Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ommy Dimpoz Kujimilikisha Youtube kwa muda

49503 Pic+ommy

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kati ya orodha ya wasanii 10 wanaotamba katika muziki wa Bongo Fleva kwa takribani miaka mitano jina la Ommy Dimpoz haliwezi kukosekana. Nyimbo kama Nai Nai, Me and You, Tupogo, Baadae, Yanje na ni Wewe ni baadhi ya kazi zilizomuweka juu kwa miaka.

Februari 4, mwaka huu alitoa wimbo Ni Wewe ikiwa ni shukrani baada ya kuwa kitandani kwa zaidi ya miezi sita akisumbuliwa na tatizo la koo.

Mapema wiki hii ametoa wimbo mwingine, You are The Best ulioandikwa na Tommy Flavour. Ilimchukua saa nne kukamilisha kurekodi wimbo huo tofauti na awali alipokuwa akitumia saa mbili au zaidi kulingana na hali ya siku hiyo.

“Mimi naweza kuandika lakini wakati mwingine najaribu ladha kutoka kwa watu wengine, ndio maana nimeuchagua wimbo huu ingawa vionjo nimeongeza kama lile ‘Spanish guiter’ linalosikika kwenye wimbo,” anasema. Kuhusu video ya wimbo kufanyika nje ya nje, anasema ilikuwa kama ajali tu kwani alikwenda Muscat, Oman kwa mapumziko baada ya kuwa hospitalini mwishoni mwa mwaka jana.

“Uongozi wangu ulitaka niende kupumzika kwa sababu Alikiba alikuwa na shoo kule. Seven aliniambia nikibaki peke yangu ninaweza kuendelea kuchoka tu. Kwa sababu ya mandhari mazuri ya kule tukaona sio vibaya tukirekodi kabisa video,” anasema.

Ommy Dimpoz ambaye jina lake halisi ni Omary Nyembo anasema huu mwaka wake na nyimbo zake zitakuwa zikipishana tu katika mtandao wa Youtube.

Kama mama yake angekuwepo!

Kitu ambacho hawakifahamu kumhusu anasema ni kwamba amekulia katika dhiki lakini imemjenga kuwa Ommy Dimpoz.

“Kwanza kitu ambacho watu hawajui ni kwamba mama yangu alifariki nikiwa darasa la tatu, nimeishi maisha yake ada unafuata kwa mama mdogo, mara mjomba. Yaani ile unasomeshwa na familia nzima maana kila mtu amechangia,” anasema.

“Watu wakiniona kwenye ndege au navaa vizuri wanaona huyu mtu anakula raha. Mimi nimeishi Buguruni kwa Mnyamani, Vingunguti, Mwananyamala na maeneo mengi ya Uswahilini. Yaani nakumbuka marehemu mama yangu nikimwambia nina hamu ya kuku anakwenda kununua miguu. Hakuwa na uwezo wa kununua kuku.”

Anasema maisha yake sasa siyo ya kuigiza kwa sababu amepiga hatua fulani katika maisha hivyo si sahihi kuendelea kujionyesha kama mtu mwenye dhiki.

“Kitu kingine ninachopenda watu wajue ni kwamba sivai mavazi ya gharama sana. Mungu amenijalia uwezo wa kujua vitu vizuri. Linaweza kuwa shati la buku tano au raba ya buku 10. Nikiiona tu najua hii itanipendeza sasa watu wanajua natumia gharama sana kwenye mavazi,” anasema.

Miongoni mwa mambo anayojinasibu kuyajua vyema ni kudai punguzo: “Mimi naweza kununua raba kwa watu wale wanaotembeza na nitamlilia aniuzie kwa bei halali maana si unajua wengine wakiona Ommy wanataka kukupiga.”

Vipi kuhusu ndoa....mpenzi

Anasema sio kila msanii huulizwa kuhusu mpenzi wake isipokuwa baadhi ambao mashabiki wamejiwekea ulazima wa kujua maisha yao binafsi.

“Najua kuna baadhi ya wasanii hawaulizwi kabisa kuhusu wapenzi wao, hata hivyo napenda mjue kuwa mimi pia ni kati ya wale wanaopenda kufanya siri kuhusu maisha yao binafsi,” amesema.

“Alikiba, AY, FA nimewakuta mastaa lakini wamekuja kuoa juzi, mimi ni nani mpaka nijifanye naoa sasa? alisema kwa utani.

Amesema anaamini ndoa inapangwa na Mungu na suala la kuweka wazi kuhusu wapenzi wake halina umuhimu kwake kwa sababu anajifunza kutoka kwa wasanii waliomtangulia.

“Yaani hata Ali (Alikiba) wakati anataka kuoa aliniambia tu kimasihara. Nilimwambia acha masihara hebu tuendelee kucheza drafti. Lakini kumbe hakuwa akitania mara ghafla jamaa katangaza ndoa kweli,” anasema.Pia, anasema kumtangaza mpenzi wake haoni kama ni jambo la busara na halina faida yoyote kwake isipokuwa mpaka pale atakopooa.



Chanzo: mwananchi.co.tz