Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NO AGENDA: Konde Boy anavyofosi kuunda ‘Big 3’ na Mond, Kiba

90922 Pic+konde NO AGENDA: Konde Boy anavyofosi kuunda ‘Big 3’ na Mond, Kiba

Mon, 6 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

MIONGO tisa na ushee iliyopita Marekani ilichapika sana kiuchumi. Zilikuwa zama za Great Depression, yaani kipindi kirefu cha anguko kubwa la kiuchumi (the longest-lasting economic downturn).

Wakati huohuo, zikaibuka zama za Adui wa Umma (Public Enemy Era), kisha Taifa la Marekani likateswa na vita ya soko haramu (black market). Kilikuwa kipindi kigumu mno.

Pakuanzia ni hapa; Aprili 1930, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uhalifu ya Chicago, Marekani, Frank Loesch, aliutumia msemo wa Kilatini, Hostis Publicus (adui wa watu), kumtangaza haramia Alphonse Capone ‘Al Capone’ kuwa adui wa watu wa Chicago.

Al Capone au Scarface kwa jina lingine, alikuwa mtu hatari kwa wakati wake. Alimiliki kundi la uhalifu wa kupangwa (organized crime), lililoitwa Chicago Outfit. Aliihenyesha dola, mpaka Loesch alimtangaza adui wa watu.

Baada ya tangazo la Loesch kuhusu Al Capone, maeneo mbalimbali ya Marekani yaliitika, majina ya wahalifu yalitajwa kwenye mamlaka za majimbo na majiji. Umma wa Wamarekani ulijulishwa kuhusu maharamia mbalimbali.

Matamko hayo kwa wingi wao kuwalenga maharamia waliokuwa wakiitikisa Marekani kwa wakati huo, yalisababisha kipindi hicho kiitwe Zama za Adui wa Umma (Public Enemy Era) kwa Marekani.

Public Enemy Era ni kipindi cha kati ya mwaka 1930 mpaka 1935. Wahalifu wakubwa zaidi waliosababisha miaka hiyo iitwe Zama za Adui wa Umma Marekani ni Al Capone, John Dillinger (siyo DJ JD wa Tanzania), Baby Face Nelson, vilevile Bonnie na Clyde.

Maharamia wengine ni Pretty Boy Floyd, Machine Gun Kelly, Ma Barker na Alvin Karpis. Kwa pamoja, majina hayo yalitamba sana. Walitafutwa na serikali na waliihenyesha dola. Watu hao walimiliki makundi makubwa na hatari.

Public Enemy ni nyakati zilizoibuliwa kipindi cha mdororo mkubwa wa kiuchumi kati ya mwaka 1929 mpaka 1939. Mdororo huo ulisababishwa na anguko la uchumi wa viwanda na kuporomoka kwa soko la hisa kwenye nchi za Magharibi.

Hivyo, Marekani ikiwa inateswa na hali mbaya ya kiuchumi, vilevile ilikuwa ikisumbuliwa na uhalifu wa mipango, uliokuwa ukitekelezwa na makundi hayo hatari. Vyombo vya dola Marekani vilipelekwa puta na maharamia hao ambao walijijengea umaarufu mkubwa wa kuogopwa. Ongeza na kushamiri kwa black market.

Mwaka 1932 aliingia madarakani, Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Delano Roosevelt ‘FDR’, memba wa koo ya Roosevelt (Roosevelt family) ambaye alimshinda Rais wa 31, Herbert Hoover ambaye uongozi wake ulishindwa kudhibiti Great Depression.

FDR katika kuikabili Great Depression, alianzisha kampeni aliyoiita New Deal (Dili Mpya) ambayo utekelezaji wake aliugawa katika mpango alioupa jina la R tatu (3 Rs).

R hizo zilikuwa na maana ya Relief (Nafuu) kwa wasio na ajira pamoja na maskini. Recovery (Uhuishaji) wa uchumi mpaka kufikia kiwango cha kawaida. Reform (Mageuzi) ya mfumo wa kifedha na kudhibiti kutojirudia kwa msukosuko wa uchumi wa viwanda.

Miaka miwili ya FDR ofisini, Zama za Adui wa Umma ziligeuka historia Marekani, soko haramu lilidhibitiwa. Mwamko wa kiuchumi ukaonekana, lakini Great Depression haikuisha mpaka mwaka 1939.

Kwa nini mwaka 1939? Jibu ni Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kimsingi Marekani ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wake, kukuza akiba yake ya dhahabu na kutanua sarafu yake kipindi cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Unataka kuuliza kwa nini? Jibu kuwa wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, hakuna nchi iliyofanya biashara sana ya bidhaa za kivita kama Marekani. Hivyo, wakati wa vita, ndipo kiwango cha uzalishaji kwa Marekani kiliongeza na kuongezeka zaidi.

Uhitaji wa silaha ulikuwa mkubwa, hivyo Marekani ilizalisha silaha nyingi na kuziuza kwa mataifa ya Ulaya yaliyokuwa mstari wa mbele kupigana. Chakula kilihitajika sana, Marekani walizalisha.

Kutokana na kiwango cha uzalishaji kuwa kikubwa, hitaji la nguvu kazi lilikuwa kubwa. Ikawa sababu ya watu wengi kupata ajira. Kabla ya vita tatizo la ajira lilikuwa asilimia 25. Mwaka 1941, tatizo lilishuka mpaka asilimia 10.

Marekani walipiga bao kwa sababu hawakuingia vitani (Vita Kuu ya Pili ya Dunia) kama nchi mpiganaji wa mstari wa mbele. Wakati Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Hispania na mataifa mengi ya Ulaya, yaliathirika kiuchumi kwa vile ziliingia vitani mstari wa mbele, Marekani yenyewe ilicheza salama kwa mbali.

Marekani iliingia vitani kama mtoa msaada kwa Uingereza na mataifa mengine yaliyokuwa yanamkabili Adolf Hitler wa Ujerumani, Japan na washirika wao. Ikafanya biashara na kujenga uchumi wake.

TAFSIRI NINI?

Katika vita kuna fursa. Hutegemea na namna macho yanaona. Hitler alikuwa anawavuruga Ulaya na tamaa zake za kutaka kutawala dunia. Marekani walipoona dalili za vita, wakajipanga kupiga hela!

Ndivyo namwona Harmonize a.k.a Konde Boy. Kipindi hiki soko la muziki Tanzania limetekwa na uhasimu wa Diamond Platnumz na Ali Kiba, zipo dalili kubwa kwa Harmonize kutengeneza ngome yake ya kimuziki kupitia mnyukano wa mafahari wawili wanaotawala soko kwa muongo mmoja sasa.

Kwa kila ambaye hafurahii mgogoro wa Ali na Diamond, Harmonize anaonesha anayo mengi ya ‘kuofa’ nje ya mafahari hao wawili. Kama ambavyo Marekani ilikuwa makini kujijenga kiuchumi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Harmonize yupo hivyo pia hasa kujiimarisha kipindi hiki cha ufahari wa Chibu na Kiba.

Kumbe ilikuwa wazi katikati ya mnyukano wa kina Mond zipo fursa nyingi kwa wanamuziki wengine. Bila shaka Harmonize aliliona hilo, ndio maana aliona bora achomoke WCB ya Chibu ili atengeneze ngome yake.

Na baada ya kufanikiwa hilo, Harmonize anapepea. Kwanza anapewa ‘sapoti’ ya nguvu na vyombo vya habari ambavyo havina uhusiano mzuri na Diamond. Wanafanya kama kumkomoa hivi bosi wa zamani wa Harmonize

Pamoja na hivyo, Harmonize ana bidii na mbunifu sana. Mjanja sana kuhakikisha anabaki kwenye mzunguko wa kibiashara. Diamond si anakwenda Kigoma kwenye kutoa shukrani nyumbani kwao kutimiza miaka yake 10 kwenye muziki? Rayvanny pia alipiga shoo Krismasi, Sokoine, Mbeya, kutoa shukurani nyumbani.

Harmonize ametangaza shoo yake ya kuwashukuru watu wake Mtwara atafanya kwa helikopta. Kwamba ataizunguka Mtwara kwa chopa akitoa shukrani. Janki ana balaa si dogo. Na hiyo ndio kuonesha Harmonize yupo makini katika kutengeneza ukuu wake. Anatoa ngoma kali, anajitangaza sana na anao uthubutu wa kutosha.

Wakati wasanii wengi Bongo ni wanyonge linapokuja suala la kuzungumzia majina ya Ali na Diamond, Harmonize haoneshi woga. Anajiona yeye ni mkali na anaweza, ndio maana anafanya makubwa. Wakati huohuo hataki bifu, si kwa Ali, Diamond wala yeyote.

Dalili zinaonesha atafika mbali. Swali ni je, ataweza kuwatikisa mafahari wawili, Diamond na Ali Kiba? Je, atamfanya mmoja aachie ‘bodi’ au atasababisha game la Bongo Fleva liwe na Mafahari Watatu kama zile enzi za kutamba kwa dansi la kina Ally Choki, Prince Mwinjuma Muumin na Banzastone? Yaani The Big Three! Muda siku zote huwa na kawaida ya kujigeuza hakimu.

Kimsingi Harmonize yupo moto kutumia tobo la mnyukano wa Ali na Diamond kujitanua. Mimi naamini anaweza.

Anachopaswa kufanya ni kuthibitisha. Hata sasa, wapo wanaoamini kuwa tayari Bongo Fleva ina “The Big Three” kwamba Harmonize ameshapenya katikati ya Ali na Diamond.

Chanzo: mwananchi.co.tz