ni namna unavyoitumia, unaweza kuwa mheshimiwa ukatumia sanaa kuhamasisha maendeleo, amani, maelewano hivyo siwezi kuiacha.

Swali: Unawasaidia wasanii?

Jokate: Yap! Juzi Nandy na Mwasiti walikuja kupiga picha ya nyimbo zao, unajua wasanii wana changamoto ya kupata mahali pa kupigia picha kama vile mahakamani na Polisi.

Lakini nimezungumza na Mohamed Allaraqya maarufu Raqey ninataka kutoa mafunzo ya kutayarisha video na masuala ya ubunifu, nimeshamuandikia barua ya wazo hilo, akiwa tayari tutafanya mchujo wa vijana wenye vipaji ili kuviendeleza.

Lengo ni kuhakikisha ajira inayopatikana kwenye ulimwengu wa dijitali inawafikia na vijana wa Kisarawe.

Pia nimezungumza na Raqey namna ya kufanya, nataka tuwe na kituo cha kupigia picha za filamu huku watu wawe wanakuja wanapiga picha.

Lakini pia tunaweza kutayarisha programu nzuri na zikawauzwa kwenye vituo vya televisheni.

Sifa za kufanya hivyo zipo kwanza kumetulia hakuna heka heka, pili ukitaka eneo la mjini lipo na la kijijini lipo, hivyo inakuwa rahisi.

Swali: Unaionaje tasnia ya filamu kwa sasa?

Jokate: Bahati mbaya vinara wa filamu waliolikamata soko hawaoni kama ni sehemu ya kutoka au endelevu.

Wapo wasanii wa filamu makini na wanaotamani kuifikisha tasnia mbali kama Gabo. Lakini wengi bado hawatamani kuibadilisha ili iwepo muda mrefu.

Hii ndiyo tofauti ya filamu na muziki. Walio kwenye muziki kila siku wanafanya vitu vipya ikiwamo kuwekeza. Wamegundua kuimba suala moja, lakini kuwa na video nzuri ni muhimu kwa sababu dunia imebadilika watu wanataka kusikia na kuona, wamefanikiwa na kila mmoja anataka wimbo wake uwe na video kali.

Waigizaji wa Nollywood wamefanikiwa badala ya kuitumia kama sehemu ya kupata umaarufu, wameitumia kama sehemu ya kuendelea ambapo walioona hawafanyi vizuri kwenye kuigiza wamekwenda kusoma na sasa ni watayarishaji mahiri.

Swali: Wasanii kushuka hususani wa kike kunatokana na nini?

Jokate: Siwezi kulisemea hilo kwa sababu kila mmoja anajua kwa nini alianguka.

Hiyo ni kawaida kwenye sanaa lazima utashuka, kuna wasanii walikuwa na majina makubwa kama msanii wa Marekani Ashanti Douglas walikuwa juu na wakashuka.

Lazima tufahamu hii ni biashara jambo la kwanza ni kujenga brand yako kisha kuilinda na kila siku kuja na kitu kipya.

Wasanii kama Beyonce Knowles na Shawn Carter maarufu Jay Z wamejitahidi kulinda walichokianzisha

Siyo lazima utoke kwenye mstari wa kazi yako, lakini unafanya vitu vingine kuhakikisha unaendelea kuwepo.

Kwa mfano Diamond asingekuwa na nguvu leo kama asingekuwa na wanamuziki ambao wapo wanaoimba kama yeye, wapo wanaoimba kwa namna nyingine kwa maana ya aina mbalimbali za muziki. Mtu hawezi kuwakwepa kila ladha ya muziki unayoitaka leo hii utaipata WCB ina maana ametengeneza mnyororo wa thamani kwenye kazi yake na bado anawekeza, lakini kupitia jina lake.

Kuna mifano ya kampuni zina miaka mingi lakini bado zipo na ubora wao umeendelea kuwa ule ule ikiwamo Coca Cola, Panasonic na Gilette zina miaka 100 kinachofanyika ni kuboresha matangazo na kuongeza ubunifu.

Swali: Unadhani wasanii wa hapa nyumbani wanakosa nini?

Jokate: Siwezi kusema kuna kitu wanakosa. Ila ninasema kuwa jambo la msingi ni kukubali kuwekeza ndani yako, kisha watu wengine waje kuwekeza kwako. Hakikisha unaitafiti kazi yako ikiwamo sanaa, ukiona kuna haja ya kujifunza kuongeza ujuzi nenda kafanye hivyo.

Hakikisha kila siku brand yako ambayo ni wewe mwenyewe inakuwa na kitu kipya ili kuwavutia wawekezaji, tena kwa wasanii ni rahisi sana wanaweza kupata dili za matangazo. Usikubali kukaa na kipaji kisichokukutanisha na fursa nyingine, fanya tafiti ujue kipaji chako kitakupa fursa zipi, zifukuzie hizo.

Lakini cha muhimu na kuzingatia jifunze vitu vipya, kuwa mbunifu na jiandae kwa yajayo.

Ipo mifano halisi mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu aliyewahi kuchezea katika National Basketball Association (NBA) Shaquille Rashaun O’Neal maarufu “Shaq” alijipanga kwa yajayo kwa kutengeneza mipango mapema.

Alipoona mpira wake umekwisha alikwenda kusoma na sasa ni mtaalamu anachambua michezo kwenye runinga na ana programu maarufu iitwayo Inside the NBA kwenye kituo cha TNT.

Swali: Unatajwa kuwa ni miongoni mwa viongozi wanaonyuka pamba. Nani anakuvalisha?

Jokate: (Kicheko...Navalishwa na Kitupe, Mac Touture nikitaka nguo za usiku na Jackies visketi na vigauni ananivalisha yeye.

Napenda kuwaunga mkono wabunifu wa ndani kwa sababu na mimi nimetokea huko.

Swali: Hupati taabu kuishi huku, ukizingatia umeishi muda mwingi jijini Dar es Salaam?

Jokate: Kicheko...Hapana. Ninapenda kuishi huku kwa sababu kumetulia, hewa ipo ya kutosha na ndiyo maana unaniona nime-relax.



Chanzo: mwananchi.co.tz