Mwanamitindo wa Uingereza, Naomi Campbell amepigwa marufuku kuwa Mdhamini Mkuu wa hisani katika Shirika la misaada la Fashion For Releaf baada ya kugundulika kuwa amekuwa akifuja pesa za misaada na kuzitumia katika matumizi yake binafsi badala ya kuzipeleka kwa Watu wenye uhitaji ambao ndio walengwa.
Imegundulika kuwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2016, Fashion for Relief ilichangisha £4.8m (Tsh. Bilioni 17,556,906,691/-) kutoka kwenye maonyesho ya mitindo lakini ilitoa £389,000 tu (Tsh. bilioni 1,422,840,979/-) kama ruzuku kwa Mashirika ya misaada yanayohudumia Watu wenye uhitaji.
Campbell alianzisha Shirika la Fashion For Relief mwaka 2005 kuchangisha fedha kwaajili ya kuwasaidia wale wanaoishi katika shida na umaskini kwa kuunganisha tasnia ya mitindo kama nguvu ya wema na kurejesha kwa jamii kupitia shughuli mbalimbali za kijamii.
Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa tangu kuanzishwa kwake, Fashion For Relief ilipeleka mipango na miradi ya mitindo huko New York, London, Cannes, Moscow, Mumbai na Dar es salaam na kuchangisha zaidi ya dola milioni 15 (Tsh. bilioni 40,894,659,570/-) lakini huenda fedha hizo zote hazijafika kwa Walengwa husika.
Uchunguzi umegundua kuwa Campbell alikua akitumia pesa nyingi za Shirika hilo katika matumizi yake binafsi ikiwemo kuishi katika Hoteli za gharama, matibabu ya mwili na kulipa Walinzi wake.