Kwanza kabisa, siku hii ambayo husherehewa kila Ijumaa ya kwanza ya Agosti, ilianza 2007 huko Santa Cruz, California, Marekani na marafiki wanne ambao ni Jesse Avshalomov, Evan Hamilton, Aaron Araki, na Richard Hernandez.
Lengo lao lilikuwa kuwepo na siku ya kimataifa ya bia ambapo mambo matatu yatafanyika.
Mosi, kuwepo na mkusanyiko wa marafiki kufurahia ladha ya bia, pili kusherehekea wale wanaohusika na usindikaji, tatu kuwapongeza wale wote kwa namna moja ama nyingine ni wahudumu wa kinywaji hicho.
Tangu kuanzishwa kwake, kutoka tukio dogo la majaribio lililofanywa na marafiki hao huko magharibi mwa Marekani, sasa limekuwa ni sherehe ya kimataifa inayohusisha miji 207, nchi 80 na mabara sita ambapo ulimwengu unaunganishwa kwa kusherehekea pombe za mataifa yote, kwa siku moja.
Washiriki wanahimizwa kupeana 'zawadi ya bia' kwa kununuliana, kisha kutoa shukrani za dhati kwa watengenezaji wa kinywaji hicho, wahudumu wa baa, na mafundi au wataalam wengine wa bia.
Katika mwelekeo wa kimataifa wa sikukuu hiyo, inapendekezwa pia kuwa washiriki watoke nje ya eneo lao la starehe na kujaribu bia kutoka utamaduni mwingine.