Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDANI YA BOKSI: Nandy kusoma inaumiza kuliko kuandika talaka...

75787 Pic+nandy

Mon, 16 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Yes. Ni kiumbe mwenye utajiri wa mashabiki. Pengine kuliko staa yeyote wa kike. Ingawa hivi sasa umaarufu wake unafubaa kama ukuta wa Uwanja wa Karume pale Ilala. Yes, unafubaa. Anatoweka. Hata mishe zake hazina utamu wa kuzisoma wala kuzisikiliza. Ni Wema Sepetu.

Katumika sana. Hashitui tena. Siku zote alikuwa kama ngazi ya kupandia watu kwenye mlima wa ustaa. Kanumba pamoja na ukali wake kwenye sanaa. Lakini urafiki wake kwa Wema lilimuongezea idadi kubwa ya mashabiki. Kabla ya kuwa na Wema hakuwahi kukaa kwenye kurasa za udaku mbele.

Hata Chalz Baba alipaa juu zaidi baada ya urafiki au ukaribu huo. Na si Chalz Baba tu, bali bendi nzima ya Twanga Pepeta. Ilikuwa inajaza watu pale Mango na maeneo mengine kutokana na uwili wa wawili hawa. Wema alifikia daraja la kugeuza chupa ya bia kuwa dhahabu. Yes, ndo ukweli. Safari ya Diamond kuanza kutikisa nchi ikichagizwa na uwepo wa Wema. Akiwa na singo mbili tu tayari alianza kukaa kwenye kurasa za mbele za magazeti ya udaku. Hili halikuwa jambo dogo kwa mwanamuziki chipukizi. Ila Wema alimfanya dogo huyu mwenye makuzi ya Tandale awe lulu kwa wadaku.

Diamond hakufikia uwezo wa Barnaba wala Belle 9. Lakini akawa mkubwa kuliko wao ndani ya muda mfupi. Mifano hai ni alipokwenda msibani kwa Kanumba pale Vatican Sinza. Watu wakasahau kuwa ni siku ya huzuni. Alipotokea tu shangwe zilikuwa kubwa kama goli la Kagere mbele ya Waarabu pale kwa Mkapa.

Hiyo yote si kwa sababu ni mwanamuziki wa ajabu. Hapana. Sababu ni Diamond wa Wema Sepetu. Leo hii yuko mita laki tatu mbele ya Wema kimaisha. Wema yuko pale pale na Kiingereza chake. Dada yetu katumika tu kupandisha. Wakimuacha bila kumshika mkono, ama sivyo hashikiki. Inaumiza.

Wema ndiye chanzo cha hawa wanamuziki kutengeneza kiki za kidwanzi. Wakiamini kuwa Diamond alipata mafanikio kwa stori za urafiki wake na Wema. Hili ni kosa kubwa sana. Wema hakuhitaji kiki ili aandikwe bali alihitaji kujificha ili asiandikwe. Lakini alisakwa na kuandikwa kila siku. Kwa sababu alikuwa mauzo.

Pia Soma

Advertisement
Hili jambo linamtesa mpaka leo hata Diamond mwenyewe. Hii leo hawezi kutoa wimbo bila kuzusha la kuzusha. Kwa sababu ya kukariri utaratibu wa miaka saba nyuma pale alipozitawala mbavu za Wema. Kwamba alipoandikwa sana mwenye kurasa za magazeti zilimuongezea kiki na mshindo wa ngoma zake.

Sasa kuna Nandy, alama na maana halisi ya uwezo wa kutambua vipaji kutoka kwa Ruge (RIP). Kaacha alama kuu na alama hiyo ni Nandy. Kuna Linnah, Amini, Mwasiti, Barnaba na wenzao. Ila Nandy yuko juu kimuziki na kimaisha kwa ujumla. Wengi walidhani kifo cha Ruge kungemuathiri, lakini imekuwa tofauti.

Yupo kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro. Anawatazama wanamuziki wenzake wa kike kwenye viunga vya Moshi. Game liko ndani ya brah yake. Analiendesha. Analiamrisha. Linamtii. Anajituma. Ana pesa. Ni maarufu na anayependwa. Kuna watu maarufu lakini hawapendwi. Hata Hitler alikuwa maarufu.

Na unaweza kuwa na pesa na usiwe maarufu. Kuna matajiri wa kike wangapi mjini wakipita Kariakoo hakuna anayewatazama? Hakuna uchawi kama kujituma na kujitambua. Utafanikiwa tu. Nandy anavyo vyote. Achana na nyimbo hata ukimtazama akihojiwa anavutia kwa sura na namna anavyojieleza.

Tatizo la Waswahili ni kutopenda mtu mmoja awe juu kila siku. Tunataka kuona mtu anapanda na kushuka. Furaha yetu ni kuzalisha kina mastaa masikini. Tunakerwa kuona Nandy akipaa kila siku. Hata kama anajituma na kupambana. Tunataka kuona mtu anapaa juu na kushuka chini ghafla.

Hasira za kutopenda hilo tunalihamishia katika kutafuta mtu wa kumfunika..Wabongo wanalazimisha upinzani wa Nandy na Ruby. Hakuna lolote zaidi ya kuona anapatikana mtu wa kuwa juu ya Nandy.

Hasa madem wenzake baadhi, wanakerwa na umaarufu wa Nandy. Hata kifo cha Ruge kwao walidhani ni mwisho wa dogo kisanii.

Mafanikio yake hata uwepo wake duniani. Kuna wengi waliongea vibaya kuhusu yeye. Mpaka mtu unalazimika kuamini kuwa hawapendi hata aendelee kuwa hai. Sasa watu wenye mioyo hiyo ya kipuuzi wanatulazimisha tuamini kuwa alikuwa anabebwa na Ruge. Hayupo sasa na Nandy ndo anazidi kukimbiza zaidi.

Leo ukimuongelea kwa sifa nzuri, utaambiwa hamfikii Ruby. Wanalazimisha vita ya uhasama kama ile ya Dai na Kiba. Davido hafikii hata robo ya sauti ya Beka Fleva. Lakini nani mwenye mafanikio na umaarufu kati yao? Daraja la Nandy hivi sasa si la kiki za kibwege. Kishavuka hiyo hatua ya kutengeneza kiki kabla ya kutoa ngoma.

Nandy hahitaji kuiba tukio lake na Billnass ili ngoma yake ibambe. Billnass anamjua nani Sudan Kusini? Ni midundo mizuri na mtiririko mtamu wa maneno ili hata asiyeelewa lugha basi afurahie midundo na melody.

Mwacheni dem apige pesa. Aliwakilishe taifa. Afurahie kujituma kwake. Atimize dua za wazazi wake juu yake.

Ni dem flani hivi asiye na elimu kubwa wala kukulia katika maisha bora. Anachofanya na kuingiza pesa, hajarithi kwa baba kama Mo au Manji. Ni dem flani aliyekuwa na ndoto za kuingia kwa pesa yake kwenye shoo za Jide. Achilia mbali kuimba kwenye jukwaa la Fiesta. Leo anawanunulia nyumba wazazi wake.

SOMA ZAIDI

Billnass aeleza jinsi mpenzi wake ‘alivyowalinda’ na Nandy

>  Nandy: Nilikuwa na ndoto kufanya kazi na Sauti Sol

> Nandy avunja ukimya kuhusu Ruge Mutahaba

Hana tena ndoto za kupanga chumba Sinza Mori wala Kinondoni Stereo. Furahia mafanikio yake badala ya kuchukia.

Mnashangaa Ajibu kutopita njia alizopita Msuva. Lakini mnapinga Ruby kupita njia alizopitia Nandy. Eti imani yenu ni kuwa Ruby anatakiwa kuigwa na Nandy.

Acheni kulazimisha mtu arudi nyuma kwa kuishi na ndoto za kutumbuiza kwenye tuzo za filamu. Au kujibishana na kina Shetta badala ya kupiga stori kwenye simu na Yemi Alade. Haya mambo ndo yanafanya hii leo Nandy aanze kutegemea kiki kabla kutoa wimbo. Si yeye bali analazimika kuishi watakavyo Waswahili.

Akiwaendekeza Wabongo ‘atalosti’. Diamond anaishi kwa kiki kwa sababu ameishi kwa kiki toka anaanza kutoa singo yake ya kwanza. Sasa Nandy kuanza kutoa ngoma kwa kiki wakati huu ni kama bamia kuharibika uzeeni badala ya kukomaa. Ngoma zote za mwanzo zilizompa jina mbona hakutoa kwa kiki?

Hatutaki kuwazalisha kina Wema Sepetu wengine. Hizi kiki zinachosha na zinakera. Watu wataanza kukereka badala ya kukuchekelea. Kutoa ngoma kwa kiki za penzi ni kuwafanya Wabongo wajinga. Soma alama za nyakati. Usitake kugeuka ghafla kuwa Wema ambaye hashitui tena habari zake.

Kesho, keshokutwa unaweza kuwa na jambo la kuwaambia mashabiki wasilibebe kiuzito kwa imani kuwa ndo yaleyale ya kiki. Usifanye kitu kwa mtazamo wa Manzese, Mwanjelwa, Ngarenaro, Makoroboi, Chumbageni, Kiboroloni wala Kihonda. Tanua soko lako kimataifa kama ulivyoanza na Kenya, endelea mbele.

Kiki hizi na Bilinenga ni kurudi hatua nane baada ya hatua kumi na kujipongeza. Piga pesa dogo kwa kuzifuata huko huko ziliko. Hawa Wabongo wapo tu waheshimu kwa sapoti yao toka unatoka lakini tazama mbele kwa sasa. Mchezo wa kiki ni wa kishamba sasa acheni. Leo wanaongea hivi kesho vile mwisho watakubwaga.

Hakuna jambo gumu kama kusoma talaka. Na hakuna kazi tamu kama kuandika talaka. Wabongo wamekupa njia ya kutoka wape heshima yao. Lakini kamwe usiruhusu wakupe na njia ya kutoweka kwenye ramani. Kwani shingapi bana. Kila siku maisha yanahitaji jambo lingine zaidi. Haya makiki siyo jambo jipya waachie waliofunga ndoa na kiki.

Usiwe miongoni mwa watu wanaokunywa divai nyingi mno, miongoni mwa wale wanaokula nyama kwa pupa. Kwa maana mlevi na mlafi watakuwa maskini, na kusinzia kutamvika mtu matambara. Kwa kuepuka pombe na dawa za kulevya na mazoea kama kucheza kamari, tunaweza kutumia maneno tu kuiandalia familia yetu ya wasanii ifaavyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz