Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyuma ya pazia nguvu ya wasanii TikTok

Nyuma TikTok Nyuma ya pazia nguvu ya wasanii TikTok

Sun, 4 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Data kutoka Kepios zinaonyesha kuna watumiaji wa mitandao ya kijamii bilioni 4.70 duniani hadi kufikia Julai 2022, idadi hiyo ni sawa na asilimia 59.0 ya watu wote ulimwenguni. Idadi ya watumiaji imeongezeka zaidi kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita ambapo watu milioni 227 walijiunga katika mitandao hiyo.

Hiyo ni sawa na ukuaji wa kila mwaka wa asilimia 5.1, kwa wastani wa zaidi ya watumiaji saba wapya kila sekunde moja, takwimu za Global Digital zinamebainisha kati ya watumiaji 10 wa intaneti tisa wapo katika mitandao ya kijamii.

Kwa siku duniani kote watu hutumia saa bilioni 10 kwenye mitandao ya kijamii ambazo ni takribani miaka milioni 1.2 ya kuishi binadamu, hivyo kwa ujumla watu hutumia takriban asilimia 15 ya maisha yao mitandaoni.

Mtandao wa TikTok umekuwa na ushawishi mkubwa sana kwa wasanii duniani kote, hiyo ni baada ya kutoa fursa kwa wasanii na mashabiki kufanya challenge ya promosheni ya nyimbo zao.

Mtandao huu ulianzishwa Septemba 2016 na unamilikiwa na kampuni ya China, ByteDance. Morning Consult iliitaja TikTok kama chapa (brand) ya tatu inayokua kwa kasi zaidi dunia mwaka 2020 baada ya Zoom na Peacock, huku Cloudflare ikitaja TikTok kama tovuti maarufu zaidi ya 2021 ikiwa imeipita Google.

TikTok inatoa fursa kwa watumiaji wake kuweka video fupi za muziki, dansi, vichekesho na nyinginezo zenye urefu wa sekundi 15 hadi dakika moja, ingawa kuna baadhi ya watumiaji wanaweza kuweka video zenye urefu wa dakika tatu.

Akizungumza na gazeti hili, Mtaalamu wa mitandao ya kijamii, MxCarter ambaye pia mwanzilishi wa Slide Digital, kampuni ya usambazaji muziki, anasema TikTok imekuwa na nguvu kwa wasanii hasa pale walipoanza kuwalipa wazalishaji maudhui (content creator) wanapofanya challenge kupitia nyimbo za wasanii.

“TikTok wanalipa kwa zile nyimbo zinazotumika, inapoonyesha huu wimbo kaimba msanii fulani analipwa, lakini ni lazima apitie kwenye ‘digital distribution campany’ ambazo zinaweza kukusanya fedha kwa niaba yake, ukiimba ukaweka tu si rahisi kulipwa kwa sababu wanafanya kazi na kampuni za kidijitali siyo msanii mmoja mmoja,” anasema.

“Nao hao TikTok kwa sababu wana watumiaji katika jukwaa lao ambalo linatumia maudhui yao kuvutia matangazo, basi kuna asilimia wanaitoa kwa kumlipa mzalisha maudhui,” anasema Mx Carter. Anasema TikTok imepata umaarufu mkubwa kwa sababu ilikuja na utofauti wa kutengeneza video na challenge, umaarufu wake ulizidi kipindi cha Uviko-19 kwa sababu watu walikuwa majumbani, hivyo wengi walianza kuitumia TikTok kujiburudisha.

“Na baada ya hapo ndipo ikapata umaarufu kwamba unaweza kuitumia kufanya promosheni ya wimbo wako, na wao ni moja ya mitandao ambayo inalipa vizuri na walikuja na wazo la kuwalipa wazalisha maudhui ili kuvutia wengi kuitumia,” anasema.

Kwa mujibu wa kampuni ya utafiti ya simu za mkononi, Sensor Tower, TikTok imepakuliwa zaidi ya mara milioni 130 nchini Marekani, kwa ujumla imepakuliwa mara bilioni 2 duniani kote na idadi hiyo haijajumlisha watumiaji wa Android nchini China.

Je, umaarufu wa TikTok unaweza kupungumza ushawishi wa YouTube kwa wasanii ambao wamekuwa wakitumia mtandao huo kwa miaka mingi? MxCarter anasema hapana, kwani TikTok na YouTube ni majukwaa mawili tofauti kabisa.

“YouTube itaendelea kubaki pale kwa sababu wasanii wanaitumia kwa kuweka video zao, TikTok inatumika kwa kufanya wimbo wako kuwa maarufu halafu mtu ataenda kuangalia video YouTube, sidhani kama inaweza kupunguza umaarufu wa YouTube,” anasema MxCarter.

Anasema YouTube nao wamezindua kitu kama TikTok ambacho kinaitwa ‘YouTube Short’, na huo ni ushindani ili kuweza kuwabakisha watu wake na sasa hivi inafanya vizuri, Instagram nao wameleta ‘Reel’, lengo ni kukabiliana na TikTok.

Hadi sasa TikTok inazitambua lugha 40 duniani kote, programu (App) hii pendwa ambayo inashika kasi duniani kwa sasa inafanya kazi kwenye vifaa vyenye mfumo wa iOS na Android, inachukua ukubwa wa Megabyte (MB) 55 hadi 60 inapopakuliwa kwenye simu.

Kwa upande wake mtangazaji wa kipindi cha 5Select cha EATV, T Bway anasema yeye ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakiwashawishi wasanii kujiunga TikTok kwa sababu imekuwa na nafasi kubwa ya kufanya promosheni ya muziki. “Mtandao huu unasaidia redio na TV kujua ni nyimbo gani zinafanya vizuri, kwa mfano kuna nyimbo ambazo hazijaenda “mainstream” lakini DJ na watangazaji wanazitoa kule TikTok na kuzileta mainstream,” anasema.

“Unakuta wimbo umetumika sana kwenye TikTok za watu wengi na kuwa maarufu, DJ unautafuta na kuja kuupiga kwenye redio au shughuli mbalimbali na watu wanaupokea vizuri kwa sababu wameshausikia TikTok,” anasema T Bway.

Ikumbukwe TikTok nchini China inatambulika kama ‘Douyin’, ikiwa na watumiaji milioni 600 kwa siku, muundo huu (Douyin) unapatikana China pekee na inaendeshwa kwenye seva tofauti ili kuendana na sera za nchi hiyo katika matumizi ya mitandao, lakini zote zinamilikiwa na Byte Dance.

Micky Singer ni mwimbaji wa Bongofleva ambaye wimbo wake ‘Wanijue’ ndio umempatia umaarufu ukianzia kwenye mtandao wa TikTok hadi kumfikia Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale ‘Babu Tale’ ambaye kupitia Instagram alieleza kuukubali sana wimbo huo.

Micky anasema TikTok ina mchango mkubwa katika muziki wake kwa sababu ndio chanzo cha watu wengi kumfahamu na tangu mwanzo aliona fursa katika mtandao huo.

Ikumbukwe hadi kufikia robo ya mwisho ya mwaka 2021, watumiaji wa TikTok kwa mwezi ni bilioni 1.2 na inatarajiwa hadi mwishoni mwa 2022 watafikia bilioni 1.5.

“Niliona TikTok ina wafuatiliaji wengi sana duniani, hivyo video yako inaangaliwa kwa haraka, kwa hiyo nikaona ni njia rahisi ya kufanya kitu changu kikaenda mbali. Mapokeo ni makubwa kwa sababu mimi ni miongoni mwa wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa, nimekuwa na nafasi nzuri katika muziki,” anasema Micky.

Kwa mujibu wa TikTok Report, mtandao huo kwa mwaka 2021 ulitengeneza mapato ya Dola 4.6 bilioni, wastani wa Sh10.7 trilioni, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 142 kwa mwaka huo.

Nchi zenye watumiaji wengi wa TikTok duniani ni Marekani wakiwa milioni 140.6, Indonesia milioni 106.9, Brazil milioni 74.0, Urusi milioni 56.3, Mexico milioni 51.3, Vietnam milioni 49.6 , Ufilipino milioni 42.7, Thailand milioni 39.5, Uturuki milioni 30.8 na Saudi Arabia ina watumiaji milioni 25.2.

Tanzania wasanii wa Bongofleva ndio wenye idadi kubwa ya wafuasi TikTok, anayeongoza ni Diamond Platnumz akiwa nao milioni 1.7, akifuatiwa na Zuchu mwenye wafuatiliaji 839,600, Vanessa Mdee anao 564,400, Nandy 526,400 na Hamisa Mobetto 402,800.

Kijana kutokea nchini Senegal, Khabane Lame ndiye anaongoza kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa TikTok, wakiwa zaidi ya milioni 148.4 na likes milioni 23,645. Huyu amempiku binti wa miaka 17 kutoka Marekani, Charli D’Amelio ambaye ni dansa, mwenye wafuasi milioni 145.3 na likes milioni 11,071.8.

Chanzo: Mwananchi