Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imezindua bodi mbili za Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB), huku ikizitaka kuhakikisha uchumi wa sekta hizo unapanda.
Pia, imezitaka bodi hizo kutatua migogoro iliyoko kwenye vyama na mashirikisho kwenye utamaduni na sanaa iishe na kuzungumza lugha moja ya maendeleo.
Waziri wa wizara hiyo, Damas Ndumbaro alisema jana kuwa migogoro mingi kwenye maeneo ya sanaa, utamaduni na michezo yanasababishwa na maslahi. Katika uzinduzi huo, uliokwenda pamoja na kumtambulisha Balozi wa Cosota, mwanamuziki, Barnaba, Waziri Ndumbaro alizitaka bodi hizo kuwajibika ipasavyo ikiwamo kudhibiti uharamia wa kazi za wasanii ili wanufaike na jasho lao.
Ndumbaro aliwapongeza wenyeviti wa Bodi ya Cosota, Victor Tesha na ya filamu, Dk Mona Mwakalinga na wajumbe wote akisema kazi yao kubwa ni kuhakikisha tasnia wanayosimamia inakuwa ni uchumi kwa nchi, kwa wadau na kwa Watanzania.
Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA alisema wana matarajio makubwa na bodi hizo ambazo wasanii Jacob Steven ‘JB na Mike Mwakatundu ‘Mike T’ ni miongoni mwa wajumbe na kuzisisitiza kutimiza majukumu kwa utiifu na kuleta matokeo makubwa zaidi ya waliyoyakuta.