Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NO AGENDA: Siku Dk Kigwangalla akimshitukia Diamond Platnumz itakuwa too late!

89614 Diamond+pic NO AGENDA: Siku Dk Kigwangalla akimshitukia Diamond Platnumz itakuwa too late!

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

NOVEMBA 30, 2019, Uwanja wa Taifa, Freetown, Sierra Leone, Diamond Platnumz alikuwa mwanamuziki ‘top-heavy’ kwenye tamasha la Ecofest.

Ufafanuzi kidogo ni kuwa Ecofest ni bonge la tamasha kwa nchi za Afrika Magharibi. Ni kama Fiesta kwa Tanzania, lakini Ecofest huchukua nafasi katika nchi kadhaa za Afrika Magharibi.

Waandaaji wa tamasha hilo, iliwapendeza kufanya kazi na Diamond Patnumz, pamoja na wasanii wengine wa nyumbani na wageni. Hata hivyo, msanii mkuu na mzito alikuwa Diamond. Ndio, Diamond ndiye alikuwa top-heavy artist wa Ecofest Sierra Leone 2019.

Novemba 28, Diamond alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Lungi, Freetown. Hali ya hewa ikabadilika Sierra Leone. Novemba 29, gazeti kubwa Sierra Leone la “Ayv News” likaandika habari kubwa ukurasa wa mbele yenye kichwa chenye maandishi makubwa mpaka kero “Diamond in Freetown”.

Tuanze alipotua; maelfu ya wananchi wa Sierra Leone walikuwa na njaa kali ya kumuona Diamond. Walitamani kumgusa, kupiga naye picha, wazima kwa walemavu. Yalikuwa mapenzi makubwa kuliko ambayo staa huyo huyapata akiwa nyumbani Bongo Land.

Mengine nilijaribu kuyapuuza, kwa kuamini ni stunt za shoo. Kama ile walemavu kutanda njiani kuungoja msafara wa Diamond, kisha akashuka kwenye gari na kuanza kuwapa pesa mmoja baada ya mwingine. Niliona ni kiki tu!

Hata hivyo, tathmini ya jumla ikanipa jawabu tofauti. Diamond amefanikiwa kuteka nyoyo za wapenda muziki Sierra Leone. Diamond anaishi ndani ya fikra na mioyo ya wananchi wengi Sierra Leone.

Jina lake ni Diamond. Sierra Leone ni nchi inayochimba almasi kwa wingi. Almasi ndio diamond. Wenyewe wanaiita nchi yao ni land of diamonds (nchi ya almasi). Basi walimuona Diamond kama kafika nyumbani kwao. Yes, Diamond in the land of diamonds.

Muda wa shoo ulipowadia, habari ilikuwa tofauti kabisa. Diamond aliwaimbisha Wasierra Leone wimbo kwa wimbo. Pamoja na ulinzi wa wanajeshi lakini mashabiki walivamia jukwaa mara kwa mara ili kumshika Diamond na kumkumbatia. Massive love!

Kingine ambacho itakuwa dhambi kutokukisema ni kwamba ule uwanja haukujaa bali ulifurika. Na umati wote ulimuitikia Diamond wimbo kwa wimbo. Nyimbo za Diamond zimo ndani ya maisha ya Wasierra Leone.

TAFSIRI KWA AKILI

Kilichoonekana Freetown ni kuwa Wasierra Leone wanampenda Diamond hadi kutamani awe mali yao. Na hivyo ndivyo ambavyo sanaa na michezo humfanya mtu apendwe kwenye mataifa mengine kuliko kwao. Ni namna ambavyo kazi yake inavyopokelewa.

Catalonia, Hispania, Lionel Messi anapendwa kuliko Argentina. Mbwana Samatta huimbwa uwanjani Ubelgiji na mashabiki wa klabu yake ya Genk, kuliko anapokuwa Tanzania. Anfield, Liverpool, Merseyside, MO Salah huimbwa kuliko Misri.

Turin, maskani ya Juventus, Cristiano anapokea love ya kutosha kama vile yupo hood aliyozaliwa na kukulia, Funchal, Madeira, Ureno. Kipaji kikitumika ipasavyo, humfanya mwenye kipaji kuwa raia wa nchi nyingi. Popote anaweza kuishi.

Kama ambavyo Watanzania wanaweza kujiona wamebarikiwa kumpokea Justin Bieber, Rihanna au Beyonce Knowles, endapo atachagua kuishi Tanzania, ndivyo Sierra Leone ilivyoonesha kwa Diamond.

Na sio Sierra Leone tu, Diamond kwa sasa ni multinational citizen. Yaani ni raia wa mataifa mengi. Tofauti ni nyaraka. Ni Mtanzania kwa kuzaliwa na ndio asili ya wazazi wake, hata hivyo kazi yake inamfanya awe na fursa ya kuishi nchi nyingi, na akiomba uraia anapewa fasta.

Mataifa mengi Diamond anakwenda kufanya shoo na kiwango cha kukubalika ni kikubwa. Kitendo cha kuwa top-heavy artist wa Ecofest, Sierra Leone, ni mapinduzi makubwa. Kutoka Tanzania ya unyonge wa kupokea wasanii kutoka nje, tena Afrika, sasa Diamond anageuza matukio. Anakwenda kwao, anachukua pesa zao na wasanii wao anawafunika. Hayo ndio mambo ambayo akina James Dandu wakiambiwa sasa hivi kaburini walipolala, hawaamini.

Ukiambiwa Diamond kwa sasa ni multinational citizen, usipige hesabu ya watoto wawili aliowatengeneza na Mganda cheupe, Zari The Boss Lady au mmoja kutoka Kenya na potable Tanasha Dona, tunazungumzia muziki. Biashara yake na matokeo makubwa ambayo amekuwa akiyatengeneza siku hata siku.

TUTANUE WIGO

Ali Kiba muziki wake unakubalika sana Kenya. Wakati wowote Ali anapokwenda kufanya ziara ya kimuziki Kenya, hupata mapokezi makubwa sana. Wakenya wanampenda. Ali anapofika Kenya ni kama yupo nyumbani. Si kwa sababu kaoa Mkenya, la, kazi yake ya muziki inamfanya awe multinational citizen.

Ali akiwa Uganda anapata mapokezi makubwa na anawaimbisha watu nyimbo zake, akikanyaga Muscat, Oman, hapati shida jukwaani, anakuta watu wapo tayari kupokea huduma yake na nyimbo zake wanazijua.

Hivyo ndivyo hasa inatakiwa kwa wanamuziki wengine wote. Kukuza muziki wao ili upenye nchi mbalimbali, waweze kuwa wenyeji wa mataifa mengi.

Sio kama Jux kumpata mrembo wa Thailand au Ommy Dimpoz kuzaa na Mspaniol, bali nguvu ya muziki wao iwawezeshe kutawala runinga na redio za mataifa mengine. Ndipo wataweza kuwa raia wa mataifa mengi.

Kama ambavyo Diamond Platnumz ameweza kuifanya Afrika yote kuimba muziki wake. Anawarahishia zaidi kwa kurekodi nyimbo za kucheza kuliko zenye ujumbe na hisia. Jiulize ni nchi gani ya Afrika ambayo Diamond hapokelewi?

Harmonize yupo safi. Tayari nchi kadhaa zinamjua. Akiwa na spidi nzuri muda si mrefu atakuwa kwenye daraja moja la kuwa raia wa nchi nyingi, kama kaka yake, Diamond, alivyo kwa sasa. Ukiwa mwanamuziki wa nchi moja, tena ileile uliyozaliwa na kukulia, wewe ni local sana.

Diamond anaonesha mwanga na wengine waige. Wajitume kufanya muziki na kujitangaza. Diamond hajawa raia wa nchi nyingi kwa bahati, isipokuwa ni matokeo makubwa ya uwekezaji. Wengine nao wawekeze. Diamond ameweza ana nini na wengine washindwe kwa nini?

Tunahitaji kuona Ali Kiba akifika Ivory Coast nchi inasimama kama Sierra Leone ilivyosimama kwa sababu ya Diamond. Vanessa Mdee akikanyaga Gambia, iwe patashika. Nandy akitua Conakry dunia ijue kuwa African Princess ameingia.

Kwa kila hatua kubwa ambayo wanaumuziki wetu watapiga na kutikisa nchi nyingine, Taifa litajivunia. Maana popote watakapokwenda, itaelezwa kuwa ni msanii kutoka Tanzania. Hiyo ni promosheni kubwa.

Jiulize Diamond aliitangaza nchi kiasi gani Sierra Leone na nyingine ambazo hutia timu kikazi? Ukifika hapo waza sasa, ingekuwaje Diamond angekuwa na ujumbe wa kuitangaza nchi na vivutio vyake kipindi chote alipokuwa Sierra Leone na mbele ya wananchi takriban 70,000 ambao wanakadiriwa kuwepo Uwanja wa Taifa, Freetown wakati wa shoo?

Kumbe sasa Bodi ya Utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii haijui jinsi ya kumtumia Diamond. Anaweza kutangaza vivutio vya nchi kwa ukaribu na mbele ya watu wengi. Waziri Hamis Kigwangalla upo wapi?

Mtu anatembea nchi mbalimbali na kufuatiliwa na mamilioni ya watu wa nchi hiyo, lakini hata fulana ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro, kuinadi Serengeti au Ngorongoro hana. Ni Mtanzania. Vivutio vya Tanzania.

Wizara inashindwa kuingia makubaliano na Diamond kwa nini? Wizara, Bodi ya Utalii, mpo? Sema nini, inawezekana siku wakiwashitukia akina Diamond, Ali Kiba, Harmonize ni dili la kuutangaza utalii wa nchi, itakuwa too late!

Chanzo: mwananchi.co.tz