Dar es Salaam. Hatimaye ndoa ya msanii Rose Alphone maarufu Munalove na mumewe Peter Komu imevunjika rasmi ikiwa ni baada ya miaka 10 tangu uwepo wake.
Hilo limeelezwa na watalaka hao leo Jumanne Oktoba 15, 2019 walipozungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, kuhusiana na hatma ya mgogoro wao wa ndoa ulioibuka kipindi cha kifo cha mtoto wao Patrick Januari 2019.
Katika mgogoro huo kulitokea tafrani ikiwemo nani mwenye haki ya kuzika mpaka kufika hatua ya msiba kuwekwa sehemu mbili tofauti japokuwa mwisho wa siku Peter alipewa haki ya kumzika mtoto wake.
Akizungumzia mgogoro wa ndoa hiyo, Muna amesema tayari wameyamaliza kwa kuachana rasmi mahakamani, hukumu iliyotolewa na Mahakama ya mwanzo Magomeni Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2019, ambayo nakala yake Mwananchi imeiona.
Akizungumzia hatua hiyo, Muna amesema “nashukuru nimepata haki yangu niliyoisotea kwa muda mrefu kwani mbali na talaka pia imeamuliwa nyumba aliyokuwa akiishi Komu iuzwe na hela itakayopatikana tugawane nusu kwa nusu.”
Alipoulizwa kwa nini hakupewa talaka muda wote tangu walipoachana, Muna amesema mume wake huyo alimpa masharti kwamba ili amuache akubali kumwachia nyumba jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya na ndio maana wamefikia hatua ya kupelekana hadi mahakamani.
Pia Soma
- Rais Zuma kukata rufaa dhidi ya kesi yake ya ufisadi
- Profesa Ndalichato atoa maagizo kwa katibu mkuu wizara ya elimu
- Upepo wajeruhi wawili, nyumba 49 na makanisa yaezuliwa Butiama
- Tasupa watoa masharti ununuzi wa alizeti Tanzania
”Ndoa yangu imefungwa kanisani na sio mahakamani, hivyo kama ningekuwa na nia ovu ya kukataa isivunjwe ningesimamia msimamo wangu lakini nimeona haina haja.”
“Muna ameamua tu kuongea kujifurahisha kwani hajachangia hata tofali katika ujenzi wake na hata hati aliyokuonyesha ni ya kughushi lakini kwa kuwa alikuwa ni mke wangu halali bado ana haki nayo, ”amesema Komu.
Amesema tayari nyumba hiyo ipo katika hatua ya kuthaminishwa ili ijulikane kila mtu atapata nini ikipigwa mnada.