Ommy Dimpoz; ni msanii wa Bongo Fleva, ambaye baada ya kujigamba kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kupiga picha na baadhi ya mastaa wa soka katika Ligi Kuu ya Uingereza, Watanzania sasa ni kama wamechoka na kitendo hicho cha kujigamba na kama walivyokosa kukaa na neno moyoni, wameamua kumtemea mbovu.
Dimpoz alikuwa miongoni mwa mashabiki waliohudhuria mechi kali kati ya miamba wa Uingereza, Liverpool na watani wao wa jadi, Manchester Unted katika uwanja wa kihistoria wa Old Trafford.
Baada ya mechi hiyo, Dimpoz aliwafuata wachezaji mbalimbali na kuomba kupiga nao picha ambapo amekuwa akiziposti kwa mbwembwe mno, mwanzo akianza na ile aliyochukua na nguli wa kandanda duniani, Cristiano Ronaldo.
Ijumaa tena Dimpozi aliendelea kuziposti picha hizo tu ambapo aliachia moja akiwa na mshambuliaji wa Misri, Mohammed Salah ambaye anakipiga Liverpool na msururu huo wa kuposti picha ni kama umewafika kwenye koo watu na wamempasha kwa njia zote.
“Ommy Dimpoz kaka imetosha sasa tunajua umekutana nao wote,” shabiki wake mmoja alimwambia.
Wengine walimtania jinsi alivyokuwa akiwasubiria wachezaji hao na kuomba picha nao hasa kwa lugha ya Kingereza.
“Siku tatu unaishi uwanjani kusubiria picha. Umefanya jambo la kishujaa sana mpwa. Nawaza tu spidi uliyokuwa unatumia ya kutoka hapa kwenda pale kupata picha na lugha sasa…” Mwingine aliandika akimalizia na emoji za kucheka.
“Ulikaa geti la kuingia unaomba picha? Umekuwa ombaomba Ulaya,” mwingine alimjia juu Dimpoz na kumfanya kujibu; “Acha makasiriko, sema nikupe connection upige picha hata ya Mayele (mshambuliaji hatari wa timu ya Yanga ya Tanzania).”