Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nandy: Wanasema Nianze na Davido

Davido Nandy Nandy na Davido

Sun, 13 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAJINA yake halisi ni Faustina Charles Mfinanga ila kwa wapenzi wa muziki wake wanamwita majina mengi kutokana na mambo anayoyafanya kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva. Wanamuita Nandy The The African Princess, Wengine wanamuita Nandera au Nandinyo; Jeshi la Mtu Mmoja, Mwanamke wa Chuma na mengineyo.

Kuwa na mashabiki wengi na wanaokusapoti kwa kile unachoifanya huwa tunasema kwamba ni sehemu ya mafanikio makubwa kwa Nandy kuwa miongoni mwa wasanii wachache ambao ni mfano wa kuigwa kwa upande wa wasanii wa kike.

Nandy ni miongoni mwa wanamuziki wakubwa waliofanya vizuri akitwaa Tuzo ya Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2021 huku akiwa ni miongoni mwa wasanii wachache wa kike wenye ushawishi na mashabiki wengi kwenye soko la muziki Afrika Mashariki kwa jumla akifuatiwa na bibie Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

Mwanadada huyu amekuzwa kwenye misingi ya kimuziki tangu akiwa binti mdogo, wakati huo akiimba kwaya kwenye makanisa ambayo alikuwa akihudhuria ibada mbalimbali.

Nandy amepitia katika Nyumba ya Vipaji ya Tanzania House of Talents (THT) ambapo alijifunza mambo mengi kuhusu muziki, jambo ambalo limemfanya kuwa Nandy huyu wa sasa ambaye kila jukwaa amekuwa akisikika.

Nandy alianza kusikika mwaka 2016 baada ya kuibuka mshindi wa pili katika shindano la kuimba lililoandaliwa na Tecno na mwaka huohuo aliachia wimbo wake wa Nagusagusa uliomta-mbulisha vyema.

Mwaka 2017 aliachia Wimbo wa One Day ambao ulimpa nafasi ya kushinda Tuzo za AFRIMMA kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.

Pia amewahi kutamba na nyimbo kama Kivuruge, Ninogeshe, Hallelujah, Acha Lizame, Leo Leo, Nimekuzoea na nyingine nyingi.

Hadi sasa, Nandy amefanikiwa kuachia albam moja ya The African Princess huku akiachia EP kama zote.

IJUMAA SHOWBIZ inakukutanisha na Nandy ambapo amezungumza mambo mengi aliyoweza kujipanga kwa mwaka huu kubwa zaidi ni kuamkua kuwaachia mashabiki wake wenyewe ndiyo wampangie cha kufanya kwa mwaka.

IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi Nandinyo?

NANDY: Salama kabisa Mungu ni mwema kila kukicha.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwanza heri ya Mwaka Mpya Nandy…

NANDY: Ahsante sana nashukuru na kwako pia.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa utabiri wako mwaka huu unauwonaje?

NANDY: Nauona uko poa sana kwa sababu mambo ni mengi, halafu ni mazuri kwa kweli.

IJUMAA SHOWBIZ: Ukisema mambo ni mazuri unatukanganya kidogo, hebu tudadavulie au ni mambo ya ndoa?

NANDY: Hapana, hapa sizungumzii ndoa jamani ni suala zima la kazi zangu za muziki basi.

IJUMAA SHOWBIZ: Okey ahsante kwa kutuondolea ukakasi, tunaona umeweza kutuwekea wazi kolabo zako za mwaka huu…

NANDY: Ndiyo.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini na wakati tunaona wasanii wengine wanafanya siri hadi kuita vyombo vya habari?

NANDY: Mimi nimeona hakuna haja ya kufanya hivyo maana ni kupoteza muda tu wakati mashabiki wangu kazi hiyo wanaiweza.

IJUMAA SHOWBIZ: Umetoa listi ya wasanii ambao wapo kwenye kolabo zako, Davido, Patoranking, Sauti Sol na Makabila na ukasema mashabiki wako wakuchagulia wa kuanza naye, je, ni nani ambaye ana kura nyingi zaidi?

NANDY: Ni kweli kazi hiyo ilikuwa ni ya mashabiki wangu kunichangulia; yaani kwa mwaka huu kazi ni kwao, mimi wakiniambia kitu, nafanya hichohicho.

IJUMAA SHOWBIZ: Kati ya hao kura nyingi zimeenda kwa nani?

NANDY: Soon nitatangaza.

IJUMAA SHOWBIZ: Kumbuka hapo mwanzo umesema huna muda wa kufanya press (kuzungumza na vyombo vya habari) ili kuweka mambo hadharani mbona tena unatuweka kwenye bracket?

NANDY: Siiti press jamani ila kura si hadi zihesabiwe? Siwezi kusema uongo.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa harakaharaka tu maoni yanasemaje, jina gani linasemwa sana?

NANDY: Wanasema Davido.

IJUMAA SHOWBIZ: Umeshakutana na Davido na kwa muda mchache ulioweza kukaa naye ni mtu wa aina gani?

NANDY: Ni mtu mwenye utu, heshima na nidhamu na anajua anachokifanya.

IJUMAA SHOWBIZ: Tukirudi kwenye mahaba mahabani (Valentine’s Day) hii hapa, ni keshokutwa, vipi kwa upande wako?

NANDY: Ni kweli huu ndiyo mwezi wenyewe wa kujua unapendwa au hupendwi.

IJUMAA SHOWBIZ: Hivi Nandy mwaume wako akikuweka profile picha ndiyo anakupenda au?

NANDY: Hapana siyo kila anayewekwa profile picha anapendwa, kuna usemi kaka yangu Mpoki namnukuu anasema; “Siyo kila anayewekwa profile anapendwa hata picha ya panya ipo kwenye kopo la sumu…”

IJUMAA SHOWBIZ: Wewe hupendi kuwekwa kwenye profile ya mpenzi wako?

NANDY: Mimi huwa sing’ang’anii kuwekwa kwenye profile, nikishawekwa moyoni inatosha.

IJUMAA SHOWBIZ: Mwezi wa mahaba wasanii wengi huwa wanaachia ngoma kwa ajili ya Vallentine kufurahi na mashabiki wao, wewe vipi mbona hatuoni jambo?

NANDY: Mambo yapo hata ukiangalia nimeamua kutoa ofa spesho kwa ajili ya wapendanao?

IJUMAA SHOWBIZ: Ni ofa gani hiyo?

NANDY: Watu wakae tayari Jumatatu siyo mbali jamani.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamwambia nini mpenzi wako Valentine hii?

NANDY: Nampenda na ninampenda tena.

IJUMAA SHOWBIZ: Mtakuwa wapi na kipenzi chako?

NANDY: (anacheka) jamani hadi sehemu tutakayokuwepo niseme bwana ee naogopa manyakunyaku.

IJUMAA SHOWBIZ: Kwa sasa upo kwenye uhusiano serious, je, unaonaje mambo yanayoendeleo kati ya Kusah na Ruby huko mtandaoni?

NANDY: Kwa kweli sina cha kuzungumza maana wale ni wazazi tayari.

IJUMAA SHOWBIZ: Hauoni kwamba wanaaibishana?

NANDY: No comment, siwezi kuzungumzia mambo ya watu.

IJUMAA SHOWBIZ: Ahsante sana.

NANDY: Karibu tena muda wowote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live