Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDANI YA BOKSI: Nini Tiffah... ‘Anti’ Wema alipewa gari ya milioni 40

Wemaaa Wema Sepetu

Sun, 14 Aug 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Huwaoni pale Mlimani City, Dar Free Market wala Cape Town Fish Market sijui. Ni vigumu kumiliki akaunti za mitandaoni. Hata kama wanazo pia hazina mashiko, zile akaunti za benki ndio zenye uzito zaidi kwao.

Maeneo mengi ya mjini hawayajui. Unakuta mara ya mwisho kufika Magomeni ni mwaka 2006. Pengine alikwenda kupakwa hina kwa Da’ Tabu au kwenye msiba wa baba wa shosti yake. Hawapatikani ovyo!

Wanakopita ni Bagamoyo Road. Ally Hassani Mwinyi, Bibi Titi na Nyerere Road kwenda Airport. Hii Morogoro na Mandela Road huona kama kuna fujo. Hawataki vurugu za madereva walioshiba pombe za kupima dukani kwa Mangi.

Mitaa yao ni ile ya Mbweni Mbweni, Ununio Ununio upepo unapovuma kule. Ni ‘Maanti’ flan hivi wale classic sana. Ambao huvaa miwani, miguuni kote kuna vikuku vya gold au silver. Na ngozi zao hazina ushirikiani mzuri na jua la Dar.

Vinywaji vyao ni ‘impotedi’ vinakuja na meli achana na loko bia. Mikononi wana simu ‘latesti’ tupu za gharama kinoma. Bei ya sawa na ploti ya Geza Ulole Kigamboni. Shingoni ni cheni na vidani vya gharama.

Siyo vilaza. Vichwani mwao wengi wana CPA, MBA na PhD sijui. Noma! Wamepaki ndinga flan hivi na husikii wakipayuka ovyo wala kucheka kwa nguvu kishambenga. Uchekaji wao unaendana na wingi wa pesa.

Wakiwa sehemu zao hawanyanyasi wahudumu. Hupiga stori hata na waosha magari kwa heshima sana. Kukuita mai lavu, bebi, darling kwao ni kawaida sana. Wana shepu flan hivi zimenona na vitambi kwa mbaali.

Lugha laini hutawala vinywa vyao, tena ni kwa muungwana yeyote bila kujali hadhi. Ila sasa kama unataka kwenda nao sawa tulia. Usikurupuke kuomba mzigo. Utakula za chembe kama Mandonga uchakae.

Madogo tafuteni pesa kokote iliko. Na ukiipata ifiche, itunze, ionee wivu kuliko eneo lolote la mwili wako. Ukitaka kutajirika lazima uwe na wivu na pesa yako na ujue kuitumia kwa staha. Kisha toa kidogo kwa wenye mahitaji.

Diamond, aliuza mpaka mitumba, lakini hakupata pesa. Akaamua kujiingiza kwenye muziki siyo tu apate utajiri, bali apate unafuu wa maisha. Lakini leo hii ni mmoja wa madogo matajiri. Kakulia kwenye umasikini kama masela wengi. Ambao muziki au soka huwa kimbilio lao.

Aliuvamia muziki akiwa hana kitu. Mungu kamjaalia. ‘Of coz’ bidii na kujielewa ni vyanzo na sababu za vipato vyake. Pesa ya muziki ni kama ya soka au kamari. Ukishindwa kuwekeza sasa ukiwa kwenye chati, utachekwa na wanaokuzunguka kwa sasa kama mfalme. Ukipenya na kupiga pesa. Piga pesa kila inayokatiza mbele yako.

Kusanya pesa kama TRA, huku ukiilinda sana heshima yako. Usiichekee pesa hata sekunde. Kamata, ficha huku ukitoa fungu la kumi kama sadaka. Ukiwa juu piga pesa kama vile kesho unaaga dunia rasmi. Piga pesa sana. Kusanya pesa, na uitunze ishike na adabu.

Usicheke na kima ujanani ukiwa na nguvu, utachekwa na sokwe kesho kutwa uzeeni. Ukijua umetoka katika umasikini, kuwa na adabu na senti inayoingia mfukoni. Unaweza kuwa siyo mtu wa klabu. Siyo mlevi wala mpenda anasa na starehe za kidunia. Lakini ukawa na udhaifu fulani wa tofauti.

Udhaifu ambao unateketeza pesa katika daraja lilelile la mlevi au zaidi. Kama mzinzi na mpenda anasa za kila aina. Kuna vitu mtoto wa masikini unatakiwa kuvikwepa ili kujenga baadaye yako.

Siri ya utajiri ni kuingiza kingi na kutumia kwa kiasi. Hakuna uchawi zaidi ya huo. Kuna zile shughuli za kujionyesha kwa watu ambazo wala hazifanani na mtoto aliyekulia katika umasikini. Achana nazo.

Kuna mambo yatafanywa na watoto wako. Ambao kwa wakati huo wao wataitwa watoto wa tajiri kutokana na namna ulivyotengeneza maisha yao kabla. Ujanani wewe piga pesa, siyo kuteketeza pesa.

Wanamuziki wengine wanataka kuwa sehemu alipo Diamond. Bila kupita njia alizopita. Wanataka ‘laifu staili’ ya Mondi, huku pesa za video tu wakiomba kwa ‘madoni’. Hatua hii Mondi alipita miaka mingi nyuma.

Huwezi kutaka uwe sawa na Mondi, mwenye soko kubwa mpaka Sierra Leone. Wakati wewe hata Tandamti na Narung’ombe unapita kwa mguu bila kutazamwa na yeyote. Pambana kwanza kujijenga kwa jina na kipato.

Mlio nyuma ya Mondi pigeni kazi kwa ajili ya Bongo. Kamata pesa na ‘fansi’ wa hapa kabla ya kuwaza kwa kina Davido. Tengeneza ‘ufalme’ wako wa wafuasi wako hapa nyumbani kabla ya kutafuta wafuasi kwa jirani.

Mondi hakuanza ghafla. Aliiteka Bongo, akaiteka Afrika Mashariki. Kabla hajaanza kuwakalisha kina Tekno, kwenye vibaraza vya mama zao huko Abuja na Lagos. Alijitekea kijiji chake ‘homu’ kwanza.

Haiwezekani uingize pesa kama Mandonga, kisha uishi kama Joshua Anthony. Utafeli tuu! Wekeza kwanza vya kutosha, maisha unayotaka sasa wataishi watoto wako. Hasira za maisha duni tuliyoishi, tulipize kwa watoto wetu.

Sisi hata tutajirike kwa kiwango gani, dunia itatumbua kama watoto wa masikini mpaka tunakata roho. Na hata wadau wa muziki wanahitaji kubadilika kifikra. Tunaposema wadau ni pamoja na Serikali. Wafanye wanachofanya kina Konde, kisha nao wapeni shoo za kujitolea kwenu.

Hivi sasa vigumu kumuona Mondi kwenye shoo za nyumbani. Mpaka aandae mwenyewe pengine. Ukumbi gani hapa wa kumlipa promota pesa zaidi ya milioni mia moja na upuuzi? Tukubaliane kuwa hakuna.

Hutaki? Ukiangalia mikononi mwake. Vidoleni mwake, shingoni mwake na kinywani mwale. Kaweka mamilioni ya pesa kwa vito vya thamani. Kuna kama milioni 300 mwilini. Huyo mtu utampa shoo ya Buza kwa Ujugu?

Tunamuongelea mtu ambaye kabla hajazaliwa Tiffah na wadogo zake, miaka tisa iliyopita alimpa ‘Anti’ yao Wema, gari ya milioni 40. Tengeneza pesa na himaya yako kwanza hapa, la sivyo utachekesha.

Leo hii pesa ambazo angeziteketeza katika kaunta za Sinza na Kinondoni. Ndizo anzonunulia ndinga anayotaka na mijengo aliyoota wakati akilaza mbavu zake mitaa ya Tandale. Hii ni ‘prinsipo’ tu wala siyo uchawi.

Wiki iliyopita gumzo alikuwa Mondi na binti yake Tiffah. Baada ya kutua Nairobi na ndege binafsi wakitokea Afrika Kusini. Akakiwasha kwenye kampeni za Raila Odinga, na kurudi ‘Sauzi’ na ndege ileile.

Wengine tukabaki kupeana stori tu mitandaoni za kiasi alicholipwa na Odinga. Wakati yeye akiwa na binti yake ‘Sauzi’ wakikata keki ya ‘besidei’ ya Tiffah.

Haya maisha siyo muujiza ni mipango, bidii na kumuomba Mungu. Achana na bata la ‘besidei’ ya Tiffah. Miaka 9 iliyopita ‘Anti’ yao Sepenga alikula ndinga la milioni 40 kwenye besidei yake. Tupambane ili tusiwe mashahidi wa maisha ya masela wetu kila siku. Twenzetu Lupaso mtu anapasuka leo mapemaa!

Chanzo: www.mwananchi.co.tz