Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDANI YA BOKSI: Unahitaji darasa zaidi kumfahamu Harmonize?

68578 Pic+haminize

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha mjini. Kibaridi fulani kisichoumiza ngozi kikipiga. Lakini vilivyopo mezani vinapambana nayo kibabe. Na kutufanya tuwe salama bila kurundika nguo nyingi mwilini. Ni vinywaji vya kupita kooni, kujaa tumboni, kisha kwenda kuvuruga akili na ‘ofu kozi’, kuchangamsha mwili. Ni Mitungi. Nina siku ya tatu Arusha, bado ukaaji wangu wa shida. Nakaa upande utadhani nina jipu kwenye kalio, kumbe ni kile kilichopo kwenye ‘waleti’. Mkwanja umejaa. Siku zote anayetamani pesa isiishe, huisha haraka. Sasa mimi nilitamani iishe bila mafanikio. Nilifanya fujo zote lakini bado pesa ipo.

Meza imechafuka vinywaji. Tunazungukwa na warembo wakihudumia kwa kiwango cha Qatar Air Ways. Walifaa kuajiriwa na shirika la ndege kwenye mataifa makubwa. Lakini warembo wale wapo pale baa, wakihudumia walevi fulani wasiojua hata thamani ya mwanamke. Ilinishangaza kidogo.

Hata hivyo hawakufikia urembo wa mrembo wangu, alikuwa bora zaidi hata kwa lugha tu. Wakati wao waliweza kujibu na kuuliza Kiingereza. Huyu alibishana kwa Kiingereza. Kwake ni rahisi kusutana Kiingereza kuliko Kiswahili. Ogopa sana mtu wa hivi. Ogopa!

Madem wengi hupambana kujua kujibu na kuuliza kwa Kiingereza. Ili wadange kwa Wazungu wajane. Lakini huyu Kiingereza kilitamani kukaa kwenye ulimi wake. Maana akikasirika anaweza kuongea Kigiriki na Kipoland wiki zima. Kiasili ni Mbongo ila ana vimelea vya Kipoland na Kichaga.

Totoz la kishua toka mitaa ya Njiro, lilinielewa ‘muhuni’ wa kitaa. Nitafeli vyote, lakini si kazi ya kufanya totozi ifurahie maisha. Hiki ni kipaji changu kama Samatta na soka. Usiku ulikuwa mtamu kiasi cha kusahau kama nilizaliwa na mwanamke kama yeye. Acha kabisa, yasikukute haya.

Nywele zake zimetawanyika kichwani kama mkia wa ndege tausi. Macho, ngozi, midomo, shingo, shepu mpaka vidole vya miguuni ni zaidi ya jini. Alifaa azaliwe nyakati zile za kina Delilah, si wakati huu wa kina Amber Rutty. Nikipewa urais siku hiyo hiyo namhonga Mlima Kilimanjaro kisha nang’atuka.

Pia Soma

Trisha ndo jina lake. Usiku ulipokuwa mwingi nilimuaga mshikaji ili niende kula pepo na Trisha wangu. Mshikaji aliniitikia kishingo upande nikashangaa. Sikujali, nikashika kiuno cha Trisha nikasepa. Nikimuacha na wahudumu wawili akifanya zoezi la kuchekeshana nao kibwege kila dakika.

Kutoka furaha kubwa hadi huzuni kuu. Nilijikuta nimelala kibwege kama paka kwenye fuko la ungo. Pombe zote zilikata na kuishia kutazama runinga na kusikiliza radio. Dakika za majeruhi kabisa niligundua sina zana. Hata niwe ‘bwiii’ kiasi gani. Siwezi kwenda ‘drai chama’ na dem nisiyemjua. ‘Neva!’

Ndo maana bado tupo na nguvu zetu mpaka leo. Tuko makini kama askari wa zamu pale Ikulu. Runinga ikawa ndo ‘mfariji’ wangu. Katika hali hiyo nilipogundua kitu. Kwamba radio na runinga na redio za mikoani ‘zina shoo laivu’ sana kwa wasanii wetu. Maana mchana wake nilisikiliza sana redio pia.

Nikakumbuka mshikaji alikua na lundo la ‘zana’. Nikatoka nje na kumuomba lakini akaninyima. Hakuna sababu nyingine zaidi ya wivu. Baada ya kuona nimeopoa mtoto kiwango kuliko misikule niliyomuacha nayo mezani. Trisha alikuwa mzuri kuliko Arusha yote. Poa tu, nikalala nikiliwazwa na ngoma za zamani.

Usiku ulikuwa mkubwa, ikawa vigumu kutoka kutafuta ‘zana’ mitaani. Jamaa alichojivunia ni kumiliki ‘zana’. Kuninyima kwake ni wivu tu. Kutaka nishindwe kufikia kilele cha mbio za mwenge. Si kesi, kulala na Trisha bila kufanya chochote ni burudani kuliko yeye kwenda kulala na yale mazombi.

Hili la ‘fea’ kwa wanamuziki naliona sana mikoani. Wiki iliyopita nilikuwa Mbeya, mambo ni hivi hivi. Mikoani ndipo utajua kuwa Nature bado anahusudiwa, na nyimbo zake zinatwangwa. Kuna tofauti na redio za Daslama. Nyimbo zinachosha ni zilezie, kuna hulka flani hivi ya kaubaguzi amazing.

Unafungulia redio zaidi ya tatu. Zote unamsikia msanii mmoja tu, kwa nyimbo au habari zake. Ataongelewa hata siku tatu. Kwenye hili mikoani wako tofauti. Dar wasanii ni walewale WCB, Kiba, Nandy, Jux, Vanessa sijui Ben Pol. Mzunguko wa habari na nyimbo za wasanii ni ule ule kila siku. Redioni na mitandaoni. Hapa ndo sehemu pekee ambayo mwanamuziki anastaafu kama askari magereza. Kama mwalimu au ofisa ugavi wa kijiji cha Naliendele. Anastaafu muziki kivipi? ‘Midia’ za mikoani ziko ‘fea’ sana. Hawastaafishi muziki wala wanamuziki kama Daslama mjini.

Msanii yuko vilevile, sauti na utunzi bora. Lakini watu wanataka astaafu ‘gemu’. Redio hazitaki kupiga nyimbo zake wala kumpa ‘eataimu’ ya mahojiano. Na mashabiki wehu utawasikia mitandaoni wakimponda. Si kwa ubovu wa nyimbo, hapana. Eti yupo muda mrefu kwenye ‘gemu’ hivyo apishe wengine. Q Chilla ampishe nani ambaye hii leo ana ubora zaidi yake? Astaafu ‘gemu’ kwa tatizo gani linalombana? Mtu ambaye robo tatu ya umri wake kautumia kwenye muziki. Unataka astaafu ili akafanye shughuli gani nje ya muziki? Mtangazaji unayetaka Chilla awapishe kina Jux, umetumia kigezo gani?

Kuna wanaoshangaa huyu mtu anapita njia za kawaida lakini mbona anafanikiwa sana? Baraka ziko mikononi mwa watu, na sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Kundi la watu linapokuombea heri hakuna uchawi wa kuzuia milango yako. Zingatia sana hili.

Unajua ni ‘maduu’ na ‘mabitozi’ wangapi mashabiki wa Chilla? Wapo walipo wakishukuru alichofanya Harmonize kwa mtu wao? Dogo ambaye wakati Chilla akiziliza totoz na kuingiza mapene. Yeye alikuwa Naliendele kama si Masasi, asijue cha kufanya.

Leo hii anamshika mkono mtoto wa mjini. Anamuinua bishoo wa Daslam mjini. Anampatia ndinga, anamtia mkwanja, kisha anaiambia dunia kuwa anataka Savimbi asimame tena toka jalalani. Savimbi si chuma wala mninga. Ni binadamu mwenye mwili wa nyama, machozi yake mbele ya wana habari yana maana nzito.

Chilla ni nani kwa ‘Konde Boy’ hadi apewe usafiri na kuingizwa studio? Ni kweli Chilla ni mgodi uliotelekezwa, akisimamiwa vyema gharama zote zitarudi. Lakini ni wangapi wenye pesa mjini hawajafanya hili. Hawakuona haja kumshika mkono. Wengi walimpa bia na kumsifia kindezindezi tu.

Kuna vipaji vingi mitaani vinafubaa na kujifia kwa sababu mioyo kama ya ‘Konde Boy’ ni michache. Chilla alikuwa wakati tu anaingia kwenye kituo cha redio anaonekana kituko. Analia asaidiwe bila mafanikio. Pengine kwa kutojua waanzie wapi au makusudi. Chilla si wa kujiuliza uanzie wapi kumsaidia.

Wasanii wengi wa kitambo kuna sehemu walikwama. Kwa ujinga au kukwamishwa na mfumo uliopo. Konde Boy anafanya alichofanyiwa na Diamond. Alikuwa hajulikani, Diamond akamshika mkono. Chilla mkwamo wake wengi waliujua, ila ni Konde Boy aliyemshika mkono leo.

Madogo walikuwa mashabiki wa ngoma zake kama ‘Tanita’. Walidata na viitikio kwenye madude yenye tani nyingi kama ‘Asubuhi’, ‘My Boo’, ‘Usinitenge’, ‘Kama unataka dem’ na nyinginezo. Zote zilifanya kina Konde Boy wajue kuna maisha nje ya kuwinda panya na kulima korosho.

Sasa wenye kujua umuhimu wa watu kama Chilla ni wachache. Wenye kuguswa na kuteswa na mkwamo wa wale walioonyesha si wote. Konde Boy hili suala haigizi, katazame anachomfanyia Dully Sykes. ‘Shoo’ zote kuanzia ‘audio’ na video dogo anasimamia.

Harmonize anapita njia za kakaake Diamond. Kuanzia uimbaji, staili, kujituma kikazi mpaka kushika mikono wenzake. Ni mgawanyo wa kazi tu, wakati Diamond anabeba wasiojulikana, Konde Boy anabeba waliofanikiwa lakini wakakwama. Acheni hawa madogo waingize pesa. Siku alipomuita Chilla studio. Na Chilla kuuliza nauli ya ‘bodaboda’, ilimuumiza. Hakutegemea staa wake wa toka utotoni akose nauli hata ya ‘bodaboda’ achilia mbali ndinga. Wakati yeye kagawa ndinga kwa mshua na Bi. Mkubwa siku mbili nyuma. Zingine zikiwa kwake kwenye maegesho.

Tunahonga pesa ngapi? Tunachezea pesa ngapi? Tunaingiza ngapi? Kwa nini kioo chake kiishi kwa shida wakati maisha bado yanawezekana? Kujiuliza haya maswali ni moja. Kuumizwa na hili ni jambo la pili. Na kumsaidia mtu kiasi kile ni jambo lingine kubwa na tofauti.

Kupigana tafu namna ile kwa vijana ni jambo zuri, hatuwezi kusikia vilio vya kindezi kitaa. Maisha ya mjini yalimkwamisha Chilla, lakini akapambana na moja. Kitendo cha kuachana na matumizi ya dawa za kulevya. Bila kushurutishwa wala kupelekwa ‘rehab’. Ilitosha kujua ‘msela’ anapambana.

Ilitosha kumsamehe. Na kumuona shujaa anayehitaji msaada. Hadi hapo hakupaswa kuachwa aendelee kuzurura kitaa. Mwisho angejihisi dunia imemtenga na kuamua kujifariji upya. Na faraja yake ingekuwa ni unga tena na pengine baadaye mauti. Kisha watu kumlilia na kumpamba.

Kuna wakati unajiuliza, bila uwepo wa watu waliomshika mkono Diamond na kuwa pale alipo. Kina Konde Boy, Van Boy na wenzao wangekuwa wapi? Hakuna namna nyingine zaidi ya vijana kushikana mikono. Maisha ndo haya hakuna mengine. Ukiondoka leo ndo imetoka. huwezi kurudi tena. Wanadamu tunaishi mara moja tu. Kuna wajinga wanakebehi aina ya ndinga aliyopewa Chilla. Hawa ni matope kama matope mengine.

Utadhani huyo Chilla alishiriki shindano ndipo akazawadiwa hilo gari. Kumbe kapewa bure kiroho safi bila kazi yoyote aliyofanya. Kuna wakati mtu unajiuliza, hivi Harmonize aliyempa ndinga Chilla. Anaishi dunia moja na yule bwege aliyeninyima ‘kondomu’ kule Arusha ili nisifurahie maisha na Trisha?

Chanzo: mwananchi.co.tz