Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nandy, Billnass acha muvi iendelee

Nandy Pic Data Nandy, Billnass acha muvi iendelee

Sat, 22 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MWEZI mmoja tangu Billnass aachie ngoma yake mpya ya ‘Tatizo’, watu wameutafsiri wimbo huo kama ni kijembe kwa mchumba wake Nandy.

Hili linakuja baada ya wawili hawa kutoonekana pamoja kwa muda mrefu na kuvumishwa kuwa wameshabwagana.

Makala haya yanaangazia ishu zinazowazunguka wawili hawa wenye maisha ya kuachana na kurudiana.

Maswali ya Nandy yanamkera Billnass

Kwa nyakati tofauti wakiulizwa, Billnass huonekana zaidi akichukizwa na swali hilo kila waandishi wanapombananisha, yaani kwa kifupi hataki kumzungumzia kabisa Nandy.

Kitendo cha kusema kwamba wimbo wa Tatizo ni stori ambayo iliwahi kumtokea huko nyuma alipokuwa na uhusiano na mtu lakini kwa kuwa hakuwa na pesa akamuacha, inachochea mitazamo ya watu kwamba kamuimba Nandy kwa sababu kimwana huyo aliwahi kuondoka kwa Billnass na kuhusishwa na mpango wa kufunga ndoa na bosi wa kituo cha radio, Ruge Mutahaba, ambaye bahati mbaya alifariki kabla ya ndoa hiyo na kisha mrembo huyo akarejea kwa Billnass.

Mapichapicha Insta na bethidei zao

Maswali ya kuwa wameachana au laah, yanatokana na ukweli kwamba wawili hawa wamezoeleka kuonekana wakiwa wawili mara kwa mara ikiwemo kutupia mapichapicha kwenye kurasa zao za Instagram wakiwa kwenye mapozi tofauti.

Aidha, unapofika muda wa kusherehekea siku zao za kuzaliwa huwa wanatumiana ujumbe mzito wa mahaba kwa kila mmoja kuonyesha anavyomkubali mwenzie, lakini mwaka huu haijaonekana na hata Nandy alivyofanya hivyo kwa mwenzie, Billnass hakujibu kitu.

Hakuna sapoti kuachia nyimbo

Kama vile haitoshi wapenzi hawa wamekuwa wakisapotiana wakati wanaachia kazi mpya, lakini hii imekuwa tofauti.

Hivyo wanazengo wanazidi kuwa na maswali na kupigia mstari majibu yao kuwa wawili hawa hawapo pamoja tena baada ya Nandy miezi miwili iliyopita kuachia kibao cha ‘Leo Leo’ alichomshirikisha mwanamuziki kutoka DR Congo, Koffi Olomide.

Licha ya kufanya hivi, BillNass alipiga kimya na alipokuja kuulizwa kulikoni, alieleza kuwa menejimenti zao zimeamua kila mmoja afanye kazi kivyake.

Pia ilipofika zamu yake alipoachia wimbo wa Tatizo, kwa upande wake Nandy aliweka andiko ambalo lilihisiwa kuwa huenda ni kijembe kwa kuandika “sasa hivi bana hadi wasanii wa Hiphop wanaimba taarabu.”

Nandy aeleza umuhimu wa Billnass

Ukiachilia hayo, wiki mbili zilizopita wakati Nandy akiwa anazindua tamasha lake la ‘Nandy Festival’ pale jijini Dar es Salaam na kuulizwa kama katika tamasha hilo watu wategemee kumuona Bilnenga, majibu ya Nandy ni kwamba msanii huyo atakuwepo kwa kuwa ni kati ya mtu ambaye mashabiki wanamuhitaji sana katika tamasha hilo na walipotaka kujua ukweli zaidi kama wameachana au lah, mrembo huyo alijibu ’Ni lini tumewahi kusimama mbele za watu au kutangaza kuwa tumeachana, hayo ni maneno ya watu yapuuzeni kwani huwezi kuwazuia kuongea.”

Tamasha hili linalotarajiwa kuanzia kurindima Juni 5, mkoani Kigoma litapita mikoa mitano nchini na miji miwili ya Mombasa na Nairobi, nchini Kenya.

Huenda ushiriki wao katika tamasha hili ndio utaweka wazi kwamba wawili hawa wapo pamoja au lah.

Billnass afuta picha zote za Nandy

Kwenye ukurasa wa Instagram wake, amefuta picha zote alizowahi kupiga na Nandy au zinazomuonyesha Nandy, jambo ambalo ni tofauti kwa upande wa Nandy ambaye picha ya mpenzi wake ipo na ni ile aliyoiweka Aprili 11 akimuwishi siku yake ya kuzaliwa kwa kuandika “More life... Happy B day!..”

Yanayojiri kati ya wawili hawa acha picha liendelee.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz