Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndoa ya muziki na siasa sasa ndio basi tena

9359 Anko+kitime TZW

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukifuatilia historia ya nchi hii hata kabla ya ujio wa wakoloni, wanamuziki wamekuwa na nafasi muhimu katika siasa za jamii yetu. Kiwango cha mchango huo na sababu za mchango zimekuwa zikibadilika katika nyakati tofauti.

Kabla ya ujio wa wakoloni, kulikuwepo na wasanii - wanamuziki katika makabila mengi ambao walikuwa wakiimba na kupiga vyombo vya muziki na kuwa na ukaribu sana na viongozi nyakati hizo. Wanamuziki hawa walikuwa ni sauti za wananchi zilizomtaarifu mkuu wa jamii, furaha na masikitiko ya wananchi wake.

Na alikuwa akifanya hivyo kwa uhuru bila kuogopa adhabu toka kwa kiongozi wake. Wasanii hawa mara nyingi walifadhiliwa na wakuu wa jamii na hivyo kuwa na nafasi muhimu katika jamii.

Ujio wa wakoloni ulieneza utamaduni wa kuanzishwa kwa miji. Miji ilikusanya watu kutoka makabila mbalimbali, watu hawa waliungana kwa vile mbaya wao sasa alikuwa mkoloni.

Simulizi zinatuambia kuwa Wajerumani walipenda sana kutumia viboko kuwaamrisha wazawa, tabia hii na tabia nyingine zilizowadhalilisha na kuwanyima uhuru wazawa zilisababisha wananchi kuanza kutafuta njia za kuilalamikia.

Wanamuziki wakaanza kufanya kazi hii. Wanamuziki walikuja na muziki ulioitwa Beni Ngoma. Muziki huu kwanza uliwaunganisha watu kutoka makabila mbalimbali na ulitumika kwa kuimba mengi yakiwemo maovu ya mkoloni. Hata uchezaji wa ngoma yenyewe ilikuwa ni kejeli kwa taratibu za jeshi la Ujerumani.

Ngoma hii ilisambaa sehemu kubwa ya Afrika Mashariki. Na hata leo baadhi ya ngoma kama Mganda na Malipenenga ni kati ya zile ambazo ni mwendelezo wa Beni Ngoma.

Waingereza walipoiondoa Ujerumani walikuta wanamuziki wa Beni Ngoma wakiwa na nguvu na umoja hata kuweza kufanya mashindano kati ya mji mmoja na mwingine. Muda si mrefu wakoloni waliishtukia ngoma hii kwa kuona kuwa ilikuwa inawaunganisha wananchi na wanaitumia kupashana taarifa kuhusu namna ya kumpinga mkoloni.

Waingereza waliupiga marufuku muziki huu. Na hata sheria ya kuanza kuomba vibali kwa ajili ya maonyesho ya muziki ilianza wakati huo. Bahati mbaya sheria hiyo ipo mpaka leo miaka zaidi ya 50 baada ya Uhuru.

Wakati zilipopamba harakati za kupigania Uhuru miaka ya 1950, muziki ulitumika sana. Nchi nzima kulikuwa na wanamuziki wakitunga nyimbo kwa kutumia ngoma za asili na muziki wa dansi na taarab nyimbo zilitungwa kuhamasisha watu kuungana kudai Uhuru.

Mwanamuziki Frank Humplick ambaye baba yake alikuwa Mzungu kutoka Austria na mama yake Mchaga alijulikana zaidi kama kijana wa Kichaga na aliwahi kutunga wimbo ulioitwa I am a democrat. Wimbo huu ulikuwa ukielezea kishairi mambo yatakavyokuwa Uhuru ukipatikana, ulimchukiza sana mkoloni. Amri ilitolewa na santuri za wimbo huo zilisakwa na askari nyumba kwa nyumba na kuvunjwa. Wimbo huo ulikuwa mmoja wa nyimbo zilizotumika kabla ya mikutano aliyokuwa akihutubia Mwalimu Nyerere wakati huo. Katika mikoa ya Kusini, wanamuziki kama Moses Nnauye walianzisha vikundi vya muziki kuhamasisha kudai Uhuru na ujumbe uliwafikia vizuri wananchi wengi. Desemba 9, 1961 bendi na vikundi vingi vilitunga nyimbo zilizoongelea furaha ya kupata Uhuru na na ndoto za wananchi baada ya Uhuru. Kaulimbiu wakati huo ilikuwa ni Uhuru na Kazi. Uhusiano wa muziki na siasa uliongezeka baada ya Tanzania kuamua kuwa nchi ya kijamaa. Serikali iliwekeza katika sanaa.

Kulikuwepo na maoafisa utamaduni wa wilaya na mikoa kila mkoa na bajeti yao ilitoka Serikali Kuu. Maafisa utamaduni walihamasisha kuanzishwa vikundi vya muziki wa aina mbalimbali mpaka vijijini.

Mashirika ya umma yalihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa na ndipo kukawepo kundi la sanaa la Taifa, vikundi vya sanaa majeshini ambapo huko pia kukawa na vikundi vya taarab na dansi. Mashirika kama Bima, DDC, Urafiki na mengine mengi yakawa na vikundi vya sanaa. Kurugenzi za mikoa kama Dodoma na Arusha nazo zikaanzisha vikundi, bila kusahau Women Jazz Band na baadaye Umoja wa Vijana wa Tanu nao ukawa na bendi yake maarufu ya Vijana Jazz.

Vikundi vyote hivyo vilishiriki katika kuimba nyimbo mbalimbali za siasa na maendeleo. Pamoja na bendi na vikundi vya taarabu, wasanii maarufu walikuja kupatikana akina Makongoro, Mwinamila, John Komba na kadhalika. Zama hizi ziko tofauti sana, Serikali inaonekana kama haioni umuhimu wa sanaa katika kuhamasisha uzalendo. Bajeti ya sekta hiyo ni ndogo, wizara inayohusika na utamaduni haina tena maofisa mkoani wala wilayani. Waliopo wako Tamisemi ambako nako hawapewi umuhimu sana. Hata Bendi yaVijana wa CCM nayo iko hoi bin taaban.

Vyama vingine vya siasa navyo ni wazi havioni umuhimu wa vikundi vya sanaa katika kueneza sera zao, hivyo ndoa ya miaka mingi ya muziki na siasa ni kama imekufa.

Chanzo: mwananchi.co.tz