Wikendi iliyopita baada ya malkia wa muziki wa Bongo Fleva kutoka lebo ya WCB Wasafi, Zuchu kuanzisha utani mitandaoni dhidi ya wasanii wenzake wa kike, wasanii hao wamejibu mipigo.
Zuchu alianzisha timbwiri kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema kwamba yeye amebarikiwa mno si tu kwa utunzi wa nyimbo bali hata kuimba na sauti nzuri pia.
Alisema kwamba kutokana na baraka hizo tele, katu hafai kushindanishwa na wasanii wa kike katika ukanda wa Afrika Mashariki. Badala yake, aliwataka mashabiki wote kuanza kumshindanisha kwenye safu ya wasanii wa kiume kwani katika ligi ya wasanii wa kike ameshahitimu.
Akizungumzia weledi wake katika tasnia ya muziki na mafanikio makubwa ambayo amezalisha ndani ya miaka miwili tu tangu kutambulishwa rasmi na lebo ya WCB, Zuchu aliwasifia wazazi wake na Mungu kwa umahiri huo.
“Niwashukuru wazazi wangu ni kwa ajili yenu na uwezo wa mwenyezi Mungu tu. Kwa uandishi wangu yafaa kuwekwa kwenye ligi za wanaume, wanadada wenzangu nitawaonea tu kiheshima lakini,” Zuchu alisema.
Alizidi kujipiga mikogo kwa kusema kwamba uwezo wake katika kutunga mashairi ni mkubwa hata anaweza kuamuandikia msanii wa kiume na mtu asigundue. Alidokeza kwamba mwezi huu ataachia madude mawili ya kutetemesha.
“Ujuzi wangu wa kalamu ni hatari hadi naweza kumuandikia msanii wa kiume ngoma na mtu asijue. Naachia ngoma mbili mwezi huu,” Zuchu alitanua kifua.
Hili lilipokelewa kwa njia tofauti tofauti na watu haswaa wasaniiwenzake wa kike ambao alisema anawachorea nje katika ushindani.
“Woow! Mungu ni mwema mwaka mwingine tena wa kuendelea kuwa balozi wa GUINESS PAN AFRICA @guiness na Gues waht??? Wame double the digits!! Imagine unaamka na 250k.... JESUUUUUS MUSIC IS SOFT 000000000H,” Nandy alimtania kwa kile wengi walisema anajaribu kutonesha kidonda cha Sakata la Zuchu kukataa dili la kuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya vileo kutokana na Imani zake za Kiislamu.
"Wasanii tupunguze mikwara tutauana kwa pressure," mkali wa iokote, Maua Sama alishindwa kujizuia.
"Ngoma zenu 10 kwa mwezi ndo ngoma yangu 1 kwa mwaka," Ruby alimtupia kiazi moto.