Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Pacha walivyokutana TikTok tangu walipouzwa mwaka 2002

Anoo And Amy.png Amy na Ano

Mon, 29 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna mtu aliwahi kusema katika dunia hii ogopa Mungu na teknolojia na hivi ndivyo ilivyotokea kwa Amy na Ano, pacha waliokutana kupitia mtandao wa TikTok baada ya kutengana kwa takriban miaka 20.

Baada ya kuzaliwa, pacha hao walichukuliwa kutoka kwa mama yao na kuuzwa kwa familia tofauti mwaka 2002.

Miaka kadhaa baadaye, walijuana kwa bahati kupitia onyesho la vipaji la runinga na video ya TikTok.

Kwa mujibu wa BBC, Amy na Ano walianza kujuana wakiwa na 12. Amy Khvitia akiwa nyumbani kwa mama yake mlezi akitazama kipindi anachokipenda cha televisheni cha kutafuta vipaji cha ‘Georgia's Got Talent’.

Wakati akitazama kipindi hicho, alimwona msichana anayefanana naye karibu kila kitu akicheza muziki.

“Watu walimpigia simu mama yangu na kumuuliza kwanini Amy yuko katika mashindano na anatumia jina jingine?” amesema Amy huku akieleza kuwa familia yake ilipuuza.

Miaka saba baadaye, Novemba 2021, Amy alichapisha video akiwa na nywele za bluu kwenye mtandao wa TikTok.

Baada ya kuchapisha video hiyo, pacha wake Ano Sartania ambaye kwa wakati huo alikuwa na miaka 19, alitumiwa video hiyo na rafiki yake baada ya kuona wamefanana.

Jambo hilo lilimfanya Ano kuanza kujaribu kumtafuta Amy mtandaoni, lakini hakumpata, hivyo aliamua kuweka video hiyo kwenye kundi la mtandao wa WhatsApp la chuo ili kuona kama kuna yeyote angeweza kumsaidia.

Mtu aliyemfahamu Amy aliona ujumbe huo na kuwaunganisha kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Baada ya kuunganishwa na kujuana, Amy alijua Ano ndiye msichana aliyemuona miaka kadhaa iliyopita kwenye Georgia's Got Talent.

“Nimekutafuta kwa muda mrefu!” alimtumia ujumbe. “Mimi pia,” alisema Ano.

Wote wawili walizaliwa katika hospitali ya wazazi ya Kirtskhi ambayo haipo tena, magharibi mwa Georgia, kwa mujibu wa vyeti vyao vya kuzaliwa, siku zao zilitofautiana kwa wiki kadhaa.

Hata hivyo, wana vitu vinavyofanana, wote wanapenda muziki, kucheza na mitindo yao ya nywele inafanana, pia wote wamegundua wana ugonjwa wa vinasaba wa mifupa unaoitwa ‘dysplasia’.

Baada ya kujuana kupitia mtandao wa Facebook, walipanga kukutana wiki moja baadaye.

“Ilikuwa kama kujiangalia kwenye kioo, uso ule ule, sauti ile ile. Mimi ni yeye na yeye ni mimi,” amesema Amy.

“Sipendi kukumbatiwa, lakini nilimkumbatia,” amesema Ano.

Waliamua kuzungumza na familia zao na kwa mara ya kwanza wakaelezwa ukweli kuwa waliasiliwa na familia tofauti, kwa tofauti ya wiki, mwaka 2002.

Amy alikasirika na kuhisi maisha yake yote yamekuwa ya uongo na hata walipohoji zaidi waligundua maelezo ya vyeti vyao rasmi vya kuzaliwa, ikiwemo tarehe waliyozaliwa, hayakuwa sahihi.

Mama mlezi wa Amy alipoulizwa juu ya suala hilo, amesema kutokana na kushindwa kupata mtoto, rafiki yake alimwambia kuna mtoto asiye na wazazi katika hospitali ya eneo hilo, lakini ili kumpata mtoto huyo atatakiwa kuwalipa madaktari na amchukue ili amlee kama mwanaye.

Mama yake Ano naye amesimuliwa hivyo hivyo, lakini hakuna hata familia moja kati ya walioasili iliyojua kuwa watoto hao walikuwa pacha, licha ya kulipa fedha nyingi kuwaasili mabinti zao huku wakieleza kuwa hawakutambua ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, hakuna familia iliyofichua ni kiasi gani walilipa. Pacha hao hawakujua ikiwa wazazi wao waliowazaa waliwauza kwa makusudi kupata fedha ama la.

Kutokana na suala hilo, Amy ameamua kumtafuta mama yao mzazi ili kujua ukweli, lakini Ano hakuwa na uhakika kama anataka kuonana naye. “Kwanini unataka kukutana na mtu ambaye alitusaliti?” ameuliza.

Amy alitumia kundi la Facebook lililojitolea kuunganisha familia za Georgia na watoto wanaoshukiwa kuasiliwa kinyume cha sheria wakati wa kuzaliwa na amechapisha mkasa wao.

Msichana mmoja nchini Ujerumani amejibu akisema mama yake alijifungua watoto pacha wa kike katika Hospitali ya Wazazi ya Kirtskhi mwaka 2002 na aliambiwa wamefariki, lakini sasa ana mashaka.

Vipimo vya DNA vimebainisha kuwa msichana huyo kutoka kundi la Facebook alikuwa dada yao na alikuwa akiishi na mama yao mzazi, Aza, nchini Ujerumani.

Amy alitamani kukutana na Aza, lakini Ano alikuwa na mashaka. “Huyu ni mtu ambaye alikuuza, hatakwambia ukweli,” ameonya. Hata hivyo, amekubali kwenda Ujerumani na Amy.

Walipokuwa katika hoteli huko Leipzig, Amy na Ano walikutana na mama yao mzazi ambaye aliwaeleza ilivyokuwa huku akibainisha kuwa baada ya kujifungua alizimia.

Alipozinduka, wafanyakazi wa hospitali walimwambia muda mfupi baada ya watoto hao kuzaliwa, walifariki. Amesema kukutana na Amy na Ano kumeyafanya maisha yake kuwa na maana mpya. Ingawa hawako karibu, bado wanawasiliana.

Chanzo: Mwanaspoti