Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndassa alikuwa kiungo katika muziki wa dansi

AFRICAN.png Ndassa alikuwa kiungo katika muziki wa dansi

Fri, 1 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

NI msiba jamani! Hadi majira ya juzi saa tano asubuhi, ndizo taarifa zilizotawala nchi nzima, hususan katika ulimwengu wa mtandao. Si mwingine, bali ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa.

Ndassa huyu mbunge, hapo ni sehemu moja inayomhusu, lakini nyayo za umaarufu wake, zinagusa idara nyingine katika maisha ya kawaida.

Muda umepita na inawezekana wengi wakamfahamu katika sura ya kisiasa, ubunge, maana kutumikia robo karne si haba, waliozaliwa wakati anaanza, leo hii ndiyo vijana mitaani, kwenye ajira, mashambani, watafuta kazi na ambao vikao vyao vya harusi vinaendelea sehemu mbalimbali.

Kurudi kabla ya hapo, mathalani kwenye sekta yetu ya habari, ni mwenyeji kindakindaki akiwa na mzizi mrefu, ni meneja matangazo wa lililokuwa gazeti kubwa nchini.

Ilikuwa kawaida, ukiingia katika ofisi za gazeti la Mfanyakazi, lililomilikiwa na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania, eneo la Mnazi Mmoja, katika ghorofa ya kwanza kulia mwa kiti cha mhariri mkongwe, James Nhende ndiko alipopatikana Ndassa, wakati wote.

Tukirudi katika maisha ya kijamii, na hususan muziki wa dansi nchini, hadi umauti unamkuta, amekuwa mdau wa chanda na pete anayejulikana vyema kuanzia kwa ndugu zake wa habari, wanamuziki ndiyo usiseme, lakini zaidi ya hapo ameshawahi kubeba haiba ya mmiliki

Kwa wanaofuatilia muziki wa dansi za zamani nchini unaotawala katika redio za nchini, hususan katika siku za mwisho wa wiki, hata kwa marejeo ya wiki moja iliyopita, ni mdau mkubwa wa kupiga simu kupongeza, kuchagua vibao au 'kutumbukiza' hili na lile kwa weledi kuhusu vibao vinavyopigwa na vituo vya hapa nchini.

Kwa kurejea nyuma kabla ya kuvaa wajihi wa ubunge, zama ambazo 'Dar inachemka kama bahari' dansi limetawala kila mahali, kumkosa Ndassa mahali hapo walau siku moja, katika mazingira ya kawaida pasipo dharura yoyote, msamiati 'haiwezekani' ni wa lazima. Naam! Hiyo ndiyo haiba yake kwa muziki.

Uswahiba wake kuanzia na bendi za muziki wa dansi, pia mwanamuziki mmoja mmoja ulikuwa juu kupindukia. Itakumbukwa, mapema miaka 1990, makazi yake yaliyopo Manzese Ukombozi, jijini Dar es Salaam, yaligeuka kuwa kijiwe maarufu cha wanamuziki.

Nakumbuka vyema, baadhi ya wanamuziki, wengine kadhaa wameshatangulia mbele ya haki, kama waimbaji maarufu mapacha raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kasoloo Kyanga na Kyanga Songa, pia kaka yao ambaye anaimba na sasa yupo nchini Kenya, Skassy Kasambula, palikuwa kama nyumbani kwao.

Wakongo wengine, magwiji wapiga gitaa la solo maarufu katika bendi ya Maquiz, Nguza Vikings aliyepo nchini na mrithi wake, Vumbi Dekula Kahanga, anayeendeleza jukumu ughaibuni, daima hawakukosekana hapo Manzese Ukombozi.

Ni simulizi zinazowafikia wengi kama aliyekuwa bingwa wa kucharaza kinanda, marehemu Asia Daruweshi 'Super Mama', pia mwimbaji na mtunzi mahiri, Zahir Ally Zorro.

Ndiyo picha halisi mahali hapo palivyokuwa kijiwe kamili cha muziki wa dansi na mara zote ukiwakuta hapo, basi wanabadilishana mawazo kuhusu mwenendo na ujuzi wa dansi, hata walifanya mazoezi.

Haikushangaza kushuhudia rasmi mwaka 1994, Ndassa huyo alipoanzisha bendi yake aliyoipa jina la Ngorongoro Heroes, hata pale ilipofyatua vibao iliibua mtikisiko mikubwa ndani ya tasnia hiyo.

Sehemu kubwa ya majina yaliyoshuhudiwa kubadilishana mawazo kijiweni Manzese, Ukombozi, ndiyo safari hii walikamata vifaa vya bendi stejini wakimwaga burudani.

Hata hivyo, kama zilivyo bendi nyingine, Ngorongoro Heroes baadaye ilisambaratika, lakini Ndassa aliendelea kuhudhuria maonyesho ya muziki wa dansi kama kawaida na wanamuziki wakimtaja jina mara tu wanapomwona anaingia ukumbini, huku mwenyewe akiinua mikono juu au kupiga makofi.

Mungu ailaze roho ya Ndassa mahali pema, peponi, Amen.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live