Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NDANI YA BOKSI: Huku Pierre, kule Baba Dai mambo mengi muda hautoshi

50799 Pic+piere

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katikati ya Jiji watu kibao wametota. Nimepaki ndinga niliyoazimwa na mshikaji. Ni kwenye maegesho ya RITA. Eneo ambalo zamani ilikuwa Club Bilcanas. Natupa hatua zangu kijivuni kufuata kilipo kibanda nipate kinywaji baridi. ‘Site senta’ tena. Totoz kibao napishana nazo utadhani Copacabana.

Mara namuona mshikaji tunayekaa mtaa mmoja. Ndani ya gari kwenye maegesho akiwa na jirani yangu mwingine wa kike. Wote hao wana ndoa zao. Mume wa mtu na mke wa mtu. Pozi lao wakilishana ‘aisi krimu’ sikuhitaji ushahidi wa CAG au Kamati ya Bunge ya Maadili kujua kama ni wapenzi.

Moyo uliniuma. Msema kweli mpenzi wa Mungu. Hata mimi kwa yule jirani wa kike nahitaji maombi ya nguvu kumshinda shetani. Akipita mtaani shetani ‘ananigusaga’ bega kama anayetaka nimuambie maneno aliyoambiwa na mumewe mpaka wakaoana. Sikutaka tena kinywaji nikatokomea kuwapa uhuru.

Watu wa leo hujifanya wanajua kujipenzisha kibwege bila woga. Ukiona huwezi kuhimili tashtiti baki njia kuu. Acha kulazimisha uonekane mtoto wa mjini kuchepuka huku nafsi haina ushirikiano. Mademu wa sasa wanadangia mpaka ada za watoto. Hawana huruma.

Michepuko? Ni tatizo kubwa sana hivi sasa. Uaminifu umetoweka kama wapiga picha pale viwanja vya Mnazi Mmoja. Tangu zama hizo walikuwepo wasiojiheshimu. Licha ya kuchepuka kwa siri hadi wachepukaji walipozoeleka na kupiga stori. Zile za enzi zangu nilikuwa hivi, nilikuwa vile. Lakini kwa teknolojia ya leo ukichepuka na beki tatu tu mtaa mzima watajua.

Mbali na teknolojia pia watu wa leo hawana adabu wala soni. Wanajipenzisha kibwege bila hofu wakidhani ni kwenda na wakati. Achana na tashtiti za michepuko baki njia kuu. Acha kulazimisha uonekane mtoto wa mjini kwa kuchepuka. Huo ni ushamba kaka. Na bahati mbaya madem wa hivi sasa nao wanadangia mpaka ada za watoto. Hawana huruma.

Si kwamba wazee walichepuka kwa akili. Hapana ni wazee wapuuzi tu ndo husimulia kuwa mchepuko uliokuwa ukifanya kazi SUKITA au RTC. Eti ndo uliompa akili ya kununua shamba au kujenga nyumba. Sasa anayetegemea akili ya mchepuko ili ajenge nyumba ana akili sawa? Ila wa sasa ndo wapuuzi zaidi huchepuka kindezi ili kuuza nyago ‘Mibs’ Sinza au ‘Tripo Seveni’ Kawe.

Yaani akili kisoda. Yanachepuka kwa kwenda maeneo flan amazing ili yajitwange ‘foto’. Hizo ‘foto’ na ‘mafilta’ kibao wanatupia insta ili wapate madanga mengine. Michepuko ya sasa ipo kwa ajili ya kuteketeza familia ya danga. Hawataki kuolewa na si kuolewa tu hata kuzeeka wanagoma.

Wiki iliyopita kuna mshikaji alipata ajali. Cha kushangaza mchepuko unang’ang’ania kumuuguza. Wakati jamaa ana mkewe, mpaka nikalazimika kubeba msala kwa kujifanya ni mchumba wangu. Baada ya mwenye mali (‘waifu’) kuhoji na kuona litakuwa timbwili wodini. Tumejaribu kushauri lakini haelewi somo.

Michepuko ya sasa kiherehere sana. Kuna jamaa alifanya fujo akalazwa polisi. Mchepuko ukajituma kumtoa kuzidi njia kuu hadi zikapigwa hapo hapo polisi. Wakalazwa wao ndani na jamaa akaachiwa ili akatoe maelezo kwa familia. Hapa tatizo siyo michepuko bali mshikaji kushindwa kuchagua vitu flan hivi mutribu kiakili.

Kuna bwege alishikiwa akili na mchepuko akawa analala huko huko. Na kumdanganya ‘waifu’ kuwa kazini kuna vimeo. Simu zake kaweka ‘pasiwodi’ kama jela ya Guantanamo. Hii ni kwamba hazungushi kwa mchepuko kiasi cha kujiwekea ulinzi .

Kuna michepuko ikikutana na shemeji au wifi ina kiherehere ili wamjue. Na siyo tu hivyo pia wamfagilie. Atataka aonekane yeye ndio anajua zaidi kujali. Washikaji nao ushamba unawasumbua. Unamuacha ‘waifu’ ukapangwe foleni kwa mchepuko? Wengi ni vicheche wahuni ‘wamejisevia’ sana na kupiga chini.

We boya unaona umepata na kuthubutu kumuacha ‘waifu’ na njaa kisa mchepuko ambao wajanja wameshapiga chini. Suala si kuchepuka tu, hata viongozi wa dini wanachepuka. ‘Ishu’ ni unachepuka na dem wa aina gani? Unachepuka ili ikusaidie nini? Usiwaze shepu na sura ya mchepuko, je akili mtambuka ipo kichwani?

Kumbuka tu uzinifu lazima ipo siku utakuacha wazi. Wote wana makosa mwanaume kwenda nje ya ndoa yake. Na mwanamke kujichetua na mume wa mtu. Sasa mbaya zaidi mnapochepuka huku familia zikiteseka. Yaani mnatenda dhambi inayozalisha dhambi zaidi. Chepukeni kwa faida basi.

Demu akiamua kuwa mchepuko ujue kajitoa ufahamu na yuko kimaslahi. Je unakidhi maslahi yake yote? Kama sivyo basi ujue kuna wenzako wengine wanaruka naye nyoka kama kawa. Usijitoe akili zako zote kwa mchepuko kibwege. Watu watakuona bwege la wiki. Jiongeze mjomba. Michepuko ina nguvu, mabwege wengine wanaacha watoto na ‘waifu’ washindie dagaa kauzu. Tena akiulizwa anakuwa mkali, ila nyumba ndogo linawajibika kilofalofa. Likirudi nyumbani baada ya kutoka kuchepuka linamnunia ‘waifu’ utadhani msukule aliyefukuliwa ghafla. Tatizo ni nini?

Likiulizwa linakuwa mbogo na kumtafutia sababu ‘waifu’. Malimbukeni wanaingizwa sana mjini na michepuko. Likitoka kuchepuka linaanza kumchana ‘waifu’, chakula umepikaje. Mwanamke gani huna akili ya biashara? Umesoma lakini aliyeishia darasa la tano anafanya vitu kwa kufikiri kuliko wewe!

Any way kila unayemuoa au kuolewa naye ana udhaifu. Mungu pekee ndiye hana udhaifu. Kila ua waridi unaloliona lina chimbuko lake.

Unayemuoa au kuolewa naye ana historia yake mbaya. Hakuna mtu ambaye ni malaika, acha kuchunguza ya nyuma samehe, sahau, songa mbele.

Hatuwezi kuwa sawa, kuna walio mbele na walio nyuma kidogo. Kupunguza stress, kuwa mtulivu, fanya kazi kwa bidii na kwa muda muafaka ndoto za ndoa yako zitatimia.

Ukishaoa au kuolewa ni kuingia katika uwanja wa mapambano. Kuwa tayari kupambana kuulinda ukanda wa ndoa yako.

Ndoa ni kazi ngumu, jitolee mwenyewe na ufanye kazi ya kuijenga ndoa yako iwe kamilifu. Mungu atakupa mtu ili wewe umtengeneze jinsi wewe unavyohitaji yeye awe. Huwezi jua nini kitatokea baada ya ndoa, hali inaweza badilika, hivyo achia nafasi ya marekebisho. Usikariri yale yale kila siku.

Mapenzi ni gundi ambayo hufanya wanandoa kuwa pamoja daima. Talaka huanzia kwenye mawazo. Hakuna mapenzi rahisi katika ndoa, huwezi kupenda au kupendwa bila kujitoa nafsi yako kwa dhati. Pambania ndoa yako ukimtanguliza Mungu. Ndoa haina jaribio ukiingia, umeingia.

Usione watu wanapita mitaani wanaongea peke yao. Familia zina matatizo sana. Na kwa kiasi kikubwa uhusiano wa mapenzi ni chanzo kikuu. Mapenzi hivi sasa ni kama kunywa bia. Yeyote anaweza kwenda baa akaagiza bia akanywa. Kama atalewa sawa, kama hawezi kulewa atajiondokea zake basi. Hata mapenzi ya leo ndivyo yalivyo.

Ndo maana unaona Pierre Likwidi anageuka gumzo. Kwa maneno yanayojirudia rudia. Lakini watu wanakufa mbavu na kuwasahau kina Joti na wenzao. Hutakiwi kumsifu Pierre bali utambue kuwa sisi wana wa taifa hili tuna msongo sana. Tumetindikiwa kiasi cha kuona faraja maneno ya kawaida kabisa ya Pierre.

Hivi ushajiuliza Pierre anachekesha kwa kipi hasa? Ai mama... Nakufa... iyoooo... Itabaki mawinguni... Konki fayaa. Itabaki kileleni. Everi bade sei yeeeeeeee. Hayo ndo maneno ya kuchekesha mpaka Bunge limesisimka na kudata naye alipokwenda Dodoma wiki hii kweli? Hatuna furaha kama taifa ndo nilichogundua.

Umesikia ya baba yake Diamond Platinumz? Mzee kaona ubwege kuwapiga mizinga watoto. Wakati kile kinachofanya wapate pesa naye anaweza kufanya. Kawaita masela wake kaingia nao studio, katoa ngoma yake. Alichoimba Baba Dai mpaka sasa sijaelewa licha ya kurudia kusikiliza mara mia moja na zaidi. Pamoja na kutoeleweka. Lakini kawa gumzo mitandaoni. Sawa ni kweli kwamba ni baba wa staa lakini mapokeo ya watu juu ya wimbo wake ni kama Pierre vilevile.



Chanzo: mwananchi.co.tz