Dar es Salaam jioni. Mida ambayo raia walioajiriwa huwa ‘bize’ kurejea kitaani. Nami ni miongoni mwao. Siku hiyo baada ya kumaliza vimeo vyangu mapema, nashuka ngazi za jengo la Dar Free Market, pale kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Najiamini mno.
Kila baada ya hatua moja nakutana na mrembo. Ni jengo lenye vinasaba na warembo wengi ukiondoa Mlimani City. Tena pale ni zaidi, kwa sababu Mlimani City kuna mwingiliano sana. Lakini pale ni vigumu kukutana na Amina Ndalafupi. Kifupi ni kiwanda cha totozi ‘klasiki’.
Mlimani unaweza kuwapima kwa viwango. Ukaona huyu wa milioni, yule wa laki, wale wote watatu elfu hamsini. Yule savanna mbili, na hao wanne wenye vijora wa chips mayai na ‘pepsi bigi’. Lakini Dar Free Market, yeyote unayemuona anakushawishi kuuza ile nyumba ya urithi ya Kijenge Juu na Pasiansi.
Ngazi si ndefu sana. Lakini hadi nafika nje ya jengo, shingo imepoteza uhalisia. Imechoka kuliko miguu na akili. Kwa ujinga wa kufuata macho yanachoona. Nilikuwa kama askari anayeongoza magari pale Buguruni Sheli. Kila kiumbe uzao wa Beyonce, niliyepishana naye alinivutia. Nikageuka kumtazama tena na tena na tena.
Kama Kamusoko dakika ya 90 anatupia goli. Nami dakika chache nikamuona mtoto mzuri. Kwa akili kubwa inayotenda kazi haraka kama yangu, tayari nikajua umri wake (23), elimu (chuo), idadi ya vidume aliotoka nao (2), kabila lake (Mbondei) na ubora wa ngozi (nyororo).
Kama upepo nikachukua namba. Tabasamu langu la kibwege, macho ya wizi, sauti tulivu yenye unyonge. Mtoto akaloa kwa sumu zangu na kunipa namba. Kitu rahisi zaidi kwa madem wa mjini ni kutoa namba kuliko kodi. Na akishatoa namba kakubali kila kitu. Usiongee zaidi.
Pia Soma
Dar Free Market hadi Morocco tayari nishajua anaitwa Lilly, kapanga Sinza, ana degree, anasubiri ajira. Hana mume, mchumba wala mpenzi. hadi hapo nikajua ndo walewale ‘maslei kwini’. Yote niliyajua kwa ‘wasapu’ tukichati. Katika jukumu lilitoweka mjini hivi sasa ni kutongoza.Zamani ilikuwa kazi kupata namba ya mrembo, leo mnakutana kwenye ‘grupu’ la ‘wasapu’. Unazama ‘bobo’ unabeba zigo kilaini. Hakuna sehemu yenye ufuska kama ‘magrupu’ ya ‘wasapu’. Wake na waume za watu wenye ndoa zao, wanabebana kama mbuzi wa shughuli. Dunia ya teknolojia inarahisisha fursa ya uzinzi.
Kwenye ‘magrupu’ unaweza kubeba wanawake hata saba wasijuane. Mkaishia kuitana ‘bebi bebi’ kama utani kumbe ndo ukweli. Kama una mke au mume, yupo kwenye ‘grupu’ zisizoeleweka, umeumia. Nieleweke, zisizoeleweka. ‘Grupu’ linaitwa ‘Don’t Touch Me’. Au ‘Lovers And Friends’. Unategemea nini?
Kabla hata sijapiga fundo la kinywaji baada ya kufika baam, zikaanza meseji kutoka kwa Lilly, niliyekutana naye jioni pale Dar Free Market. Kaanza kuniita ‘bebi’, na lawama juu, kwa nini sijibu meseji zake. Huku akiuliza niko wapi aje. Yaani muda mfupi uliopita hakunifahamu, saa chache mbele natwishwa zigo la kuitwa ‘bebi’.
Ndo maisha ya sasa yalivyo hakuna la ajabu. Mavazi ya mtoko ‘wikiendi’ ya ‘mabebez’ unakutana nayo makanisani. Totozi zinadanga popote. Wapo wanaopanda daladala au mwendokasi, kwenda mjini asubuhi bila shughuli yoyote. Vazi lake haliendani hata na kazi ya kibanda cha M Pesa. Anaenda wapi? Udangaji.
Maisha yamekuwa chochote hivi. Ukiyabeba kama yalivyo hayasumbui. Ukishindana nayo yatakuacha njiani. Kila kitu kimebadilika, wanaoolewa sasa ni totozi zenye umri mkubwa kuliko umri mdogo. Fuatilia. Mdogo atakuacha njiani. Maisha ya mjini yana mvuto kuliko kukuandalia shati na maji ya kuoga asubuhi.
Wanaotamani ndoa ni wale waliovuka miaka 28. Huwezi kukuta ‘dem’ wa miaka chini ya 28 anawaza ndoa. Ngumu sana kwa sababu maisha ya dunia huru yanamvutia zaidi ya ujinga wa kunyoosheana nguo na mume asubuhi, na kupikiana chai kidwanzi. Dunia huru inatamanisha.
Mvuto wa maisha huru kwa vijana unachangia sana kuua ndoa na uhusiano. Uhuru wa kutoka atakapo na kubeba amtakaye. Hili ni tatizo kubwa, na si suala la kipato wala umasikini. Dunia imeamua kutupeleka kwenye mvuto wa uhuru. Mademu na vidume tunahusudu ‘teki awei’ kwa kuwa haibani. Uhuru ndo tatizo.
Hebu tuwekane sawa. Mwanamke anampenda mwanaume kwa utajiri au pesa? Vipi wake wa matajiri wenye michepuko? Je mwanamke anampenda mwanaume kwa sababu ya shoo nzuri na pumzi ya 6x6? Vipi askari na wapiga ‘gym’ wanaojiua kisa wake zao kuchepuka?
Kwa sasa dem anapelekwa ukweni kutambulishwa. Siku ya kwanza kashinda akichati. Siku ya pili anachati. Tena anajisifia kwenye magrupu kuwa yupo ukweni. Mashost wa ‘grupu’ nao wanampamba. Ukweni wanamtazama, wanampima. Hawamwambii kitu. Siku ya tatu anaambiwa zamu yake kupika. Anaona kila kitu kigeni jikoni. Cha huku kaweka kule, cha kule kaweka huku. Hana anachojua kwenye upishi. Sufuria anabeba kama chupa ya savanna. Mwiko anashika kama power bank. Hataki kuchafua nywele wala kufuta lipstick. Mvuto wa maisha ya dunia huru unaua uhusiano na familia nyingi.
Mdomo kama mnyonya damu. Mikono imefunikwa na mapambo kama mnara wa simu. Kimini kama staff wa Fast Jet. Akiambiwa hafai ananuna kama kanyimwa chaja ya simu. Analalamika hapendwi na wakwe. Kumbe tatizo ni yeye. Kesho tu anaweka ‘dipii’ yake ya ‘wasapu’ maneno ya kunanga mawifi.
Ukiolewa mume atakula chips za Sele Bonge au wali wa ‘Shishi Bebi’? Au ‘utadaunlodi’ ‘apu’ inayopika chapati na ubwabwa? Unadhani ndoa ni ‘kuedit’ picha uliobinua kiguu kimoja kama umekanyaga kinyesi na ‘kupost insta’? Au unadhani ndoa ni kama kusutana kwenye ‘peji’ za Instagram?
Kuna umri fulani wanajikuta hawana mvuto tena. Hana bwana mwenye ‘fyucha’ wala dalili ya mchumba. Pale wanapoona kuna wasichana wadogo wazuri zaidi yao na ndo wanaopendwa na madanga, wanaanza kuwaza ndoa. Ndo maana wengi wanaoolewa hivi sasa umri umesogea kama basi la mwendokasi.
Kuna wakati haishangazi kuona Anti Ezekiel kashindwa kuishi na Mose Iyobo. Davina kakimbia ndoa, Uwoya kamtosa Dogo Janja. Na sasa tunaambiwa King Kiba kamtwanga talaka tatu mkewe. (Kiba amekanusha akisema matatizo ya mkewe na familia yao ni asilimia moja tu lakini yalishaisha)Dunia ya sasa inahitaji uhuru zaidi.
Dogo Janja anawezaje kuificha dhahabu kama Irene Uwoya. Katika dunia ya uhuru na kujiachia? Ni ngumu sana. Uwoya Kavuka daraja la kuhifadhiwa. Dunia huru inamhitaji naye anaihitaji zaidi kuliko mbavu za Chalii ya R. Lazima wamwagane.
Anti Ezekiel ni mtu wa kusubiri agizo la bwana mdogo Mose Iyobo? Bado dunia huru inamhusudu kuliko Iyobo. Na Iyobo pia anahitajika na dunia huru kuliko kukariri nyonga za Anti. Ilikuwa ngumu mno kuendelea ‘kushea’ joto la shukani kibwege bwege tu. Ilikuwa waachane siku nyingi.
Wiki hii fununu za kuachana kwa Kiba na mkewe zilitawala na tayari mwenyewe amezikana lakini fununu hizo zinaturudisha kwenye yale yale ya kutaka dunia huru zaidi.
Lakini kwa umri wao na nyakati hizi dunia ya uhuru inawavutia machoni, kuliko heshima ya kuitwa mke au mume wa mtu.