Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nitasikitika sana kufa na kumbukumbu nyingi sandukuni

73651 Anko+kitime

Sat, 31 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sina maelezo kwa nini nilianza tabia ya kukusanya picha na hadithi za wanamuziki toka nikiwa na umri mdogo, nilijikuta tu nikihakikisha nakusanya picha za magazetini na picha kamili kwa miaka mingi. Baadaye nikaanza kukusanya pia santuri na kanda za muziki, huwa mwenyewe nashangaa hazina niliyoweza kukusanya kwani nina hata muziki wa askari Kea, hivyo ndivyo walivyojulikana askari wa jeshi la Mwingereza kirefu chake kilikuwa ni Kings African Rifles (KAR), katika kanda niliyonayo, askari hawa wanaimba nyimbo za furaha mara tu baada ya vita ya pili ya dunia mwaka 1945!!

Picha na hadithi nilizoweza kukusanya miaka ya 60 na 70 sasa ni mali muhimu, si kwangu tu bali kwa wapenzi wa muziki wa zamani na pia ni kumbukumbu muhimu za historia ya muziki wa Taifa letu.

Mwaka 2009 nilianzisha blog yangu ya kwanza ili kuziweka kumbukumbu hizi hadharani, nikaanzisha blog iliyokuwa na anwani www. mwakitime.blogspot.com, ilipokewa vizuri na nikaanza kusaidiwa na watu wengi kwa picha na kumbukumbu nyingine kuiboresha, kikawa kijiwe cha wapenzi wa muziki wa zamani, hatimaye niliiboresha na kuipa anwani ya www.tanzaniarhumba.blogspot.com. Watu wengi walikuwa wakiipitia blog hii kupata burudani na hata wasomi wa hapa nchini na nje ya nchi kuitumia hata kwa utafiti. Pamoja na kuwasiliana kwa ukaribu na wapenzi wa muziki wa zamani kutoka hapa nchini, nimeweza kupata mawasiliano ya karibu ya wadau wa muziki wa zamani kutoka nchi mbalimbali, kama vile Uingereza, Ujerumani, Kenya, Afrika ya Kusini, Marekani na Brazil. Wasanii wengi wa zamani nawafahamu sasa na wao wananifahamu, na hata wengine wameweza kunitumia ili kupata haki zao. Mfano wanamuziki wa Atomic Jazz Band wamepata bahati ya kulipwa fedha mara mbili na nikatoa msaada kutokana na kuelewa zaidi kuhusu nyimbo zao. Mara ya kwanza walipata fedha kutoka kampuni moja ya filamu toka Norway, iliyotaka kutumia sehemu ya wimbo wao waliorekodi Mombasa miaka zaidi ya 40 iliyopita. Na mara ya pili walilipwa baada ya kusikia msanii mmoja amerekodi wimbo wao, na kuniomba nifuatilie haki zao hapo. Juzi juzi kampuni moja ilinitafuta kusaidia kuwatafuta baadhi ya wanamuziki wa Western Jazz Band kwani walikuwa na nia ya kutumia mmoja ya wimbo wao, ilikuwa rahisi kuwapata kutokana na kuwa na kumbukumbu za kuweza kuwatafuta, mtunzi haswa wa wimbo unaotakiwa kwa sasa anafanya shughuli za uganga wa asili huko Kigoma. Lakini jambo ambalo limenipa faraja kubwa mwezi huu ni barua pepe niliyoandikiwa kutoka huko Denmark. Barua hiyo ilitoka kwa mtu aliyesema amepewa jina langu na watu wawili mmoja kutoka Ujerumani na mwingine kutoka Marekani, ambao wamemshauri atume mzigo mmoja muhimu sana kwangu. Mzigo huo ni barua, picha na nyimbo zaidi ya 80 ambazo bwana huyo alikabidhiwa na marehemu Otto Larsen, aliyefariki mwaka 1989. Huyu Otto Larsen ni Mdenishi aliyeendesha kiwanda cha kwanza cha kutengeneza santuri Afrika ya Mashariki. Kiwanda hiki kilikuwa na ‘label’ kubwa mbili, East African Records Limited na Jambo Records.

Wanamuziki wengi waliotamba na kazi nyingi za wanamuziki zilizotamba Afrika ya Mashariki kuanzia miaka ya 50 mpaka miaka ya 70, zilitokana na kazi nzuri iliyoanzishwa label hizi mbili za Mzee Otto. Katika makabrasha haya kuna barua za mikataba ya kazi ya wanamuziki maarufu kama Fadhili Williams na Fundi Konde, kukiwa na sahihi zao wakikubali kuwa waajiriwa wa Jambo Records na masharti waliyopewa. Pia kuna nakala za matangazo ya shughuli za burudani wakati huo, mchekeshaji aliyeitwa Kipanga anaonekana alikuwa mmoja wa ‘Masupastaa’ katika maonyesho ya burudani enzi hizo. Katika makabrasha niliyopokea ndio nimekuja kugundua kuwa waimbaji wa wimbo uliokuwa maarufu sana ulioitwa Mwalimu Shekinuru, kumbe walikuwa Watanzania. Bi Eddah ambaye makabrasha yanasema ni Msukuma na Harry Makacha ambaye anaelezwa alikuwa Mmakuwa, walikuwa wanandoa na wanamuziki maarufu miaka hiyo na nyimbo zao zilirekodiwa na kusambazwa na Jambo Records.

Kitendawili cha nani aliyetunga wimbo wa Malaika kimenirudia tena baada ya kukuta nyimbo mbili tofauti zilizorekodiwa zama hizo, kila moja ikiwa na baadhi tu ya maneno yaliyomo katika wimbo wa Malaika, lakini zikiwa na melodia ile ile.

Si rahisi kuandika kuhusu yote niliyonayo, ingekuwa enzi ile ningeweka picha na taarifa nilizonazo kwenye blog yangu, bahati mbaya sheria za TCRA zinanilazimu kulipia Sh1.1 milioni ili kupata ruhusa ya kutumia blog yangu. Kukiuka hilo najiweka katika hatari ya kulipa faini ya mamilioni ya shilingi. Kwa sasa nitaendelea kutumia njia hii ya kuandika makala hizi kuelezea machache kati ya nitakayoyakuta kwenye hayo makabrasha ya marehemu Mzee Otto Larsen.

Pia Soma

Advertisement   ?

Chanzo: mwananchi.co.tz