Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDANI YA BOKSI: ‘Video’ ya Uwoya, itazame kwa jicho la fursa

69661 Pic+uwoya

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Irene Uwoya wa sasa. Ni Tanzanite na almasi ndani ya mwili mmoja. Miaka zaidi ya kumi inateketea akiwa kwenye kilele cha umaarufu. Alianza kukimbiza kama mshiriki wa umiss. Ni kizazi cha mastaa wa utawala wa Kikwete, ambacho asilimia kubwa kilitokana na shindano la Miss Tanzania 2006.

Washiriki wa Miss Tz 2006, wengi wanapendwa mpaka leo. Wakiongozwa na Wema, Jokate, Anti Ezekiel na Uwoya mwenyewe. Hawa ni wadada wa mjini ambao hivi sasa umri unawatenganisha. Kwa majukumu ya kikazi na biashara, lakini ni kapu moja katika ‘mazao’ ya Hashim Lundenga.

Lundenga na majaji wake, kichwani hili bado wanalo na linawazunguka kama tiara. Tukio la usiku mmoja 2006. Pale Wema Sepetu na Jokate Mwegelo, walipogeuza ukumbi wa Diamond Jubilee, kama majukwaa ya Uwanja wa Taifa. Ilikuwa kama Simba na Yanga zimekutana. Jokate akipita yowe, Wema akipita shangwe.

Bonge la ‘bato’. Watoto wadogo waliofanya watu wazima ukumbini na majumbani wasitulie. ‘Team Wema na Team Jokate’ hii haikupata kutokea kabla na baada. Nani atakuwa Miss Tz wa kwanza ndani ya utawala wa JK? Mwisho mshindi akawa mtoto wa Balozi Abraham Isac Sepetu (R.I.P).

‘Anko’ Lundenga atabaki na kumbukumbu ya shindano hili. Kwa sababu ushindani wa Wema na Jokate ulihama kutoka jukwaani mpaka mitaani. Waliosema Wema alistahili walikuwa idadi sawa na waliosema Jojo alistahili. Hata kama haweki wazi, Jojo hawezi kukiri kushindwa.

Asilimia kubwa ya washiriki wa mwaka ule, waliendelea kutunza majina yao kwenye kilele cha umaarufu kupitia michongo mingine. Wema, Jokate, Uwoya, Lisa na Anti Ezekiel walijikita kwenye filamu. Katika hao ni Anti Ezekiel peke yake ambaye hakufanikiwa kuwepo kwenye tano bora.

Pia Soma

Wema Sepetu akatokea kuwa Miss Tz mwenye umaarufu mkubwa. Lakini hakuwa na mafanikio katika Miss World, kama mtangulizi wake wa mwaka 2005, Nancy Sumary, aliyefanikiwa kuwa Miss World Africa. Lakini Wema akabaki kuwa maarufu na mwenye nyota ya kupendwa zaidi.

Umaarufu ambao hata watu maarufu wakatamani kuwa yeye. Akapendwa na wengi waliompenda na bado wanampenda tu bila sababu. Katika dunia hii wapo watu wa aina hiyo, wanaopendwa bila sababu. Beckham alipendwa na Waingereza kuliko Scholes, ingawa kwangu hakufikia hata robo ya kipaji chake.

Ndo Wema, kuna mamilioni ya watu ambao wanampenda, lakini sababu ya kumpenda hawana. Ni kipawa. Karama ya kupendwa na watu. Hana uwezo wa kuigiza kuliko Riyama au Thea, hafikii hata uwezo wa Johari, ila ndo anapendwa. Hana urembo kuzidi washiriki wote wa Miss Tz, lakini alipendwa zaidi.

Tazama mamilioni ya roho za watu mitandaoni, zilizotaka kujua chochote cha Wema, warembo wa Kikenya Huddah na Vera Sidika, wanaingiza pesa nyingi kwa mfumo ambao Wema kashindwa kuutumia. Waliomzunguka toka mwanzo hawakujua cha kufanya kumgeuza Wema kuwa pesa.

Huddah na Vera hawana vipaji, si waigizaji, si wanamuziki, mamisi’ wala watangazaji, ni wadada wa mjini pale Nairobi, wamepata umaarufu nao wanautumia kupiga pesa, haijalishi pesa wanaingiza kwa namna ipi. Lakini hawatii huruma wala kuendeshwa kibwege na mabwege.

Wema hakuhitaji kubeba bahasha kuomba ajira. Alitakiwa kutafutwa na kampuni za kibiashara, lakini akawa ‘bize’ kuhesabu ‘siksi paksi’ za Dangote wa Tandale, badala ya kina Kelvin Twissa wamsake kwa matangazo. Yeye akawa ‘bize’ kusaka wezi wa kitu chake kwa Diamond.

Kuna mashabiki waliopata mashabiki kwa kuwa shabiki wa Wema. Hukaa vyumbani mwao wakiwa watupu na laptop au simu. ‘Hukomenti’ kwenye kurasa za Wema mitandaoni. Nao wanapata mashabiki na wateja wengi kwa sababu ya kujivisha ushabiki kwa Wema. Haya hayapo tena.

Wema na watu wake waliishia kufurahia ‘komenti na laiksi’ za mashabiki. Badala ya kugeuza kuwa mfereji wa pesa. Alikuwa na mashabiki wengi kuliko Gwajima, Kakobe au Mzee wa Upako. Lakini hajafikia hata theluthi tu ya mafanikio ya hao wazee. Martin Kadinda siwezi kumpa jukumu lolote.

Kama alishindwa kazi rahisi zaidi ya kutengeneza pesa kupitia jina la Wema ataweza lipi? Mtu ambaye kuanzia lips, hips, nywele, kiuno, miguu na kope ilikuwa utajiri? Wakati wa kutengeneza pesa, alitumia kugombea kitu fulani na Penny. Na kumuonyesha Jojo kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa ‘six packs’ za Diamond.

Wema ni kama muda wake umepita. Anaweza kutajirika kwa namna nyingine. Lakini itakuwa kwa kuvuja jasho sana, tofauti na wakati ule ambao angetajirika akinywa maji ya dafu kando ya ufukwe, hata wafia Wema mitandaoni wengi wamejichokea kama si kulea vitoto vyao mitaani.

Hivi sasa kuna Irene Uwoya, kizazi cha Miss Tz 2006. Yupo juu sana kwa sasa, na kipimo chake ni hivi karibuni baada ya kuzuka kwa stori ya video yake ya utupu. Namna ‘alivyotrendi’ katika mitandao ya kijamii na mitaani. Ni picha tosha kuwa hivi sasa ndiye staa wa kike anayekimbiza.

Unadhani ana filamu mpya? Hapana. Hana alichofanya cha ajabu, hata posti zake mitandaoni hazina lolote. Zaidi anatupia picha akiwa na pamba mpya ‘deile’. Lakini ndo ‘totoz’ iliyojenga ‘ushosti’ na midomo ya wambea wa mjini. Anakimbiza sana na kumpiku Hamisa Mobetto.

‘Porojo’ za uwepo wa video yake ya utupu, ule mwitiko wa watu bila hata uhakika kama video ipo au haipo. Iwe ni taa kwake ya kutambua kuwa kakamata nchi. Lolote atakalofanya hivi sasa ni pesa. Lakini nani wa kukaa nyuma ya huyu dada mwenye mtoto mmoja (Krish), apige pesa zaidi? Hakuna.

Mataifa ya wenzetu, hili tukio wangepita nalo na kugeuza pesa. Uzushi ule, umeonyesha kuwa huyu ‘manzi’ nyota yake ipo juu kuliko mawingu ya ‘Pierre Likwidi. Kila kona mitaani, na kurasa za watu mitandaoni stori zilikuwa ni Uwoya. Kama una nyota ya giza ni ngumu kuongelewa vile.

Madogo waliomaliza vyuoni wanawaza kuajiriwa tu. Na walioajiriwa wanawaza mishahara tu. Na mabosi wao wanawaza kuumiliki mwili wa Uwoya tu. Hakuna mwenye akili ya kibiashara ya kupiga dili kupitia jina la Uwoya. Ndo dem anayekimbiza kwa sasa kuliko Zari, Mobetto, Wema na staa yeyote wa kike.

Iko hivi. Kamwe usithubutu kujilinganisha na watu wengine, hili jambo huwa linawatesa wengi sana.

Asikwambie mtu maisha ya watu wengi sivyo kama uyaonavyo. Huenda ukawa na uafadhali kuliko unaowatamani, siku hizi watu wanaekti sana kwenye maisha.

Hata kwenye uhusiano, hali ni ile ile tu labda hutofautiana uafadhali. Jifunze kuikubali hali yako. Jiulize kama wewe unatamani kuwa kama fulani, sasa nani atatamani kuwa kama wewe? Ikiwa wewe mwenyewe unajisaliti na kujikana, nani atakayeiona thamani yako?

Unakuta mtu anapata mfadhaiko kila akimuona jirani yake amepiga hatua fulani, kiasi anashindwa kushughulika na maisha yake. Watu wa dunia ya sasa wanapenda kufuatilia maisha ya watu zaidi kuliko maisha yao, ndo iko hivyo. Tazama mitandaoni kinachofuatiliwa zaidi. Umbea.

Wenye akili nchi za wenzetu, hutumia hiyo kama fursa ya kupiga pesa. Wakati hapa kwetu tunakimbilia kusema “Umbea, hayakuhusu, fuata yako, unanilisha?” Na maneno mengine mengi. Hata Uwoya baada ya uzushi huo, alitoa maneno ya kuwasuta watu wanaotaka kuona ‘video’ yake.

Uwoya atazame tukio la uzushi huo, kwa jicho la fursa kwake. Heka heka za watu kuongelea kitu ambacho hakieleweki chanzo wala mwisho wake kinakupa picha ya kukubalika na jamii. Alifunika kila kitu mpaka ‘clip’ za Mzee Makamba na Kinana, kila mtu akili na macho yakawa kwa Uwoya.

Dunia ya sasa wanaotajirika ni ‘wanaotrendi’ mitaani na mitandaoni. Na hauwezi ‘kutrendi’ kama haukubaliki. ‘Kutrendi’ ni utajiri, usipuuze na kuona kama umbea.

Uwoya wa sasa hana kazi mpya mitaani, ila ndiye ‘manzi’ ambaye anawasha masikio na macho ya watu mjini. Ni dili.

Chanzo: mwananchi.co.tz