Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Namuona Shilole kwenye mwili wa Asha Baraka

63885 Shilolepic.png

Mon, 24 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hakika ni msichana toleo la 1953 kushuka chini. Kabla Tanu haijazaliwa. Kukutana naye 2019 ni maajabu. Si kizazi cha miaka ya 60, 70, 80, 90 wala 2000. Unachotakiwa ni kuelewa tu kuwa alikuwa wa pekee. Nilijikuta napigwa ganzi mwilini na kushindwa kuelewa nini kilifanya niwe mbele yake kwa wakati ule.

Sekunde kadhaa zilipita kabla ya kukumbuka kuwa natakiwa kutoa pesa. Nikajikuta naulizia jina lake badala ya namba ya wakala.

Hata yeye aligundua kuwa nilipatwa na jambo lenye uhusiano na mshituko.

Licha ya kuzuga lakini uso wake katu haukuficha kunyanzi la papi za midomo kama mtu anayejizuia kucheka.

Nikarudi kutoa pesa kwa mara ya pili. Safari hii nikitoa kiasi kingi zaidi, bado haikusaidia. Aliendelea na msimamo wa kukataa kutoa namba yake ya simu. Angekataa akiwa kakunja ndita ingekuwa afadhali. Tatizo alikataa huku akitoa tabasamu lile la kukaribisha mtu futari. Na kufanya nihisi ataitoa. Nikarudi mara ya tatu. Hola!

Nilitumia njia zote za ushawishi kumuaminisha kuwa kamwe sitamsumbua.

Pia Soma

Nikimhakikishia kwamba atakuwa rafiki yangu wa kawaida. Ushawishi na sauti niliyotumia sijawahi tumia popote. Mgombea urais 2020 atakayeniiga vile kwa kuomba kura za Wabongo, saa 12 asubuhi atakuwa Ikulu. Bibie aligoma.

Mpaka leo nahisi atanipa. Kwa tabia ya kukataa huku uso akiurembesha kwa tabasamu mujarabu. Kuna watu omba Mungu usikutane nao kabisa maishani.

Ukikutana naye basi iwe mara kwa mara siyo mara moja na kukuacha ubaki na kumbukumbu kichwani tu. Itakutesa. Na ndo kilichotokea kwangu wiki iliyopita.

Nilikuwa ndani ya Dodoma. Nimechukua bodaboda mitaa ya Area D nikielekea stendi ya mabasi ya Shabiby. Sikuwa na keshi mfukoni nikamuomba bodaboda anipeleke sehemu yenye huduma ya M Pesa. Na ndo majanga yalipoanza. Stendi ya Shabiby hapo hapo ndipo zilipo huduma za fedha.

Badala ya kutoa pesa nikakate tiketi nirudi Daslama mjini. Nikajikuta namaliza muda wangu kwa muhudumu wa M Pesa. Licha ya kupoteza muda sikuambulia lolote zaidi ya kumbukumbu ya urembo wa ajabu wa mrembo yule. Kwa sura tu alikuwa bado kiumri, ana umbo na ngozi isiyotaka kutoa jibu la kabila lake.

Ningemleta Daslama mjini kisha nikamkutanisha na waongozaji wa filamu. Kupitia yeye pekee soko la filamu lingerudi kwenye chati. Anafaa kuigiza bila kupewa elimu ya uigizaji. Kwani wasanii waliopo wana elimu ya sanaa? Hakuna.

Wengi wao kanjanja walirukia baada ya kuona sanaa ni mgodi wa kuchuma pesa.

Mjini mipango tu. Hakuna aliyetegemea wakati ule kama Shilole angekuwa staa wa muziki. Alipoona tundu liko wazi akalivaa na kudumbukia.

Leo hii vijana wengi hawajui kama Shilole ni zao la Bongo Movie. Hata sanaa ya filamu nayo hakuwa na elimu nayo. Ni maisha tu ndiyo yaliyompa jeuri ya kukomaa na kuzidisha juhudi akawa staa wa filamu.

Alipoweza kwenye filamu akapata nguvu na kuona lolote linawezekana. Alipotazama sura za watoto wake zikimtazama yeye kama baba kama mama. Akashika maiki, akapanda jukwaani na kina Linnah, Mwasiti, Recho na wenzao. Akapasua anga. Hata shughuli zake za upishi ni ubishi wa maisha.

Si Bongo tu. Katika uso wa dunia hii ukiamua na kupania kitu unaweza. Ni juhudi na imani huku ukimtanguliza Mungu. Nani aliamini Sugu angekuwa mbunge wa kwanza kutoka kwenye zao la hip hop?

Leo hii ameshakuwa ‘legendi’ tayari kwenye ubunge. Alipoonyesha njia mwenzake Profesa Jay naye akafanya kweli.

Shilole anabaki kuwa alama ya mwanamke mpambanaji. Ndo kizazi kipya cha kina Asha Baraka, Fatma Karume, Shy-rose Bhanji na wengineo.

Kuna kina Shilole wengi mitaani kwa kuwa yeye ni staa anasimama kwa niaba yao. Ukweli ni kwamba hivi sasa madem wapambanaji ni wengi kuliko masela.

Unaweza kumchukulia poa kama huyajui maisha. Ukifuatilia mapito ya Shilole, utakubaliana nami kuwa anastahili heshima. Ni sahihi kumuita mwanamke mpambanaji. Mapungufu mengine hata mawaziri, wabunge na viongozi wa kiroho wanayo. Tusimamie kwenye upambanaji wa maisha.

Ndo maana huoni Shilole akihangaika kupunguza mwili. Kupost wigi jipya instagram wala kushinda kwenye maduka ya nguo na salon kutangaza bidhaa za watu.

Lakini wenye akili tegemezi tunawaona kila leo kwenye mitandao ya kijamii. Wako ‘bize’ kuuza sura na kubishana na mashabiki. Huo muda haupo kwa Shilole.

Kuna madem tunawaona wanasukuma ndinga na kula bata deile. Chanzo cha kipato kinabaki kuwa kitendawili. Hana kazi wala biashara ya kueleweka ila kila wikiendi yuko Nairobi.

Ni dhahiri anadanga kwa sababu hatuhitaji mganga wa jadi atueleza hali halisi ya maisha kitaa. Si filamu wala mchele wenye soko la maana wakati huu.

Akili tegemezi ya mwanamke hufanya awe mtumwa na kujikuta akimkosoa Mungu. Au kulazimisha Mungu amuumbe kulingana na matakwa ya mwanaume.

Wanaoendeshwa kwa matamanio ya wanaume hujikuta wakiiharibu miili na afya zao. Utumwa ni ule ambao unasababishwa na tamaa za wanaume.

Yaani wanachotaka wanaume ndicho wanachokifanya wadangaji. Miaka ya nyuma wanaume walikuwa wanataka wanawake wembamba (English figure). Ilikuwa habari ya mjini. Wakaanza kupambana kupunguza miili. Wakishinda njaa ili mradi akipita barabarani avutie macho ya wanaume. Ubwege mtupu.

Kama hiyo haitoshi yakaja masharti mengine. Bila rangi nyeupe huyo dem siyo mzuri na hafai. ‘Carolite’ zikahusika wakakoboka hadi Wazungu wakaanza kuogopa maana kasi ilikuwa kubwa.

Wanaume sijui walirogwa na nani. Wakaanza kuwapeleka puta wanawake kuwa wenye matiti makubwa ndo mzuka. Wenyewe wanaita big boobs.

Brah za kutunisha vifua vya kina dada zilianza kuuzwa kwa kasi. Ghafla wakageuka msambwanda na hapo ghafla tu Mchina akahusika.

Watu wakahamia kupaka hadi ugoro. wenye ‘flat screen’ waliitwa kila jina mtaani. Yote hiyo ni njaa na kuishi kwa kudanga. Wanalazimika kuendana na matakwa ya madanga.

Wakaja na kali ya mwaka kutaka wenye ‘blue eyes’ (macho ya blue). Inasikitisha sana. Kila dem akataka awe na macho hayo. Mara ghafla makope ya bandia yakawa ndo mzuka. Dhumuni ni nini? Madem wapate upofu? Madem acheni undezi wa kufanya kile wanachotaka wanaume badala ya mioyo yenu.

Kila siku mtajibadilisha mpaka mpoteze uhalisia wa koo zenu. Miili mnaifanyia ‘sevisi’ kama bodaboda kwa sababu tu wanaume wanataka hilo.

Ina maana wakianza kuvutiwa na wabwia unga nyote mhamia kwenmye kubwia mitaani? Puuzeni tamaa za wanaume. Fanyeni kile roho zenu wenyewe zinataka.

Ukipata nafasi fuatilia mihangaiko ya Asha Baraka kwenye muziki wa dansi. Waliomuita ‘Iron Lady’ hawakukosea hata kidogo.

Alikalisha madume wenye ukwasi na ‘koneksheni’ kubwa mjini. Alisimama kama mama na kuwapa heshima kina Ally Choki na wenzake mbele ya mbwembwe za Wakongo kama kina Nyosh El Sadat na wengineo wengi tu.

Wabongo tuna tabia ya kuzoea shida. Tumeshazoea hata kukosa burudani ya dansi. Na mbele ya safari bila kuacha alama hata za wino kama hivi, historia zitawakataa mashujaa wa kike kama Asha Baraka. Na maendeleo yanafuta utu kiasi kwamba bidii ya Shilole inazidiwa na post za mawigi zilizozagaa kwa kasi mitandaoni.

Hata kale karembo kalikokataa kunipa namba kule Dom. Ndo sampuli ya kina Shilole. Ni kahangaikaji na kanaridhika na mshahara kanakoupata kwa kazi ya kuhudumia watu pale.

Kama kangekuwa na akili tegemezi ya udangaji, kangetoa namba haraka na mpaka sasa ‘kangenisevu’ kama ‘Bebi King’ang’anizi’.

Chanzo: mwananchi.co.tz