Waimbaji wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Zuchu na Mbosso ndio wasaniii wa muziki pekee Tanzania waliochomoza katika orodha ya vijana 100 barani Afrika waliokuwa na ushawishi kwa mwaka 2022.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Avance Media iliyotoka wiki hii ambayo imeangazia vijana 100 Afrika kutoka nchi 25 tofauti katika sekta mbalimbali kama burudani, biashara na uongozi.
Ikumbukwe wawili hao ndio wasanii wa mwishoni kusainiwa WCB Wasafi, Mbosso akichukuliwa Januari 2018, Zuchu Aprili 2020 na tangu hapo hakuna mwingine aliyesainiwa katika lebo hiyo yenye wasanii watano kwa sasa.
Hata hivyo, majina makubwa katika muziki wa Bongofleva kama Diamond Platnumz, Alikiba, Rayvanny na Harmonize hajaonekana katika ripoti hiyo.
Nchi ya Nigeria ndio imetoa vijana wengi wenye ushawishi Afrika wakiwa 31, inafuatia Kenya 11, Ghana 10, Tanzania saba, Afrika Kusini watano, huku wanawake wakiwa ni 43 na wanaume 57.
Miongoni mwa waimbaji wa Nigeria waliotajwa ni Wizkid, Burna Boy, Tems, Davido, Kizz Daniel, Fireboy DML, Asake, Ckay, Omah Lay, Mr. Eazi na Rema.
Kwa ujumla Watanzania saba waliotajwa katika ripoti hiyo ni Zuchu, Mbosso, Kili Paul, Jokate Mwegelo, Millard Ayo, Benjamin Fernandes na Barbara Gonzalez.
Kando na ripoti hiyo, mwaka 2022 kuna maeneo Zuchu alifanya vizuri kuliko Diamond, mfano alishinda tuzo ya Afimma kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki akiwabwaga Nandy, Maua Sama, Femi One, Sanaipe Tande, Jovial, Sheebah Karungi na Winnie Nwagi.
Diamond ambaye aliwania kipengele kama hicho, Msanii Bora wa Kiume Afrika Mashariki alizidiwa na Rayvanny aliyeibuka mshindi baada ya kuwazidi wasanii wengine kama Otile Brown, Meddy, Eddy Kenzo, Sat B, John Frog na Khaligraph Jones.
Vilevile Zuchu alikuwa ndiye msanii pekee Afrika Mashariki aliyechaguliwa kutumbuiza katika tuzo hizo zilizotolewa Novemba 19, 2022 huku Dallas, Texas nchini Marekani.
Wakati Zuchu akichaguliwa kuwania tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV EMA) 2022, Diamond hakupata nafasi hiyo, hivyo Zuchu ndiye alikuwa msanii pekee Tanzania aliwania tuzo hizo kwa mwaka huo.
Licha ya kutoa EP yake, First of All (FOA) Machi 11, 2022, Diamond hakuwa na mwaka mzuri ukilinganisha na miaka iliyopita, nyimbo zake nyingi zilizidiwa kimauzo baadhi ya maeneo na wasanii waliokuja miaka ya hivi karibuni kama Jay Melody na Mavokali.
Wimbo wa Jay Melody ‘Nakupenda’ uliotoka Julai 20, 2022 ndio wimbo wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi Boomplay 2022 na hadi sasa ukiwa na ‘streams’ milioni 55.6, tangu Diamond ameanza muziki, hakuna wimbo wake uliofikia rekodi hiyo ya mauzo katika mtandao huo.
Huu ni wimbo uliotoka zaidi ya miezi mitatu tangu Diamond aachie EP yake, FOA yenye nyimbo 10 ambayo hadi sasa ina ‘streams’ milioni 91 Boomplay sawa na wastani wa ‘streams’ milioni 9.1 kwa kila wimbo, idadi ambayo ni zaidi ya mara sita na ‘streams’ za wimbo wa Jay Melody, Nakupenda.
Mavokali ambaye anatajwa kusainiwa WCB Wasafi, wimbo wake ‘Commando’ ndio uliongoza upande wa Bongofleva kusikilizwa zaidi Spotify 2022 ukiwa na ‘streams’ milioni 4.9, ukifuatiwa na Mi Amor wa Marioo ‘streams’ milioni 3.6, Diamond alidondokea nafasi ya tatu na wimbo wake, Melody ‘streams’ milioni 3.5.
Mwaka uliopita, Diamond hakuchaguliwa kuwania tuzo za BET kama ilivyokuwa 2021, huku msanii wa Uganda, Eddy Kenzo akiwa ndiye mwimbaji pekee Afrika Mashariki aliyechaguliwa kuwania tuzo za Grammy ambazo Diamond hajawahi kuwania.
Licha ya kuendelea kuongoza Kusini mwa Jangwa la Sahara kama msanii aliyetazamwa zaidi YouTube kwa muda wote akiwa na ‘views’ zaidi bilioni 2, bado namba zinamkataa Diamond ukitazama kwa wimbo mmoja mmoja kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Mfano mwaka jana video ya wimbo wa Rema ‘Calm Down’ ndio iliongoza ukanda huo ikiwa na ‘views’ zaidi milioni 300, wakati video ya Diamond iliyofanya vizuri zaidi YouTube 2022 ni ya wimbo ‘Mtasubiri’ akimshirisha Zuchu iliyomaliza mwaka na ‘views’ milioni 24.
Kwa ujumla hakuingiza hata video moja kwenye 10 bora, video nyingine zilizofanya vizuri ni; Calm Down Remix ya Rema (mil. 190), Last Last ya Burna Boy (mil. 140), Buga ya Kizz Daniel (mil. 108) na For My Hand ya Burna Boy (mil. 70).
Pengine Diamond mwenyewe anajua hakufanya vizuri sana mwaka 2022, kwa mujibu wa ujumbe wake wa Januari 21, 2023 alipotangaza kuwa mwaka huu atafanya mambo makubwa katika muziki kama ndio ametoka leo kimuziki na kuwahakishia mashabiki wake watafurahi.
“Mawe ya Kibongofleva, Kiafrika na Dunia. Nyimbo za mapenzi, maisha, maumivu na starehe. Video za ndani, Afrika na Dunia. Ni mwaka wa tasnia na Taifa kujivunia kuwa na kiumbe kinaichoitwa Nasibu Abdul, Diamond Platunumz, Simba,” alisema Diamond.
Tangu wakati huo Diamond ameweza kuachia nyimbo mbili, Yatapita na Zuwena ambazo zimepokea sifa lukuki kuwa ndio ile Bongofleva halisi iliyomtoa Diamond kupitia nyimbo kama Mbagala na Kamwambie. Video za nyimbo hizi mpya nazo zimesifika na wengi wa ubunifu mzuri uliobeba uhalisia wa kile alichoimba.