Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndani ya Boksi: Diamond hata akipewa Rihanna, wataachana tu

98341 Diamond+pc Ndani ya Boksi: Diamond hata akipewa Rihanna, wataachana tu

Mon, 9 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watoto wazuri. Yes wazuri kweli kweli wa kishua. Wale wa maneno mawili Kiswahili, ishirini Kiingereza. Ambao hawapajui Kariakoo wala Ubungo. Manunuzi kwao ni Ulaya. Hata wakienda kusalimia bibi zao vijijini ni ndege au ndinga binafsi. Hawa ungewakuta kule pembezoni mwa Bahari ya Hindi Slipway kila mwisho wa wiki.

Ni maisha ya mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa 2000. Vijana wote wa mjini tulipenda kwenda huko. Nyakati ambazo TID anakimbiza mjini na Zeze watoto wazuri wote wake. Wanaimba jina lake Top In Dar kweli. Toka Sinza mpaka Mikocheni la Fiesta ogopa sana. Ni kumbukumbu tamu kuliko penzi jipya kwa kijana.

Kilikuwa na warembo kwelikweli. Wale waliokuwa bado kuharibiwa na vipodozi toka China. Ukiingia disco unavutiwa na wao kuliko muziki na pombe. Unaingia na kutoka bila kucheza wala kulewa. Kitu pekee ambacho unasepa nacho mwilini ni harufu ya moshi wa sigara. Lakini huchukia maana macho yameona vingi vinono. Tukitoka hapo wenye umri mkubwa wangejichanganya Bilcanas ‘Site Senta’. Mambo Club ‘Ostabei’. Kama siyo Blue Palm Mikocheni kumuona Dj Bon Love. Lakini kuna ambao usingewaona kote huko zaidi ya kwenye dansi. Twanga Pepeta Mango Garden au Fm Academia Msasani. Mji ulifurika starehe kila kona. Achana na wale wakeshaji wa kwenye baa.

Banza Stone katika wakati wake bora kila alichoimba kiligeuka madini mjini. Nani Kama yeye? Acha! Kina Nyoshi na Wakongo wenzake walinyoosha mikono juu. Mwendo wa mateka toka kwa Msukuma aliyekulia Kariakoo na Sinza. Alikuwa maarufu kwa jina lake halisi mpaka a.k.a zake zote. Ardhi hii ya dunia imehifadhi akili nyingi sana chini aiseee.

Unaongelea WCB? Kumbuka kulikuwa na Camp tu za mashabiki wa dansi zenye nguvu kuliko bendi kibao. Home Alone wale watoto wa Kinondoni, walikuwa na maamuzi na mipango ya bendi ya Twanga kuliko Asha Baraka sikia tu kwa watu haya mambo. Unaongelea Team Kiba na Mondi wa mitandaoni? Hawa ni cha mtoto mno.

Hayo makundi yalikuwa zaidi ya bendi. Yanatoka na Twanga Leaders Club mchana hadi usiku wa manane TCC Club Chang’ombe. Utawaona Chang’ombe, Leaders, Mango, Bilcanas na popote pale wanapopiga. Waliipandisha bendi na kuishusha. Uwezo huo walikuwa nao. Waliweza kusajili au kufukuza mwanamuziki yeyote ambaye hakuenda nao sawa.

Pia Soma

Advertisement
Maeneo yote hayo yalikuwa na totoz mtambuka. Wale wa Disco na kwenye bendi. Ni tofauti na wale ambao ungewakuta baa kubwa za kukesha. Kulikuwa na wa kwa Macheni pale Migo. Baa ilikuwa marufuku kuliko wanamuziki kibao. Si Magomeni Dar nzima ilipajua pale. Ndivyo ilivyo kwa Jolly Club na Q Baa.

Jolly na Q Bar vilikuwa viwanja vya wadada flan waliokata ringi. Walikuwa katika kipindi cha kuweka au kuchana mkeka. Betting yaani. Wakivizia vibabu vya Kizungu vya kuwatoa nje ya Bongo au kuzaa navyo. Ilikuwa ni jamii flani ya totoz wenye makazi Msasani ya Namanga. Wapo waliopaa Ulaya, kuzalishwa na Wazungu kama si kujengewa mijengo. Na waliozeeka au kuishi kilofa hadi leo.

Lakini dunia ya sasa wote hao unakutana nao eneo moja. Kama siyo Instagram kuzama DM, basi ni kwenye grupu za WhatsApp. Huko ndipo mambo yote matamu yanaporatibiwa. Twanga Pepeta, Bilcanas, Mambo Club, Blue Palm, kwa Macheni, Jolly Club au Q Baa. Yote hayo unayakuta mtandaoni. Hakuna usumbufu wa kuhangaika usiku wa manane. Maendeleo.

Diamond na wanamuziki wenzake wanapiga pesa mitandaoni. Wambea na madalali wa vyumba, viwanja na magari wanapiga pesa mitandaoni. Vyombo vya habari na wanahabari nao wanapiga pesa mitandaoni. Lakini vicheche vya mjini vilianza kitambo sana kupiga hizi pesa. Long time wanapiga pesa kwa simu, Yahoo messenger, Facebook, BBM kabla ya whatsApp na Instagram.

Lakini sasa imekuwa rahisi. Kuna magroup mengi ya WhatsApp ambayo asilimia 90 watu wanajadili ngono tu. Na ndo yenye wafuasi wengi kuliko ya asasi za kiraia au Tasaf.

Leo hii Mondi katemana na mtoto Tanasha. Kusema tulijua lazima waachane utakuwa uchawi tu. Na kushangaa kuachana kwao ni ushirikina zaidi. Dunia ya sasa maajabu ni mtu kama Mondi kudumu na dem mwaka mzima. Insta pekee achana na mikusanyiko ya shoo na safari zake. Inatosha kuvuruga ubongo wa msela yule wa Tandale. Ndo ukweli.

Kama mtu wa kawaida ambaye hajulikani hata mtaa wa pili. Lakini insta anakutana na majaribu ya totoz kama zote DM. Unategemea nini kwa Simba wa Tandale? Wakati mwingine haya maendeleo huja na hasara kubwa. Dawa ni Mondi kuachana na matumizi ya baadhi ya vitu kama insta? Je yupo tayari? Kivipi yaani? Maisha kwake yatakuwa kama jela ya kipuuzi.

Wanandoa mitaani waachane na simu za WhatsApp ili wasiingizwe kwenye grupu ambazo huchangia kuchepuka? Maana mitaani nako ndoa zinapukutika kila uchwao kama zinatafunwa na nzige. Nani wa kujifanya bwege aache kutumia simu janja? Dunia yote ipo kiganjani halafu utake watu warudi miaka 50 nyuma? Haiwezekani, kifupi sahau.

Kwanza ukitaka demu akuteme kataa kumnunulia simu janja. Na ukitaka demu asikuzingatie omba namba yake wakati huna simu ya WhatsApp. Kwanza picha linaanza mademu hawapendi kutumiwa wala kutuma meseji za kawaida. Lazima utatemwa. Simu janja haikwepeki. Ukikosa simu janja mwezi tu huna tofauti na wafungwa tena mahabusu wa vituoni.

Unafiki ni kushangaa Mondi kutodumu na mademu. Tukiwa wasema kweli tutashangaa Mondi kudumu na Tanasha muda wote huo. Dogo ana kila kitu anachohitaji kuwa nacho msela wa umri wake. Ni vigumu sana kuishi kiinjilisti na kiustaadhi, kama kile afanyacho ni upuuzi. Huenda mimi ningekuwa yeye ningekuwa mpuuzi mara tatu yake. Ogopa sana pesa na umaarufu.

Ieleweke kwamba muziki na totoz ni kulwa na doto. Alikuwepo Fela Kuti Mnigeria na Bob Marley Mjamaica. Hawa wote walikuwa mastaa wa muziki katika kipindi chao. Fujo zao kwa viumbe uzao wa Delilah. Huyo Simba wa Tandale akasome mara buku. Ndivyo ilivyo kwa wanamuziki wengi ukiachana na mwamba wa muda wote Michael Jackson.

Kwa aina ya maisha na kazi za Mondi. Kitu rahisi zaidi kwa sasa ni kutabiri juu ya uhusiano wake wa mapenzi. Hata akija Rihanna hii leo na kuweka makazi yake Madale, wataachana tu. Namna Diamond anavyowapata hawa mademu ndivyo anavyoachana nao. Wengi huvutwa na Diamond Platinamuz na siyo Naseeb Abdul, huo ndio ukweli. Wema Sepetu pekee ndiye mwenye uwezo wa kusema akaeleweka, kwamba alimpenda Naseeb Abdul na siyo Diamond. Lakini mapito yake yanamuweka mbali sana na uso wa Mondi wa leo. Mademu wengine sijui kina Zari na wenzake kamba tupu. Walimuelewa msela mwenye jina na pesa. Walivyojileta ndivyo walivyoachwa huo ndio ukweli.

Demu ukijirahisi sana kwa msela pia atakuchukulia kirahisi na kukutema kirahisi.

Na jamaa anatumia fursa. Wanaojileta ili wapate jina na pesa. Naye anawatema ili apate kiki na pesa. Hajawahi kumuacha Demu kindezi bila yeye kupiga pesa. Kuanzia Wema na Diamond Are Forever mpaka Zari na Wasafi Festival.

Wanamtumia na yeye pia anawatumia. ‘Bata tredi’.

Chanzo: mwananchi.co.tz